Monday, October 17, 2011

NHC yauza nyumba

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limeanza kuuza nyumba zake likianzia na zilizopo katikati ya Jiji la Arusha.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara wa NHC, David Shambwe alisema nyumba hizo zitauzwa kwa Watanzania wa ndani na nje ya nchi, wenye
mahitaji ya nyumba za makazi.

Bei ya chini kabisa ya kila nyumba ni Sh 175,314,366.48 bila kujumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Ukiongeza asilimia 18 ya VAT bei ya chini kwa nyumba yenye vyumba vitatu ni Sh milioni 200.

Aidha, baada ya mauzo hayo, kwa mujibu wa Shambwe, mnunuzi atakayekabidhiwa nyumba
anaruhusiwa kumpangisha mtu mwingine kwa bei watakayokubaliana, ilimradi tu mpangaji aitumie kwa makazi na sio biashara.

Hata hivyo, bei inaweza kuwa kubwa zaidi ya hiyo kwa kuwa kwa mujibu wa maelezo ya Shambwe, nyumba hizo zitauzwa kwa wateja 30 tu, watakaotangaza dau kubwa katika maombi yao.

Nyumba hizo zenye ukubwa wa meta za mraba 169.45 ziko katika majengo mawili ya ghorofa tatu kila moja yaliyojengwa katika kiwanja namba 565/1 na kwa pamoja yatakuwa na eneo la kuegesha magari 24.

Shambwe alisema kila nyumba ina baraza tatu, tangi la maji la ujazo wa lita 1,000 na kati ya vyumba vitatu vya kulala, chumba kimoja kina choo na bafu ndani.

Sifa nyingine ya nyumba hizo ni kuwa na sebule kubwa, chumba cha kulia, jiko, stoo, bafu na
vyoo vya jumuiya.

Alisema nyumba hizo zinazotambulika kwa jina la Meru kutokana na uamuzi wa NHC kuuenzi Mlima Meru na zitaanza kutumika ndani ya siku 90 kuanzia Oktoba mosi, mwaka huu.

Mkurugenzi huyo aliwataka Watanzania kuanza kutuma maombi yao leo, ili wanunuzi 30 wapatikane na kukabidhiwa.

“Mwisho wa kutuma maombi ni Oktoba 31, mwaka huu, saa 04:00 asubuhi. Nyumba zipo 48
katika maghorofa yetu mawili na ni 30 tu zitakazouzwa kwa sababu 18 zitatumika kwa biashara ya kupangisha.

“Wanaopenda kuzinunua wachukue fomu za maombi katika ofisi zetu za Arusha na kwingineko
au katika tovuti yetu www.nhctz.com,” Shambwe alisema.

Aliongeza kuwa, fomu ya maombi itakayojazwa na kuwekwa sahihi na mteja mwenye dhamira ya kununua nyumba hizo inatakiwa iambatanishwe na barua inayoonesha kiasi ambacho mhusika anaweza kulipa, pamoja na ushahidi wa malipo yasiyorejeshwa ya Sh 10,000, kama ada ya maombi.

“Pamoja na viambatanisho hivyo, mteja anapaswa pia kuambatanisha ushahidi wa malipo ya
awali ya asilimia 10, aliyoyafanya kupitia benki, kulingana na thamani ya nyumba aliyochagua,” alisema.

Baada ya malipo hayo ya awali ya asilimia 10, Shambwe alisema mteja atapewa siku 90 kuanzia tarehe ya barua yake ili akamilishe asilimia 90 ya malipo yaliyobaki, vinginevyo, nafasi ya ununuzi atapewa mtu mwingine.

Hata hivyo, alisema wateja watakaoshindwa kukamilisha malipo hayo katika muda uliopangwa, watarudishiwa asilimia nane tu ya malipo walioyafanya awali ya asilimia 10 na asilimia mbili itakayokatwa itatumika kama gharama ya kumhudumia.

“Endapo mteja hatahitaji kurejeshewa fedha hizo, anaweza kuomba asilimia 10 yake itumike katika ununuzi wa nyumba katika miradi mingine ya shirika hili ambayo hata hivyo, itakamilika ndani ya miezi mitatu au minne ijayo.

“Tukianzia na ule wa nyumba za makazi kwa watu wa vipato vya kawaida wa Ubungo na
Chang’ombe Dar es Salaam, na mwingine wa Arusha, utakaokamilika miezi kadhaa ijayo,”
alieleza.

Alisema mradi huo ambao ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa nyumba 1,500 za NHC, uliogharimu Sh bilioni tano na unategemewa kuliingizia shirika hilo Sh bilioni saba au nane.

“Faida yoyote itakayopatikana itatumika kujenga nyumba nyingine kwa ajili ya makazi bora ya
Watanzania wa kipato cha chini,” alisema Mkurugenzi huyo.

No comments:

Post a Comment