Wednesday, January 4, 2012

Mabasi zaidi ya 50 yaendayo mikoani yazuiwa Ubungo

MABASI zaidi ya 50 yaendayo mikoani, jana yalishindwa kufanya safari zake na kusababisha usumbufu na vurugu kutokana na mamia ya abiria kushindwa kusafiri kama walivyopanga.Vurugu hizo ambazo zilizuka pia katika miji ya Moshi na Arusha, zilisababishwa na kubainika kwa baadhi ya madereva wa mabasi hayo kutokuwa na leseni mpya.

Sakata hilo jijini Dar es Salaam lilitokea katika Kituo Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani, kilichopo Ubungo ambapo abiria wa kwenda Arusha, Moshi, Morogoro, Iringa, Mbeya, Mwanza, Singida, Dodoma, Songea na Mtwara yalikwama.

Kutokana na kuharibiwa ratiba zao za kusafiri kundi kubwa la abiria wenye hasira  lilianzisha vurugu na kutahamaki kwa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani waliokuwa wakikagua leseni hizo na kuwalaumu kwa kuwasababishia usumbufu wa usafiri.

Abiria hao wenye jazba walikuwa wakitoa maneno makali na kushinikiza kurudishiwa fedha zao kama usafiri haupo na wengine kuwazomea baadhi ya maofisa wa usalama waliokuwa wakiendesha zoezi hilo la ukaguzi.

Hata hivyo wakati zoezi hilo likiendelea, hali ilikuwa tete kwa abiria wengi waliokuwa na tiketi tayari baada ya kukosa msaada wowote kutokana na baadhi ya ofisi za mabasi  walizokuwa wamekatia tiketi hizo kufugwa na wahusika kutoonekana katika maeneo hayo.
Zoezi hilo pia limedaiwa kusababisha usumbufu kwa abiria wengi kutokana na wengi wao kutokuwa na taarifa yoyote juu ya msako huo na mpaka majira ya saa 5 asubuhi ,magari yaliyotarajiwa kuondoka saa 12 alfajiri yalikuwa hayajaondoka kituoni hapo.

Wakati hayo yakitokea baadhi ya madereva wa mabasi walibuni mbinu kwa  kukodi  baadhi ya madereva wa daladala na pikipiki  waliokuwa na leseni hizo mpya  ili kuweza kuonyesha na kuruhusiwa kuondoka.

Akizungumza kwa masikitiko mmoja wa abiria,  Mustafa Muddy aliyekuwa anasafiri  kwenda Mwanza kwa gari la Super Najmnisa alisema wamesikitishwa na hali hiyo kwani hawaelewi watasafiri lini na wengi wao ni wafanyakazi wanarejea katika vituo vyao vya kazi.
“Serikali ilitakiwa iangalie utaratibu mzuri wa kufanya kwani kuyazuia magari asubuhi wakati abiria wamekwisha  wasili kwa ajili ya safari siyo vyema , ukizingatia kosa si la abiria ni la madereva na matajiri wao,” alisema Muddy.

Aidha baadhi ya madereva walilalamikia usumbufu huo na kusema zoezi hilo ni la kupoteza muda kwani mamlaka husika haiwajibiki ipasavyo kwa kukagua leseni hizo kama ni halali au ni feki.
“Hawa wanafanya kazi bure, wenyewe wanaangalia jina na picha katika leseni lakini hizi leseni zipo feki na pia wapo ‘Madeiwaka’ wasio na uzoefu” alilalamika Victor Mhavile.

Aidha walisema utaratibu  uliowekwa ni mgumu kwani madereva hao wanatakiwa kwenda kusoma  upya na chuo kilichochaguliwa kutoa elimu ni kimoja tu cha usafirishaji (NIT) ambacho uwezo wake wa kupokea wanafunzi ni mdogo.

Naye,  Mkurugenzi Mtendaji wa mabasi ya Al  Saedy,  Ibrahim Hawadhi alisema utaratibu wa kukagua mabasi siyo mbaya ila una upungufu mwingi ambao unasababisha athari kubwa kwa abiria na wahusika wote.

“Hatukatai  agizo la serikali lakini walipaswa wazingatie baadhi ya mambo kwani wapo madereva wenye barua za uthibitisho  na risiti za malipo ya leseni hizo ambao  hawajazipata kutokana na utaratibu uliopo kwani ni wa muda mrefu sana.

Na kuongeza kuwa hao wenye uthibitisho wa barua hizo walipaswa waruhusiwe kuondoka na magari hayo kwani barua hizo ni uthibitisho tosha kuwa wanastahili kuwa na leseni hizo”, alisema Hawadhi.

Aliongeza kuwa serikali pia inapaswa kuangalia uzoefu walionao baadhi ya madereva na siyo kuangalia  elimu ya dereva kwani kuna madereva waliosoma kwa muda mfupi lakini hawana uzoefu, hili litasababisha ajali nyingi.

“Madereva wanaoweza kuendesha mabasi vizuri ni wale wanaoendesha magari makubwa ya mizigo na malori siyo wa magari madogo kama daladala na nyinginezo kama wanavyofanya, waangalie dereva  atakayeweza kuepusha ajali na siyo leseni tu,” alisema Hawadhi.
Naye, Ofisa  Msimamizi wa Ukaguzi huo, Kanda  ya Dar es Salaam, Prakson Rugazia alisema zoezi hilo ni endelevu na kama kuna watu wa kulaumiwa ni wamiliki wa mabasi kwani taarifa za ukaguzi walipewa tangu muda mrefu.
“Maagizo yalitolewa muda mrefu, kama wameshindwa kutekeleza muda wote wa miaka 3 hilo ni tatizo lao, na kuongeza kuwa sheria ya kuwalinda abiria walioachwa bila kusafiri ipo na itawalinda” alisema Rugazia.

Aliongeza kuwa serikali ilitoa  muda wa kutosha  ila  wahusika walishindwa kuutumia ipasavyo ,hivyo isilaumiwe kwani wao wameamua kutekeleza  sheria iliyowekwa na kitakachofuata ni wamiliki hao kutozwa faini na  kufungiwa. Alisema waliotoa magari kinyemela wanajisumbua kwani kila kona maaskari watafanya ukaguzi.

Serikali ilitangaza  mchakato wa kubadilisha  leseni  tangu mwaka 2007 na ilitoa muda wa kutosha kwa wahusika kufanya marekebisho hayo kutokana na kukithiri kwa leseni feki za awali.

No comments:

Post a Comment