Wednesday, October 26, 2011

Basi laungua, zaidi ya watu 20 wahofiwa kufa


WATU zaidi ya 20 wanahofiwa kufa baada ya basi la Delux Coach lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kupasuka tairi la mbele kulia, kupinduka na kushika moto kwa zaidi ya saa tatu likiwa Misugusugu mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Ernest Mangu, ajali ya basi hilo namba za usajili T 334 AAD, ilitokea jana saa 9.30 alasiri.

Alisema kwa mujibu wa taarifa za awali, chanzo cha ajali hiyo ni tairi hilo lililosababisha liserereke na kupinduka na kuwaka moto na kuteketeza idadi kubwa ya abiria waliokuwa ndani, ikiwa ni pamoja na dereva.

“Kuna majeruhi 17 waliotoka ndani ya gari na wamekimbizwa katika hospitali ya Tumbi, mpaka sasa hatujapata taarifa kamili ya waliokufa, kutokana na hali ilivyo,” alisema Kamanda Mangu. Hata hivyo taarifa zilizopatikana baadae, zilieleza kuwa majeruhi katika hospitali ya Tumbi, waliongezeka na kufikia 35.

Kwa kawaida ujazo wa basi kubwa ni abiria kati ya 55 kwa basi la viti viwili viwili au Luxury na 65 kwa basi lenye viti vitatu upande mmoja na viwili upande mwingine.

Kamanda huyo alipotakiwa kufafanua juu ya ajali hiyo na iwapo kuna taarifa zozote za ziada, alisema hana taarifa zozote na kuzima simu hali iliyolazimu atafutwe Kamanda wa Kikosi cha Usalama wa Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, ambaye naye hakuweza kufafanua kwa kuwa alikuwa njiani kwenda eneo la tukio.


Hata hivyo taarifa zaidi ailieleza kuwa basi hilo liliondoka Kituo cha Mabasi ya Mikoani Ubungo likiwa na watu 42 tu na haijulikani kama lilipakia watu wengine njiani na majeruhi wengi wako katika hali mbaya.

Kwa mujibu wa tarifa hizo, idadi ya waliokufa imeshindwa kupatikana kwa kuwa miili yao imeteketea kabisa na moto kiasi cha kushindwa kutambulika.

Shuhuda wa ajali hiyo aliyezungumza na gazeti hili, Anna Amani, alisema basi hilo baada ya kupinduka lililipuka na watu waliokuwa ndani kushindwa kutoka na uokoaji kuwa mgumu na hivyo kutoka hao wachache huku wengine wakiteketea.

Alisema basi hilo lililala kiubavu huku likiwaka moto na baadhi ya abiria walitoka kupitia madirishani huku wengine wakishindwa kufanya hivyo na kukutwa na mauti.

“Waliotoka na kuwashuhudia ni wachache sana, wengi wao wameteketea na mpaka sasa basi halijainuliwa zaidi ya kusogezwa pembeni ili kupisha magari mengine yapite,” alisema.

Hivi karibuni zaidi ya watu tisa walipoteza maisha baada ya basi dogo aina ya Toyota Hiace kugongana uso kwa uso na gari aina ya Prado katika barabara ya Tunduma – Mbeya ambapo watu 11 walijeruhiwa.

Pia ajali nyingine mbaya ya majini iliyotokea hivi karibuni na kuua watu zaidi ya 200 waliokuwa wanasafiri kati ya Unguja na Pemba kwenye meli ya mv Spice Islander.

No comments:

Post a Comment