MADAKTARI 229 walioko katika mafunzo kwa njia ya vitendo katika  Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, wamegoma  wakishinikiza kulipwa jumla ya Sh176 milioni, zikiwa ni posho zao za  kijikimu.Mgomo huo ulianza jana mchana na madaktari hao wamesema  hautakwisha hadi hapo watakapolipwa fedha zao.
Madaktari hao ni  wa kada za tiba ya vinywa, maabara, dawa na wafamasia ambao wametishia  mgomo huo utaenea hadi katika Hospitali za Mnazi Mmoja, Zanzibar, Bombo  mkoani Tanga, Temeke, Amana na Mount Meru, jijini  Arusha ambako wenzao  nao hawajalipwa kwa miezi miwili. 
Wakizungumza  mbele ya Mganga  Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa. aliyekwenda Muhimbili kuwasikiliza  madai yao,  madakatari hao walisema maisha yao yamekuwa magumu kwa  sababu ya kukosa fedha za kujikimu.
 Mmoja wa wataalamu hao,  Dk Frank Kagoro, alisema  tatizo  lililopo ni kukosekana kwa uwajibikaji kwa upande wa Serikali.
“Mnachukulia  mambo kirahisi sana tupo katika mafunzo lakini tutawezaje kufanya kazi  bila fedha. Tunajua tuna wagonjwa na wanaumia kwa sababu ya hatua hii,  hivi nani hapa asiyejua kuwa muda huu alitakiwa kuwa wodini akiwapitia  wagonjwa, hivi kweli mnatupa kipaumbele," alihoji Dk Kagoro.
Kwa  upande wake Mwenyekiti wa madaktari hao, Dk Mally Deogratius, alisema  madai yao ni zaidi ya Sh176 milioni, zikiwa ni posho za kati ya Novemba  na Desemba mwaka jana, kipindi ambacho hawakulipwa.
Hata hivyo, Dk  Mtasiwa aliwahakikishia kuwa malipo yao yatafanyika leo na kwamba  yamechelewa kutokana na taratibu za Serikali katika malipo.
Mgogomo  wa madaktari hao, unakuja wakati wanafunzi wa udaktari waliokufuzwa  katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi cha Sayansi za Tiba cha  Muhimbili, wakiwa wameomba radhi, kufuatia vurugu walizofanya mwezi  uliopita.
Wanafunzi hao walifanya hivyo jana ambapo walisema  wametafakari na kujiridhisha kuwa walifanya makosa yaliyosababisha  kukosekana kwa amani na utulivu katika chuo hicho.Wanafunzi hao  walifanya fujo Desemba 8 na 10 mwaka jana wakishinikiza kusikilizwa kwa  madai yao.
No comments:
Post a Comment