Friday, January 6, 2012

Majambazi wavamia uwanja wa ndege Geita

Salum Maige, Geita
MAJAMBAZI matano yakiwa na silaha za kivita huku wakiwa wamevalia kijeshi jana yaliuteka uwanja wa ndege wa mgodi wa dhahabu wa Geita mkoani Mwanza na kuugeuza kuwa wa kivita kufuatia mapambano kati yao na walinzi wa mgodi.Mapambano hayo yaliyodumu kwa muda wa saa moja.

Habari zilisema majambazi hayo yalikuwa na mpango wa kupora dhahabu iliyokuwa inatarajiwa kusafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya kukodi ya Tanzania JT.Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya gari lililokuwa likisafirisha dhahabu kutoka mgodini, kuwasili katika uwanja huo na ndege ilipokuwa kwenye harakati ya kuruka, watu hao walianzisha mashambulizi.


Kwa upande wao polisi walijibu mapigo na kufanikiwa kumuua mmoja wa majambazi hao kwa kupigwa risasi.Polisi hao walikwenda katika eneo la mgodi kusaidiana na walinzi katika kupambana na majambazi hayo.Majambazi mengine manne yalifanikiwa kutoroka.Kabla ya kuanza kwa majibizano ya risasi kati ya majambazi na walinzi, kundi lilirusha bomu ya mkono kwa lengo la kutaka kulipua ndege.Hata hivyo bomu hil liliishia nje ya uzio wa uwanja huo na kushindwa kulipuka.

Habari zilisema kuna uwezekano kuwa majambazi hayo yametokea nchini jirani na inasemekana yalikuwa yamejificha porini hadi wakati gari liliokuwa limebeba madini, lilipowasili kwenye uwanja huo .

Katika tukio hilo majambazi yalimjeruhi mkononi wa kulia raia mmoja wa raia wa Afrika Kusini aliyetambulika kuwa ni, Engenas Vainder aliyekuwa mmoja wa wasafirishaji wa dhahabu kwenda Dar es Salamu.

Jambazi lililouawa na mwili wake kuhifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita alikutwa na simu mbili mfukoni zikiwa na laini za Airtel, mabomu manne na silaha moja,

Polisi walifanikiwa kukukamata bunduki aina ya SMG yenye namba UA 89381997 iliyotengenezwa mwaka1997, ikiwa na risasi 62, bastola yenye namba N004847aina ya Chines na mabomu manne ya kurushwa kwa kwa mkono.

Kwa mujibu wa ukaguzi wa polisi wa Geita, dhahabu iliyokuwa imetarajiwa kusafirishwa iikuwa katika makasha 16 zenye uzito wa kilo 400,taarifa ambayo imetofautiana na idara ya madini wilaya ya Geita.Ofisa mahusiano wa mgodi huo Joseph Mangilima alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo alisema hawezi kusema lolote kwa kuwa tayari jeshi la polisi lilikuwa kwenye upelelezi wa tukio.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barrow, alipopigiwa simu kuzungumzia tukio hilo simu yake iliita bila kupokelewa.

No comments:

Post a Comment