Wednesday, August 10, 2011

Wauza mafuta wabanwa, watakiwa kujieleza


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetaka kampuni nne kubwa za kuuza mafuta kuanza usambazaji na uuzaji wa mafuta hayo mara moja na kuzipa saa 24 kujieleza kwa nini zisichukuliwe hatua kwa kuvuruga mfumo wa usambazaji mafuta nchini.

Hayo yalibainishwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Dar es Salaam na kutaja kampuni hizo kuwa ni Engen Petroleum Tanzania Limited, BP Tanzania Limited, Oil Com na Camel.

Hatua hiyo ilikuja huku Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati, Januari Makamba, akiomba Bunge liahirishe mambo yote na kujadili suala la mafuta ya petroli nchini kama jambo la dharura.

Baada ya Bunge kuridhia, wabunge walichangia kwa uchungu juu ya wafanyabiashara ya mafuta kuendesha mgomo wa kuuza bidhaa hiyo na kusababisha usumbufu kwa wananchi.

Makamba aliomba mwongozo na kutoa hoja ya dharura kuhusiana na suala la mafuta akisema hadi jana asubuhi, karibu nusu ya vituo nchini vilikuwa zimefungwa ama kutokana na uhaba wa bidhaa au mgomo wa wafanyabiashara.

“Nchi imesimama, watu hawaendi kazini, biashara zimesimama. Ni jambo kubwa na ni hali ya hatari kwa uchumi na usalama wa nchi. Naomba suala hili lijadiliwe na Serikali itwambie tumefikaje hapa na tunaondokaje kwa sababu Watanzania wako katika shida kubwa,” alisema Makamba.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi, na hivyo kumfanya Naibu Spika, Job Ndugai kubariki hoja hiyo ijadiliwe, huku ile ya Wizara ya Viwanda na Biashara iliyokuwa imesomwa na kuingia katika kipindi cha majadiliano kuweka kando kwa muda.

Makamba alikazia hoja yake kwa kusema kuwa, mgawo wa umeme ni adha na kufananisha suala la mafuta kuwa ni sawa na kiyama kwa nchi.

“Hali ni mbaya, naiomba Serikali itoe makucha yake, hali ya mafuta irejee kawaida kufikia leo (jana) jioni au kesho asubuhi…tuiokoe nchi, kama hata jenereta na minara ya simu haviwezi kupata mafuta, nchi itasimama…nasema hivi kwa sababu wiki nzima Serikali imekaa kimya, huku wananchi wakiteseka … jamani hali ni mbaya,” alisema.

Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, aliwataka wafanyabiashara wa mafuta kuanza kuuza mafuta haraka na kushauri, endapo ingefika saa 12 jioni (jana), wafanyabiashara wanyang’anywe leseni.

Alitaka pia kama watafanya ubishi, askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) liruhusiwe kuvifungua vituo hivyo ili mafuta yapatikane.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alihoji kitendo cha Shirika la BP nalo kugoma kuuza mafuta, licha ya kuwa serikali ina hisa asilimia 50 na bado imekuwa kimya.

Kutokana na hofu ya mafuta kuendelea kuiyumbisha nchini, Mnyika alisema Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuchukua hatua kumaliza tatizo la mafuta, na ana ushahidi kwamba, baadhi ya maofisa wa Serikali wanahusika katika suala hilo kwa kuwa wamehongwa.

Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango-Malecela, alisema wafanyabiashara wa mafuta wasidhani kwamba wako juu ya sheria na wanapaswa kuiheshimu Serikali.

Mbunge wa Mkanyageni, Mohammed Habib Mnyaa (CUF), aliunga mkono kauli ya Zitto kwamba, wafanyabiashara wakiendelea kugoma kuuza mafuta, JWTZ iingilie kati na kusema, kuna taarifa kwamba viongozi wa Serikali wanafanya biashara ya mafuta, hivyo tatizo la sasa liwe fundisho kwa Serikali.

Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama (CCM), naye alikuwa mkali akiitaka Serikali kuhakikisha inamaliza tatizo la mafuta, vinginevvyo haitaheshimiwa. Tundu Lissu (Chadema), alisema ukaidi wa wafanyabiashara hao hauna tofauti na uhaini.“Huu ni uhaini, kampuni za mafuta zimetuwekea bastola kichwani…wanataka kuhujumu uchumi wa nchi, kama haziwezi kufuata taratibu, serikali isipepese macho…ichukue hatua zote,” alisema.

