Wednesday, October 26, 2011

Walibya waiomba Nato kukaa zaidi


Mkuu wa baraza la mpito la Libya NTC ametoa wito kwa majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya Nato kuongeza muda wake wa kukaa Libya mpaka mwisho wa mwaka.
Mkuu wa NTC Mustafa Abdel Jalil amesema kuongeza muda huo kunahitajika ili kusaidia kudhibiti silaha za ziada na kupambana na wanaomtii Kanali Gaddafi.
Nato imechelewa kutoa uamuzi rasmi wa lini utamaliza harakati zake nchini humo.
Ilitoa uamuzi wa awali wa kumaliza harakati zake Oktoba 31.
Wanadiplomaisa walitarajiwa kuthibitisha tarehe hiyo siku ya Jumatano.

Bw Jalil aliwaambia mkusanyiko wa watu huko Qatar kwa mataifa yaliyotoa msaada wa kijeshi kwa NTC, "Tuna matumaini kuwa Nato itaendelea na harakati zake mpaka angalau mwisho wa mwaka huu ili kutusaidia sisi na nchi jirani."
Alisema ombi lake lilikusudia "kuhakikisha hamna silaha zozote zinazopenyezwa katika nchi hizo na kuhakikisha usalama wa Walibya kutoka kwa baadhi ya majeshi ya aliyekuwa kiongozi Kanali Gaddafi waliokimbilia nchi jirani".

Bw Jalil aliongeza kuwa NTC lilitaka msaada " kuendeleza ulinzi wa Libya na mifumo ya usalama".
Nato, ambayo ilianza shughuli zake Libya tangu mwezi Machi chini ya azimio la Umoja wa Mataifa kwa minajil ya kulinda raia, ilisema sasa itatoa uamuzi rasmi wa muda wa kukaa nchini humo siku ya Ijumaa.
Msemaji wa Nato Bi Carmen Romero alisema, "kama ilivyokubalika, NATO itaendelea kuangalia hali, na itaendeleza uwezo wake wa kupambana na vitisho vyovyote dhidi ya raia.

No comments:

Post a Comment