Tuesday, August 9, 2011
Spika amtwisha Zitto Kabwe zigo la UDA
SAKATA la kuuzwa kwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) limezidi kugonganisha vichwa vya mamlaka mbalimbali, baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuhamisha mchakato wa uchunguzi huo kutoka Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwenda Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).Utata wa uuzaji wa shirika hilo umesababisha pia mvutano mkubwa kati ya wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam na Meya wa jiji hilo, Dk Didas Masaburi ambaye wiki iliyopita aliwashambulia wawakilishi hao kwa maneno makali huku akitoa vitisho kwamba atalipua tuhuma zao za ufisadi.
Makinda aliikabidhi jukumu hilo POAC Ijumaa ya Agosti 5, Spika na kuliondoa Kamati ya Miundombinu ambako Profesa Juma Kapuya ambaye ni mmoja wa wajumbem, ana maslahi na UDA kutokana na kuwa mmoja wa wanahisa wa Kampuni ya Simon Group.
Kaimu Katibu wa Bunge John Joel alithibitisha jana Spika amefanya mabadiliko hayo na kwamba tayari Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe amekwishapewa taarifa. "Ndiyo, kimsingi kamati inayopaswa kuchunguza ni Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma na tayari Spika ametoa uamuzi huo na maelekezo kwa kamati husika," alisema.
Tafsiri ya uamuzi wa Spika
Uamuzi huo wa Spika pia unaonekana kutengua ule wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye wakati akitoa kauli ya Serikali kuhusu UDA alisema, ingeshirikiana na Kamati ya Serukamba (Peter, Mwenyekiti Kamati ya Miundombinu). Kiutendaji, jukumu la ubinafsishaji ni la POAC kama ilivyofafanuliwa katika nyongeza ya 8 ya kanuni za Bunge, ibara ya 13 (e).
Vyanzo vya habari vilifafanua kwamba kama uchunguzi huo ungeachwa chini ya Kamati ya Miundombinu kungeibuka mgongano wa kimaslahi kutokana na ubia wa Profesa Kapuya na Simon Group, iliyonunua shirika hilo.
"Uamuzi wa Spika kuhamisha jukumu hilo kutoka kamati ya miundombinu kwenda POAC umelenga kuondoa mgongano wa kimaslahi, kule kuna Kapuya ambaye ni mbia wa Simon Group kwa hiyo kitendo chochote cha uchunguzi kufanywa na miundombinu kingeathiri mchakato huo, " kilifafanua chanzo hicho.
Kauli ya Zitto Kabwe
Kwa upande wake Zitto akifafanua jukumu hilo zito alilotwisha alisema kimsingi kamati yake ndiyo yenye dhamana na ubinafsishaji na kuweka bayana kwamba ataunda kamati ndogo kutokana na uwiano wa vyama na Dar es Salaam kupewa mbunge mmoja.
Alifafanua kwamba, kutoka Dar es Salaam atapaswa kumchagua mbunge mmoja kuingia katika kamati hiyo ndogo huku pia kukiwa na wawakilishi kutoka CUF, NCCR-Mageuzi na CCM.
Alisema ataunda kamati kwa kuzingatia maeneo ya msingi ambayo wajumbe pia wataweza kutoka Katiba na Sheria kwani jambo hilo ni la kisheria, Kamati ya Miundombinu, Serikali za Mitaa kutokana na kugusa Halmashauri ya Jiji na wengine POAC.
Alisema tayari amepata taarifa kutoka Ofisi ya Bunge kuhusu agizo hilo lakini anasubiri taarifa rasmi zitakazomwelekeza namna mchakato huo unavyopaswa kufanywa hadi kukamilika.
"Nimeambiwa lakini sijapata barua rasmi, nasubiri taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Spika. Lakini, kimsingi jukumu la ubinafsishaji liko chini ya kamati yangu ya mashirika ya umma," alisema Zitto, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni.
Zitto alisema kama atapata taarifa rasmi hadi jana jioni, leo atatangaza kikosi kazi chake hicho ambacho kitafanya uchunguzi huo kwa undani kuona mchakato mzima ulivyo.
Mpango wa kuizima POAC
Vyanzo vya habari vilidokeza kwamba kumekuwa na juhudi za makusudi kuhakikisha suala hilo linabaki Kamati ya Miundombinu na kuzuia lisifike POAC, ili kulizima 'kiana'.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, baadhi ya wahusika wanataka kutumia mwavuli wa Kamati ya Miundombinu ambayo ina baadhi ya wajumbe wenye maslahi na Simon Group kuzima suala hilo huku pia wakitumia mwavuli wa uchunguzi uliotangazwa na Pinda.
Zitto alipoulizwa kuhusu mpango huo Zitto alisema hakuwa akiufahamu kwani mamlaka ya kuunda kamati na majukumu yake ni jukumu lililo chini ya Spika kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.
Alisema hata kama Waziri Mkuu ametangaza uchunguzi, bado Bunge likiwa mhimili huru wa dola linapaswa kufanya uchunguzi wake. Alisema uchunguzi wa Serikali na vyombo vyake ni wake lakini Bunge nalo linapaswa kufanya uchunguzi wake huru kuhakikisha linapata kile ambacho linataka.
"Uchunguzi wa Serikali ni wa kwao serikalini lakini Bunge nalo uchunguzi wake ni wake. Kwa hiyo hata kama Serikali inachunguza bado Bunge nalo halifungwi kufanya uchunguzi wake, " alisema.
Utata wa uuzwaji wa shirika hilo uliibuka baada ya Dk Masaburi kufumua menejimenti ya shirika hilo. Suala hilo lilifika bungeni baada ya kuibuliwa wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2011/12, ambayo wabunge wengi waliochangia walionekana kustushwa na uuzwaji wake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment