JAMBAZI sugu mkoani Arusha anayetambuliwa kwa jina la Pokea Samsoni, amemuua askari kanzu kwa risasi ya shingo na kumjeruhi Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha (OC-CID).
Mauaji hayo yalifanyika jana saa 10 alfajiri katika Kijiji cha Nambala katika eneo la Shangarai
wilayani Arumeru mkoani Arusha wakati jambazi huyo alipokuwa akijaribu kuwakimbia polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye alimtaja askari aliyeuawa kuwa ni Konstebo Kijanda Mwandu mwenye namba F. 2218.
Kamanda Andengenye alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa nyumba inayomilikiwa na mkazi wa eneo hilo aliyejulikana kwa jina moja la Agnes, inahifadhi majambazi.
Alisema walielekezwa kuwa nyumba hiyo ipo barabara ya Peace Point eneo la Shangarai na
ndipo walipojipanga na kwenda kufanya upekuzi na hatimaye kuwakamata watuhumiwa hao
wa ujambazi.
Andengenye alisema askari walipofika karibu na eneo la nyumba hiyo, jambazi hilo liliwahi
kuwaona na kuanza kurusha risasi ovyo hewani na kwa bahati mbaya risasi moja ikampata
huyu Konstebo Kijanda akafa papo hapo na nyingine kumpata OC-CID, Faustine Mafwele
kwenye bega la kushoto.
Kamanda Andengenye alisema kuwa Mkuu huyo wa Upelelezi amelazwa hospitalini kwa matibabu.
Baada ya hapo jambazi hilo lilitoroka na msichana Agnes Silasi ili kuficha maovu yao katika eneo hilo na katika upekuzi katika nyumba hiyo walikuta risasi 36 za SMG, risasi 12 za shotgun, kitako kimoja cha shotgun, mtutu mmoja, mtambo mmoja wa bunduki ya shotgun na soksi za kuvaa usoni nyeusi mbili.
Baada ya hapo polisi iliwakamata watoto wawili; Daines Msawe (9) mkazi wa Nambala na
Allex Parumina (13) mkazi wa Nambala ili kuwahoji kwa sababu mmoja wa watoto hao ndiye
aliyemfungulia mlango jambazi huyo na kutoka nje kufanya mashambulizi dhidi ya Polisi.
“Kuanzia sasa polisi mkoani Arusha imetangaza donge nono la shilingi milioni 5 kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa jambazi huyo.
No comments:
Post a Comment