BARAZA Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) leo linatarajiwa kukata mzizi  wa fitina kwa ama kumfukuza uanachama Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid  Mohammed na wenzake 13 au la.
Wakati baraza hilo kuu likitarajiwa  kukata mzizi huo wa fitina, tayari mpasuko zaidi umejitokeza ndani yake  baada ya uongozi wa chama hicho Mkoa wa Mwanza, kutishia kujiengua  endapo Hamad na wenzake watafukuzwa.
Hamad na wanachama wengine  12 wa chama hicho watafikishwa mbele ya Kikao cha Baraza Kuu la uongozi  la chama hicho kinachoketi mjini Zanzibar, kusomewa mashtaka na  kuhukumiwa.
Katika barua walizopewa kutoka ofisi ya chama hicho,  Dar es Salaam za Januari Mosi, mwaka huu na Shaweji Mketo kwa niaba ya  Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad, wanachama hao wanatakiwa kufika  kwenye kikao hicho bila kukosa. Barua hiyo inaeleza kuwa kikao hicho  kitafanyika leo kuanzia saa 3:00, asubuhi katika Hoteli ya Mazson.
“Kwa  mujibu wa Katiba ya CUF, kifungu cha 63 kinachozungumzia wajibu wa  Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kifungu cha 63 (1)(d), kinafafanua wajibu  huo kuwa ni kulinda na kuendeleza heshima ya chama na Serikali zote  halali za nchi,” inasema sehemu ya barua hiyo na kuendelea:
“Kifungu  cha 63 (1) (j) kinaeleza wajibu wa kuwachukulia hatua za kinidhamu  viongozi na wanachama wanaoshutumiwa kwa makosa mbalimbali, kwa kufuata  masharti ya katiba hiyo na kanuni zinazatungwa mara kwa mara.”
Sehemu  ya barua hiyo ilifafanua zaidi kwamba kwa kuzingatia hali hiyo, Kamati  ya Utendaji ya Taifa imeridhika kwamba kuna haja ya kutumia uwezo  iliyopewa chini ya kifungu cha 62(1) cha Katiba ya CUF kuitisha kikao  cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama ili kutafakari  hali hiyo na kusikiliza tuhuma zinazomkabili kila mmoja wao.
Wanachama  hao pia watapata nafasi ya kujitetea ambayo ni ya kikatiba na kisha  baraza hilo litatoa uamuzi kwa kadri inavyofaa, kwa mujibu wa katiba ya  chama hicho.
CUF Mwanza
Wakati CUF kinajiandaa kutoa uamuzi  juu ya mgogoro huo, huko Mwanza chama hicho kimetoa tamko la kutaka  maamuzi hayo yawe ya kisayansi na kwa maslahi ya chama na si vinginevyo.
Akisoma  tamko hilo kwa niaba ya wanachama wote jana, Mwenyekiti wa CUF Wilaya  ya Nyamagana, Hamduni Mercei alisema wanachama hao wataunga mkono uamuzi  utaoleta suluhu katika chama na hivyo kuwaweka wanachama na chama chao  katika mazingira bora ya kujiimarisha kisiasa.
“Chama hakiko  vizuri kimpangilio na tunahitaji juhudi za pamoja kuhakikisha tunarejea  tulikotoka na pengine kwenda vizuri zaidi ya jinsi tulivyokuwa kabla na  baada ya uchaguzi mkuu uliopita,” alisema Mercie na kuendelea:
“Tunaomba  wajumbe na viongozi wetu watilie maanani maoni ambayo yanatolewa na  wanachama mbalimbali wanaokitakia chama mafanikio, siasa iwe urafiki,  udugu, kuvumiliana, kuheshimiana, kukosoana na kusameheana,” ilisomeka  sehemu ya tamko hilo.
Hofu ya Hamad
Akizungumzia kikao hicho jana, Hamad alidai kwamba uamuzi utakaotolewa umeshapangwa na Maalim Seif.
Alisema yupo tayari kwa uamuzi wowote utakaotolewa lakini, hawezi kuhama chama na kwenda kingine kama inavyodhaniwa.
“Mimi  nimeshajua wamepanga kutufukuza wanachama watatu mimi na wenzangu Doyo  Hassan Doyo na Shoka Khamis Juma ambao tunaonekana ni vinara wa mgogoro  ndani ya chama na wengine watapewa karipio,” alisema Hamad.
Wanachama  wengine ambao wanadaiwa kwamba watapewa karipio ni Juma Said Saanani,  Yasini Mrotwa, Mohamed Albadawi, Mohamed Masaga, Doni Waziri, Yusuph  Mungiro, Haji Nanjase, Ahmed Issa, Tamim Omary, Amir Kirungi na Ayub  Kimangile.Katika nakala ya barua pepe aliyoipata Hamad iliyotumwa  Desemba 14, mwaka jana na Maalim Seif kwenda kwa Mwenyekiti wa CUF,  Profesa Lipumba ilieleza kwamba, wameshauriana na makamu na wameona kuna  haja ya kuwaita katika kamati ya wanachama hao.
“Nimeshauriana  na makamu na tumeona kuna haja ya jamaa yako na genge lake kuitwa katika  kamati ya nidhamu na maadili kuhojiwa, ushahidi wa kutosha umekusanywa  dhidi yake na wasaidizi wake, Doyo na Shoka na kamati ya maadili ilete  taarifa katika kikao kijacho cha Kamati ya Utendaji (KUT)ambacho   kitafanyika mwisho wa mwezi,” ilieleza barua hiyo.
 “Chama ki-act  decisively hasa dhidi ya jamaa yako yeye muono wetu tumfukuze kwenye  chama na akiamua kwenda mahakamani na mahakama kutoa uamuzi wa  kumpendelea yeye mwache awe mbunge wa mahakama kama walivyokuwa wakina  Asha Ngede na Naila Majid,” ilisisitiza sehemu ya barua hiyo.
No comments:
Post a Comment