WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amesema CCM katika mchakato wake  maarufu wa kujivua gamba, haina budi kurudia zama za TANU na kupiga vita  tabia inayoota ya kununua 
madaraka wakati wa uchaguzi.  
Pia ameitaka Serikali iachane na nyongeza ya posho za wabunge kutoka  Sh 70,000 kwa siku mpaka Sh 200,000 kwa kuwa suala hilo linaweza  kumweka pabaya hata Rais.  
Sumaye alisema hayo kupitia kipindi cha televisheni ya ITV cha  Dakika 45 kilichorushwa juzi usiku, alipokuwa akizungumzia mambo  mbalimbali ya chama na Serikali kwa Tanzania na Afrika.  
Kujivua gamba “CCM iliamua kwa nia njema kuwa kuna tatizo la rushwa  na ufisadi na kuwataka waliokiingiza chama katika aibu ya kutumia rushwa  wajiondoe wenyewe…tafsiri yake ni 
magamba yajiondoe yenyewe,” alisema Sumaye. 
Alisema kama kati ya waliotakiwa kujivua magamba katika ngazi  tofauti za chama hicho wako waliokataa, kazi ya chama kwa sasa ni  kuwashughulikia.  
“Kama kuna gamba limeng’ang’ania, basi apatikane mtu wa kulivua kwa  nyuma … CCM ina watu jasiri wa kuyatoa hayo makoti (magamba), tunajua  yana fedha na dhahabu lakini yakitoka hayana nguvu,” alisema Sumaye. 
Alifafanua kuwa kama mtu anatumia rushwa kupata cheo, akiondolewa katika hicho cheo, 
maana yake hatakuwa na pa kumfanya atumie rushwa. 
“Rushwa ni balaa katika uchaguzi, hatuwezi kuchaguana kwa rushwa, lazima turudi enzi za 
TANU, hakukuwa na ‘bahasha’ katika uchaguzi,” alisema na kuongeza kuwa CCM haijapambana 
vizuri na rushwa.  
Alifafanua kauli hiyo kuwa katika mapambano ya rushwa, kumejitokeza  kambi mbili; moja ya wanaojiita wapambanaji wa rushwa wanaodaiwa kutaka  kuiondoa kambi nyingine katika 
ushindani. 
Alihoji kwa nini hiyo kambi inayopigwa vita haisimami hata siku moja na kusema inapiga vita 
rushwa na badala yake jamii inashuhudia nguvu kubwa ikijaribu kunyamazisha wanaopambana na rushwa. 
“Rais Kikwete (Jakaya), aliikuta rushwa na ataiacha, tunapaswa kuendelea kupambana na 
wanaonunua madaraka, mtu akiingia serikalini kwa kununua madaraka, atatafuta fedha 
kununua tena kwa bei ya juu na si kuhudumia wananchi. 
“Hali ni mbaya na watu wakati wa uchaguzi wamefikia hatua ya kuita wakati wa mapato, kwa 
namna hii Taifa litakwisha,” alionya na kuongeza kuwa watu wamechoka  na kama CCM ikishindwa iseme na wananchi wataiondoa madarakani.  
Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema anatarajia 
kazi ya kujivua gamba itafanikiwa na katika uchaguzi ujao wa ndani wa CCM utakaofanyika 
mwaka huu, hakutakuwa na vitendo vya rushwa kama ambavyo imekuwa ikifanyika. 
Posho na hatari kwa uongozi  
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu nyongeza ya posho za wabunge,  Sumaye alisema kwanza suala hilo halijaeleweka vizuri kwa kuwa  kumejitokeza 
kupingana kati ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, huku Ikulu ikiwa kimya.  
“Kama unataka kuwa mwanasiasa mzuri, unaposimamia kitu cha maslahi yako kinachokera 
wananchi, ujue umekosea,” alisema Sumaye.  
Hata hivyo alionya kuwa ikiwa Serikali itabariki nyongeza hiyo ya  posho, kesho yake walimu nao watataka posho na baadae watafuata  wanajeshi na ikifikia huko hata Rais wa nchi hatakuwa sehemu salama.  
Alikumbusha kuwa baada ya miaka mitano ya kwanza ya uongozi wa Rais  wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, wakati wa kipindi cha pili alipotakiwa  kuendelea kuwa Waziri Mkuu mwaka 2000, alikataa kwa kuwa alizuia  nyongeza ya posho kwa wabunge.  
“Nilimwambia Rais Mkapa, usinipe hicho cheo kwa kuwa kule bungeni  hawanipendi nilizuia posho zao, akaniambia nenda nikakosa la kufanya,”  alisema Sumaye.  
Alionya kuwa suala la posho linapukutisha mapato ya Serikali kwa kuwa hata watumishi wa 
umma wameamua kuhamishia makongamano mahotelini, kila kukicha  kulipana posho na kusababisha mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato  (TRA) kutoonekana yakifanya kazi.  
Harakati za urais  
Alipoulizwa kuhusu maneno yanayosemwa mitaani kuwa ana nia ya kugombea Urais wa 
2015, Sumaye alisema hajaamua kufanya hivyo na siku akiamua, atatangaza. 
“Urais lazima usubiri wakati ukifika ujipime kama unaweza na kama Watanzania wanakuhitaji 
kwa nini usigombee? 
“Kuwania urais si jambo baya hata ukitangaza leo, kwanza unaelezea  mipango yako ya muda mrefu,” alisema na kuongeza kuwa haramu ni kutaka  kumuondoa rais aliyepo madarakani au kupita pita kujaribu kufanya nchi  isitawalike. 
Umiliki wa mashamba Morogoro  
Alipotakiwa kufafanua kuhusu mashamba anayomiliki Morogoro, kwamba anadaiwa alipora 
wananchi ambao sasa hawana ardhi, alisema shamba hilo la hekta 300 halikuwa la wanakijiji. 
Alifafanua kuwa shamba hilo, lilikuwa likimilikiwa na Chama cha Ushirika ambacho kililitoa 
kama rehani ili kupata mkopo.  
Kwa mujibu wa Sumaye, chama hicho kilishindwa kurejesha mkopo na mdai akataka 
kulichukua, kikaona ili kuepuka hasara ni bora kuliuza. 
“Sasa mimi kununua kitu kinachouzwa ni kosa?” Alihoji na kuongeza kuwa hata madai 
kuwa ameliacha pori si ya kweli kwa kuwa kuna majani ya mifugo  ambayo wanaoyaona wanadhani ni pori wakati hayatoshi kulisha mifugo  yake.
No comments:
Post a Comment