BAADA ya vuta nikuvute baina ya madaktari wanaoendelea na vikao vya  kutaka nyongeza ya posho na mishahara na Wizara ya Afya na Ustawi wa  Jamii, hatimaye madaktari hao wametangaza kuisusa Wizara hiyo na kubisha  hodi kwa  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakimwomba asikilize madai yao. 
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya juzi kutokea kutokuelewana  baina ya Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya na  madaktari hao baada ya kutofautiana juu ya mahali wanapotakiwa kuonana  ili kujadiliana. 
Wakati Dk. Nkya alikwenda katika ukumbi wa mikutano wa Arnatouglo  Mnazi Mmoja ili kuonana na madaktari hao, wao walikusanyika ukumbi wa  Don Bosco nao wakimsubiri. 
Kutokana na hatua hiyo, madaktari hao chini ya Chama cha Madaktari  Tanzania (MAT), jana waliendelea na vikao vyao vya kudai nyongeza hiyo  ya mishahara na posho wakiwa Don Bosco na baadaye Makamu wa  Rais wa  MAT, Dk. Primus Saidia  alitangaza azma ya kukutana na Pinda ili  kutafuta jibu la madai yao. 
“Napenda kuwafahamisha kwamba baada ya jana (juzi) Naibu Waziri wa  Afya kushindwa kukutana nasi, sasa tumeona Wizara ya Afya na Ustawi wa  Jamii haina dhamira ya dhati ya kusikiliza hoja zetu. 
“Naibu Waziri aliamua kwenda Arnatouglo kukutana nasi wakati  hakukuwa na mawasiliano yoyote rasmi ya sisi kuonana naye kule, sisi  tulikusanyika hapa (Don Bosco) kumsubiri, kwa vile tulikuwa na  mawasiliano rasmi ya kuonana naye hapa. 
“Baada ya kutafakari, sasa tumeona suala hili tulifikishe kwa Waziri  Mkuu, kwani ndiye kiongozi pekee ambaye sasa tumeona anaweza  kutusikiliza na kujibu hoja zetu. Hapa tunaandika barua rasmi kwenda kwa  Waziri Mkuu. Rais wetu (Dk. Namala Mkopi) atakwenda kwa Waziri Mkuu na  ataambatana na baadhi ya madaktari kati yetu,” alisema Dk. Saidia.  
Alisema chama hicho kina imani kubwa na Waziri Mkuu Pinda, kuwa ana  uwezo na utashi wa dhati wa kutatua matatizo yao kutokana na kuwa na  uhusiano mzuri na chama hicho. 
“Nikukumbusheni tu kwamba mara zote Waziri Mkuu amekuwa mtu makini  na msikivu sana kwetu. Kama mtakumbuka Novemba mwaka jana Waziri Mkuu  alifanya mazungumzo na viongozi wa MAT Mwanza alipokuwa kwenye hafla  Chuo Kikuu cha Bugando. Baadhi ya mambo tunayoyatoa leo tulimpa wakati  ule, hivyo anafahamu kwa dhati madai yetu,” alisema. 
Gazeti hili jana jioni liliwasiliana na mmoja wa viongozi wa  madaktari hao ambaye alisema Ofisi ya Waziri Mkuu, ilikuwa tayari  imeanza kujibu hoja zilizowasilishwa na madaktari hao kupitia barua  maalumu waliyomwandikia Pinda. 
“Waziri Mkuu hataweza kuja, lakini ofisi yake imeanza kujibu hoja  zetu na viongozi wetu wapo huko wanasubiri majibu tutakayojibiwa ingawa  tuna imani kubwa ya kupewa majibu mazuri. 
“Tumeambiwa kwamba huenda Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Peniel  Lyimo) atakuja kuzungumza na sisi ili kutafuta muafaka. Uwezekano wa  kuonana naye kesho (leo) ni mkubwa sana,” alisema kiongozi huyo wa MAT. 
Kutoka Mwanza,  Grace Chilongola, anaripoti kwamba MAT Kanda ya Ziwa  imeiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuacha  malumbano na madaktari na badala yake isimamie matatizo yaliyopo ili  kuboresha sekta ya afya. 
Walitoa ombi hilo jana baada ya kikao cha pamoja kilichojumuisha  madaktari wa Kanda ya Ziwa kilichokuwa kikiunga mkono madai ya madaktari  wenzao wa Muhimbili. 
Akizungumza Katibu wa MAT, Dk. Rodrick Kabangila alisema Serikali  iangalie mambo ya msingi katika sekta ya afya kama ya milipuko ya surua  inayoendelea kutokea wakati chanjo zinatolewa, ukosefu wa dawa na vifaa  badala ya kuendeleza malumbano na madaktari. 
Kabangila ambaye pia ni Mwenyekiti wa MAT, Kanda ya Ziwa alisema  Serikali inapoendeleza malumbano na madaktari, inaamsha machungu ya  madaktari ya siku za nyuma na kutaka kuyafanyia kazi madai yao ya  mishahara, posho na kusomeshwa, ili waweze kufanya kazi pamoja. 
Aidha, aliiomba Serikali kuangalia ugumu wa shule ya madaktari,  gharama kubwa wanayosomea pamoja na changamoto wanazokumbana nazo  kazini, kwa kuwalipa kile kinachostahili na si kusingizia kuwa Serikali  haina fedha. 
Dk. Godfrey Mbawala alisema madaktari hawataki wafikie kwenye mgomo,  kwani itakuwa ni vita na watakaoathirika ni wananchi wenye wagonjwa  hospitalini. 
“Hofu ni kwa wagonjwa watakaokufa na kuziacha familia zao  zikihangaika na ugumu wa maisha na ukiuliza sababu ni madaktari  kulumbana na Serikali, inatia uchungu sana, hatutaki kufika huko,”  alisema na kuiomba Serikali ichukulie suala la madai ya madaktari kwa  uzito unaostahili. 
Alisema jamii inapaswa kuwaunga mkono ili nao wasiathirike na mgomo unaoweza kutokea .  
“Hatutaki kufikia mgomo kutokana na athari zake kuwa kubwa kiuchumi,  kidini na kijamii, lakini kwenye mgomo tutafikishwa na Serikali iwapo  itashindwa kutusikiliza,” alisema Dk. George Adriano.
No comments:
Post a Comment