Ismail Rage wa Tabora Mjini (CCM), alilitaka Bunge kurudisha sheria ya watu kuwekwa kizuizini, ili watu wenye nia mbaya na nchi kama wafanyabiashara wanaozuia mafuta wawekwe huko kama sehemu ya adhabu.

Akijibu hoja hizo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema adha wanayoipata Watanzania kwa sasa kutokana na kukosekana kwa mafuta haina uhusiano na uhaba wa mafuta, akisema hadi Jumamosi iliyopita nchi ilikuwa na akiba ya lita milioni 191 za mafuta ya aina mbalimbali.

Kwa upande wa Masebu alisema tangu jana Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) liliomba leseni ya biashara ya mafuta, ili kuanza kusambaza mafuta hayo mara moja na kuongeza kwamba kuna shehena kubwa ya mafuta inakuja ambayo alisema itarekebisha hali hiyo.

Alisema ni kosa kisheria katika biashara ya soko huria, wafanyabiashara kukaa na kupanga bei na akasema wana taarifa muhimu kutoka kwa baadhi ya kampuni kubwa kufanya mawasiliano juu ya misimamo ya pamoja ya kupanga bei za mafuta, tofauti na bei elekezi kutoka Ewura.

Masebu alisema amri ya Ewura ni sawa na hukumu ya Mahakama Kuu, hivyo kuwataka wafanyabishara hao kutekeleza hukumu hiyo mara moja, kabla hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao. Alisema kimsingi suala la kushusha bei linalogombaniwa na kampuni hizo ni kisingizio, kwa vile tangu mwanzo fomula iliyotumika mwaka 2008/09 ni ile ile iliyotumika katika punguzo la sasa na kwa makubaliano, lakini akasema kinachowabana ni baada ya kudhibiti mianya yote ya kujiongezea kipato haramu.

Alikiri kwamba kwa sasa hali ni tete, lakini akasema haijafikia hatua ya kutangaza hali ya hatari ambayo inaweza kuchukuliwa na Waziri mwenye dhamana - Waziri wa Madini na Nishati.

Alisema miaka mitatu iliyopita, Ewura ilikuwa ikiwaongeza wafanyabiashara hao asilimia 7.5 kwa kila tozo iliyokuwa ikifanywa na mamlaka nyingine, ikiwemo Ewura yenyewe, ili kuondoa uwezekano wa kupata hasara kutokana na ununuzi katika soko la dunia, lakini baada ya kulifanyia kazi, walibaini kwamba hakuna haja hasa baada ya kufanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa hakuna hasara zaidi ya kuwaongeza faida.

Hata hivyo, alisema hivi sasa asilimia 7.5 imebaki kwa gharama za msingi za kununulia mafuta kutoka soko la dunia, hivyo baada ya kutoa punguzo hilo dogo, wafanyabiashara wamejikuta hawana tena mianya ya kupata faida ya ziada ya pembeni.

Alisema: “Hivi sasa Ewura inafanya kazi kwa weledi, uaminifu na uzalendo, jambo ambalo limewapa shida, kwani hakuna uchakachuaji uliokuwa unawafanya wapate fedha nyingi zisizo halali”.

Alipoulizwa ni kwa vipi BP ambayo serikali ina hisa asilimia 50 nayo ni miongo mwa kampuni zinazochukuliwa hatua, Masebu alisema wameichukulia kampuni hiyo kama mmoja wa wabia katika biashara ya mafuta na si vinginevyo.

“ Sisi tunaichukulia BP kama mmoja wa wabia katika biashara ya mafuta, tunatarajia ifuate sheria na kanuni za biashara tulizojiwekea, hivyo ikikiuka kanuni hizo, inachukuliwa hatua kama mfanyabiashara mwingine yeyote,” alisema Masebu.

Mkurugenzi wa Mafuta Ewura, Sirily Masei, alikanusha kuwapo upungufu wa mafuta kama inavyodaiwa sasa na baadhi ya kampuni kwa kile alichodai ukaguzi uliofanywa Agosti 5 ulionesha kuwapo shehena ya petroli ya siku 40 na dizeli kwa siku 38. Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Titus Kaguo, alisema mbali na sababu zilizotajwa hapo juu, suala la kuweka vinasaba kwa njia ya kisasa kwenye mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, ili kubaini uchakachuaji limechangia kwa kiasi kikubwa kuwabana wafanyabiashara wasio waaminifu.

No comments:

Post a Comment