Friday, January 6, 2012

Askofu Kilaini: Ndugai jibu hoja

Waandishi Wetu
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini, amemshangaa Naibu Spika Job Ndugai kwa kile alichoeleza kuwa amekwepa kujibu hoja ya msingi  ya Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye inayohusu nyongeza ya posho za wabunge,  badala yake, ameshambulia kiongozi huyo kama mtu binafsi.

"Sumaye kama mwanadamu anaweza akawa na upungufu mwingi, lakini alichokisema kuhusu posho tujihoji kina ukweli gani? Hilo ndilo la msingi. Alichotakiwa Ndugai ni kufafanua uhalali wa posho na sio kusema aliyetoa hoja hiyo, hana usafi wa kuhoji."

Katika kuonesha kukerwa na kauli ya Ndugai, kiongozi huyo wa kiroho alikemea kauli za baadhi ya wanasiasa kutotaka kukosolewa hata pale wanapofanya makosa  na kutaka watu waachwe waseme ukweli bila kuzibwa midomo wala kubezwa.

" Watu waachwe waseme kweli wasibezwe. Kwamba naye (Sumaye) alijiongezea posho, hilo ni jambo lingine ambalo kama anataka (Ndugai), alianzishe mjadala watu wajadili. Lakini sasa tunazungumzia suala la posho za wabunge ambazo sote zinatukera,"alisema Kilaini.

Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, si sahihi mtu kujadili hoja aliyoanzisha mtu kwa kuangalia udhaifu wa mtoa hoja. "Hakuna hoja ya msingi katika kumshambulia mtu anayetoa hoja kwa kutumia udhaifu wake, kwani ukweli utaendelea kuwa ukweli na udhaifu wa mtu ni jambo lingine."

Askofu Kilaini alisema: "Nataka watu wajue kwamba hakuna mtakatifu hapa, wote tuna udhaifu, lakini kama mwenzetu kasema ukweli tujadili hoja yake kwa moyo mkunjufu na sio kumpuuza kwa sababu tu eti aliyeongea ana upungufu fulani."

Aliongeza;  "Ndugai lazima asome alama za nyakati. Huu sio wakati wa kutetea posho kwani hakuna atakayemwelewa. Watanzania wa matabaka yote wamezipinga sasa yeye akianza kuzitetea atabaki peke yake."

Wanasheria
Kauli hiyo ya Askofu Kilaini, iliungwa mkono na baadhi ya wanasheria waliozungumzia hoja hiyo jana ambao kwa nyakati tofauti walisema kitendo cha Ndugai kuponda maoni ya Sumaye, kimeonyesha kuwa si mtu makini.
Wakili wa kujitegemea, Lupia Augusto alihoji kama Ndungai alikuwepo bungeni wakati sheria ya kupandisha posho za viongozi wastaafu zilizomwezesha Sumaye kujiandalia uzee mwema, kwanini hakupinga. "Iweje aje na hoja hiyo leo?"alihoji.

Augusto alisema tabia aliyoionyesha  Ndugai inatakiwa kutafsiriwa kama hakujua majukumu ya ubunge wake  wa kuhoji  na badala yake, alijua itamnufaisha.Alifafanua kwamba kitendo alichokifanya Ndugai ni ishara kwamba maoni yake yamekumbatia kujinufaisha na sio kunufaisha wananchi.

Alisema Ndugai ameanika udhaifu wake kwani hakuna rekodi zinazoonyesha kwamba alipinga hoja ya kupitisha posho ilipoletwa wakati Sumaye alipokuwa Waziri Mkuu.Augusto alisema kuna kila dalili kwamba kuna mambo mengi yanayofanywa kwa siri kwa maslahi ya wachache na kwamba wanapopingana ndipo mambo hayo hujitokeza wazi.

 “Wananchi wajiulize alifanya nini kupinga, maana hapa anaazisha malumbano yasiyokuwa na tija baada ya watu kupinga posho ambazo wabunge wamejipandishia bila kuweka uzalendo mbele,”alisema

Awakera wananchi
Baadhi ya wananchi nao wameeleza kukerwa na kauli ya Ndugai dhidi ya Sumaye na kwamba ni mbinu za kuwatisha viongozi wastaafu wasitetee maslai ya Umma.

Mkazi wa Dar es Salaam, Kimazi Totera alisema Ndugai anatumia Bunge kama sehemu ya kutetea matakwa yake binafsi kwa kuziua kauli za viongozi wastaafu pale wanapotetea maslai ya Umma.

Fatma Haji alisema Ndugai ana siri kubwa kutokana na kuyajua mazingira ya uongozi ya awamu ya tatu kwa kudai Sumaye alijiwekea sheria ya viongozi wa juu wastaafu kulipwa asilimia 80 ya mshahara.
“Yeye kama kiongozi alikuwa wapi kupinga sheria ya viongozi hawa kulipwa kiwango hicho cha pesa ina maana naye ana chuki binafsi, tungemwelewa kama angesema mapema,”alisema Fatma.

Alichosema Sumaye
Jana alipotakiwa kuzungumzia hoja za Ndugai jana, Sumaye alisema," No comment," nataka kusoma na kuelewa vizuri alichokisema kwa hiyo unitafute kesho (leo)."

Kilichoamsha hasira za Ndugai ni kauli ya Sumaye alioyoitoa kupitia kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV,  kwamba ongezeko la posho za wabunge linaweza kuchochea makundi mengine kudai kama Wanajeshi, Polisi, Mahakama na walimu nao kutaka nyongeza, hivyo kumweka Rais katika wakati mgumu kufanya uamuzi.

“Mwanasiasa mzuri akifanya jambo akiona limewaudhi wananchi anatakiwa aliache, lakini pia kwenye hili huu mkanganyiko wa Spika na Katibu wake na huu ukimya wa Ikulu ni tatizo, tungependa waseme ili umma ujue hali ikoje,”
 alisema Sumaye.

Alisema hatua ya Bunge kujipandishia posho ya kikao kutoka 70,000 hadi 200,000 kwa
siku haliingii akilini na kwamba, inakiuka utaratibu uliowekwa na serikali katika kulipa gharama kwa maofisa wake ikiwa ni pamoja na gharama hizo  za fedha za kujikimu.
“Siyo kwamba napinga posho, wabunge wanastahili posho, lakini kwa kweli kujiongezea kutoka 70,000 hadi 200,000 siyo sahihi,” alisema Sumaye.

Alisema wakati yeye alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kwa awamu ya pili kushika wadhifa wa Waziri Mkuu, aligoma kwa sababu alikuwa amekwaruzana  na wabunge kuhusu nyongeza ya posho.

“Nilimwambia wabunge watanikataa kwa sababu nimegombana nao sana juu ya suala la posho lakini akasema lazima uwe na mimi ndipo nikakubali, lazima hili suala liangaliwe mara mbilimbili…, leo wabunge mmejiongezea kesho jeshi, polisi na walimu nao watataka, tutafanyaje tusifanye mambo ambayo yatamuweka Rais pabaya,” alisema Sumaye.

Alisema posho ni jambo ambalo kwa sasa limekuwa tatizo kwa serikali na kwamba imefika wakati ofisi za serikali zimehamia hotelini, lengo likiwa ni watumishi wa umma kutafuta mwanya wa kulipana posho.

“Ndiyo maana watu wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wanakusanya fedha nyingi lakini ni fedha kidogo sana zinakwenda kwenye huduma za jamii, nadhani hili ni tatizo na ni utawala mbaya kabisa, lazima kuwepo mabadiliko kama kweli tunataka kuisafisha nchi yetu,” alisema Sumaye

No comments:

Post a Comment