Monday, January 2, 2012

Tanesco ina mzigo wa gharama -JK

RAIS Jakaya Kikwete amesema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linakabiliwa na mzigo mzito wa gharama za uzalishaji uliosababishwa na uzalishaji wa umeme kupitia mitambo ya mafuta.

Kutokana na gharama hizo, Rais Kikwete amesema juzi katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa
Taifa, kuwa shirika hilo limelazimika kupeleka maombi ya kuongezabei ya umeme kwa asilimia zaidi ya 100 kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

“Kwa sababu ya kutumia mafuta, umeme huu ni ghali na umekuwa mzigo mkubwa wa gharama kwa Tanesco. Kutokana na sababu hizo, Tanesco wamepeleka maombi Ewura ya kutaka kuongeza bei ya umeme,” alisema Rais.

Rais Kikwete alisema kwa muda mrefu shirika hilo limekuwa likijiendesha kwa kutegemea zaidi umeme wa mvua na hivyo kukabiliwa na wakati mgumu wakati wa ukame huku kukiwa na upungufu wa gesi na hivyo kulazimisha mitambo ya kampuni za kufua umeme kutumia mafuta.

“Lakini, kwa sababu ya kutumia mafuta, umeme huu ni ghali na umekuwa mzigo mkubwa wa
gharama kwa Tanesco. Kutokana na sababu hizo, Tanesco wamepeleka maombi Ewura ya kutaka kuongeza bei ya umeme,” alisema Rais Kikwete.

Historia ya gharama za Tanesco
Akifafanua historia ya gharama hizo, Rais Kikwete alikumbushia ukame ulioikumba nchi mwaka 2006 ambao alisema ulisababisha kupungua sana kwa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.

Kutokana na upungufu wa maji, Rais alikumbusha kuwa taifa liliingia katika tatizo kubwa la upungufu wa umeme na ili kukabiliana na tatizo hilo, Tanesco ikalazimika kuingia mikataba na kampuni za kuzalisha umeme kwa malipo.

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema kwa kuwa gesi inayozalishwa hivi sasa kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya kufulia umeme iliyopo Ubungo haitoshelezi mahitaji ya taifa,
kampuni hizo zililazimika kutumia mitambo inayotumia mafuta.

Alisema kampuni hizo zilipata mitambo inayozalisha umeme kwa kutumia mafuta na tayari inazalisha umeme ndiyo maana mgawo sasa haupo lakini akatahadharisha kuwa umeme huo gharama yake ni kubwa na ndio iliyosababisha mzigo wa gharama kwa Tanesco.

Hali hiyo ilisababisha mwishoni mwa mwaka jana Tanesco kuomba kupandisha bei za umeme kwa wastani kutoka Sh 141 ya sasa kwa uniti hadi Sh 359 ifikapo Januari mwaka huu ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 155.

Tatizo la umeme kuwa historia
“Nilisema kuwa tutaanza juhudi za kuendeleza vyanzo vingine vya nishati hasa gesi asilia na makaa ya mawe mpaka tufikie mahali ambapo hata kama maji hayatoshi katika mabwawa ya vituo vya umeme, nchi haitakosa umeme,” alisema Rais Kikwete.

Alisema Serikali itaendelea kutekeleza uamuzi huo kwa busara na kwamba hadi sasa Serikali kupitia Tanesco imeshaongeza megawati 245 za umeme unatokana na gesi asilia.

Aidha alisema maombi ya Serikali kwa Serikali ya China ya kupata mkopo wa kujenga bomba la
kusafirisha gesi kutoka Mtwara na mtambo wa kuchakata gesi inayotoka Songo Songo tayari yamekubaliwa.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, baada ya kukubaliwa kwa maombi hayo, kwa sasa utekelezaji wake unatarajiwa kuchukua miezi 18 na gesi itakayoletwa inaweza kuzalisha mpaka Megawati 3,000 za umeme.

“Baada ya hapo kasi ya kuongeza umeme itakuwa kubwa zaidi na tatizo la upungufu wa umeme linaweza kuwa historia,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment