Wednesday, January 4, 2012
Ajali ya Upendo yaua wawili
ABIRIA wawili wamekufa papo hapo na wengine 29 kujeruhiwa na baadhi yao kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, baada ya basi la Upendo Travel Coach walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Iringa kupinduka eneo la Doma, Wilaya ya Mvomero, Barabara kuu ya Morogoro- Iringa.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 10 jioni jana eneo la Kijiji cha Doma, Wilaya ya Mvomero, Morogoro kwa kuhusisha basi lenye namba za usajili T 510 AMZ aina ya Scania na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine 29 miongoni mwao wakiwemo watoto wadogo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba chanzo chake ni baada ya lori moja ambalo lilikuwa likitaka kulipita jingine na hivyo kutaka kugongana uso kwa uso na basi hilo.
Hata hivyo alisema, maiti moja imetambuliwa kwa jina la Hamis Mbwana (26) mkazi wa Handeni mkoani Tanga na kwamba alitambuliwa baada ya kupekuliwa nguo alizovaa na kukutwa na leseni yake ya udereva ikiwa na jina hilo.
Hata hivyo karibu majeruhi wengi walikuwa ni wanafunzi wa Vyuo na Shule za Msingi, ambao walikuwa wakirejea vyuoni na shuleni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo, Firbert Nyoni, Maneno Abdallah , Maserina Mwagessa, Jestina Lema, Aline Mhina pamoja na Salum Mfaume, walisema kuwa juhudi za dereva wa basi kulikwepa lori iliwezesha kuokoa maafa makubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Mfaume aliyeunguzwa maji ya rejeta tumboni na mgongoni ambaye alikuwa wodi ya majeruhi namba moja katika hospitali hiyo, alisema malori hayo yalikuwa yakifukuzana kwa mwendo kasi.
“Juhudi za dereva wa basi ndizo zimewezesha kupunguza vifo na majeruhi…lakini wenye malori walikimbia baada ya sisi kupatwa na ajali hii…na mimi nimeungua sana mgongoni na tumboni,” alisema majeruhi huyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment