KUNDI la kigaidi nchini Somalia lenye uhusiano na al Qaeda, la al  Shabaab limetishia kufanya mashambulizi Tanga na Kilimanjaro na tayari  vyombo vya usalama mkoani Kilimanjaro, vimetoa hadhari katika maeneo ya  viwanda vinavyoweza kushambuliwa. 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Absalom Mwakyoma, alithibitisha kuwapo  kwa tishio hilo lakini alikataa kuzungumzia zaidi kwa madai ni la  kiusalama zaidi. 
“Hilo jambo lipo lakini sitalizungumzia, kwani ni mambo ya kiusalama  zaidi…wewe nani amekupa taarifa hizo, muulize aliyekwambia  akufafanulie,” alisema. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Mtendaji Utawala wa  Kiwanda cha Sukari cha TPC, Jaffary Ali, wamepewa taarifa za kuchukua  hadhari juu ya kuwapo kwa tishio la shambulio kiwandani hapo.  
Alisema taarifa hizo zimetolewa na Kamanda Mwakyoma baada ya kupata  taarifa mbalimbali za kiusalama zilizopatikana juu ya kuwapo kwa tukio  hilo.  
“Ni kweli tumepata taarifa za kuwapo kwa shambulio la kikundi cha al  Shabaab lakini haijataja moja kwa moja kwamba sisi ndio tunashambuliwa  ila tumetakiwa kujihadhari na watu, magari na hata pikipiki,  tusizozifahamu,” alisema.  
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda Mwakyoma, huenda kikundi hicho  kikatekeleza mashambulizi yao kwa kutumia pikipiki, jambo ambalo  linasababisha kutilia shaka vyombo vyote vya usafiri vinavyopita  kiwandani hapo. 
Alisema kutokana na taarifa hizo, tayari kiwanda kimetoa hadhari kwa  wafanyakazi wake, viongozi wa vijiji vinavyozunguka kiwanda pamoja na  familia za wafanyakazi kuwa makini 
dhidi ya watu wasiowafahamu.  
“Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda, kwa Tanga kimetajwa kiwanda cha  saruji, lakini huku kwetu tumehadharishwa katika maeneo haya ya viwanda,  kwani ndiyo lengo lao, tumewataka wafanyakazi wasiwe na hofu, lakini  pia tunaendelea na kazi,” alisema. 
Alisema menejimenti imeimarisha ulinzi katika eneo la kiwanda,  lakini pia imeagiza mbwa maalumu wa kutambua mabomu kutoka Arusha ili  kusaidia ukaguzi wa maeneo yote.  
Alisema wafanyakazi wa mashambani wamepewa taarifa kuhusu ubebaji miwa, kwani huenda 
wakabeba bomu na kuliingiza kiwandani, iwapo kikundi hicho kitatega kupitia mashamba. 
"Hawa mbwa tulioagiza watafanya doria maeneo yote ya kiwanda na mashamba kutokana na 
hofu kwamba wakitumia mashamba ni rahisi kuyabaini," alisema.  
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha TPC,  waliojitambulisha kwa jina moja la Mziray na Juma, walisema tishio hilo  limeleta hofu, kwani athari za mashambulizi ya kikundi hicho ni makubwa.   
Alisema wameshuhudia mara kadhaa kupitia vyombo vya habari, katika  nchi za Kenya na Uganda, jinsi ambavyo vimeshambuliwa na kikundi hicho  na kusababisha vifo vya mamia ya wananchi wasio na hatia.  
"Hili tishio limetulazimu kuhamisha baadhi ya wanafamilia wetu, tumewataka waende mjini 
Moshi kuishi na ndugu," alisema.  
Akizungumzia taarifa hizo, mkazi wa kijiji cha Langasani wilayani  Moshi vijijini, Abdul Sultan, alisema ni vyema Serikali ikaimarisha  usalama katika mipaka ili kudhibiti kikundi hicho. 
Alisema pamoja na suala la mipaka ya nchi, lakini pia zipo sababu za  msingi kwa wananchi kupewa elimu ya utambuzi wa watu wenye nia ovu ili  iwasaidie kukabiliana na watu hao. 
Kikundi cha al Shabaab kimekuwa kikifanya vitendo vya ugaidi ndani  ya Somalia, Uganda na Kenya hata kulazimu majeshi ya Kenya kuingia  nchini Somalia kukabiliana nacho.
No comments:
Post a Comment