Wednesday, January 4, 2012

Wabunge waliomshambulia Magufuli wakosolewa

SAKATA la nauli ya kivuko cha mv Magogoni limechukua sura mpya baada ya mfanyabiashara
maarufu nchini, Azim Dewji, kuwajia juu wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam, akiwataka kuacha kumshambulia Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na badala yake watatue matatizo ya msingi ya wananchi majimboni mwao.

Wabunge hao wakiongozwa na Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, juzi walizungumza na
waandishi wa habari na kusema, kitendo cha Magufuli kutangaza ongezeko la nauli ya kivuko hicho kwa asilimia 100 bila kushirikisha wananchi, hakina tofauti na udikteta.

Akizungumza jana, Dewji alisema wabunge hawapaswi kupinga kila jambo kwa lengo la kujijenga kisiasa na kusisitiza, kuwa Magufuli ana hoja za msingi, hivyo aungwe mkono kwa lengo la kuboresha usafiri wa majini katika eneo hilo na mengine ya nchi.

“Jamani, ongezeko la Sh 100 linaleta chokochoko za nini? Leo hii hata ombaomba ukimpa Sh 100 anaweza kukurushia usoni. Wanalalamikia Sh 100 wakati wao walijiongeza posho za Sh 200,000, hawakuona ubaya wowote…nadhani wabunge wa Dar es Salaam walipaswa kumuunga mkono Magufuli, ili kivuko kijiendeshe na kutoa huduma bora na za kudumu,
badala ya kila kitu kutegemea Serikali Kuu.

“Hivi kila kitu kikitoka serikalini, fedha nyingine za maendeleo zitatoka wapi, kama si kuishia kuziba upungufu kama unaojitokeza kwenye vivuko vyetu vinapoharibika?” alihoji na kusema kama fedha zisipokusanywa, na vivuko vikapata hitilafu na kushindwa kutoa huduma,
watakuwa wa kwanza kudai Serikali imewasahau wana-Kigamboni.

Alikwenda mbali zaidi na kusema pesa zitakazokusanywa kutokana na nauli mpya zitachangia kulipa ongezeko la posho za wabunge, kwa kuwa ni fedha za wananchi na wabunge wanalipwa kutokana na fedha za walipa kodi.

“Daladala zinapanda kila kukicha, hatusikii kelele, sasa angalia, Waziri Magufuli amesema kwa mara ya mwisho bei ya kuvuka kwenda na kutoka Kigamboni ilipandishwa miaka 14 iliyopita, hawaoni kuwa bei hiyo imepitwa sana na wakati?

“Na mbaya zaidi nasikia wanataka wakabidhiwe kazi ya kuendesha kivuko, mbona baadhi yao majimboni mwao tayari mambo yameanza kuwa maji ya shingo, hayaendi kabisa. Nadhani wangejikita katika kustawisha majimbo kwanza, wakishamaliza ndipo waombe kusaidia kazi za wengine, huu kwao si wakati sahihi wa kutoa msaada,” alisema na kuhoji kwa nini wasizungumze kumaliza kero nyingine za jijini, ikiwamo foleni.

Kauli ya Dewji, aliyekuwa anazungumza kwa hisia kali, huku akisisitiza wabunge kuacha kudandia mambo kwa lengo la kupata umaarufu aliouita wenye kuwajenga zaidi kisiasa badala ya kuwanufaisha wananchi wa kawaida, imeibuka huku kukiwa na mjadala mkali tangu kupandishwa kwa nauli za kivuko cha Kigamboni.

Jumapili iliyopita, Dk. Magufuli alitangaza kuwa, Serikali imeamua kupandisha nauli hiyo kutoka kati ya Sh 50 na Sh 100 hadi Sh 200 kwa safari moja ya kivuko hicho, kutokana na gharama za uendeshaji kuwa juu.

Alisema nauli iliyokuwapo ni ya tangu mwaka 1997, huku nauli za vivuko vingine zaidi ya 30 nchini imekuwa ikipanda mara kwa mara.

Magufuli alisema kivuko cha Magogoni kimekuwa kikitoza nauli za chini ikilinganishwa na Chato, kinachotoza Sh 300, Pangani Sh 200, Kisorya Sh 300, Lugolora Sh 500, Nyakarilo Sh 300, Chato-Bukombo Sh 2,000, Kirambo Sh 500 na Utete Sh 300, huku wanafunzi wakisafiri bure.

Sambamba na upandishaji nauli kwa watu, pia nauli ya magari imepanda ambapo madogo yatatozwa Sh 800 na Sh 1,500; pick up Sh 1,000 na Sh 2,000 na ya kuanzia tani tatu na nusu Sh 5,000 hadi Sh 7,500.

Wabunge waliokutana Dar es Salaam juzi na kutoa tamko dhidi ya Magufuli ni pamoja na John Mnyika wa Ubungo, Dk Faustine Ndugulile wa Kigamboni, Mussa Azzan Zungu (Ilala) na wa viti maalumu, Mariamu Kisanji, Zarina Madabida na Philipa Mtulano.

No comments:

Post a Comment