Thursday, January 5, 2012

Ndugai amshukia Frederick Sumaye


ASEMA HANA USAFI WA KUBEZA NYONGEZA YA POSHO

Fredy Azzah
NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai amemjia juu Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye kuhusu kauli yake ya posho za wabunge, akisema hakupaswa kuitoa kwani aliwahi kufanikisha kupitishwa sheria ya malipo kwa viongozi wakuu wastaafu ili kujinufaisha akistaafu.Juzi, Sumaye pamoja na mambo mengine, alizungumzia mwelekeo wa taifa kwa sasa na kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015 huku akisema mpango wa ongezeko la posho za wabunge unapaswa kuachwa kwani unaweza kufanya makundi mengine ya utumishi wa umma kudai nyongeza.

Kauli hiyo ilijibiwa vikali jana na Ndugai ambaye aliwatahadharisha viongozi wastaafu kuwa makini na kauli wanazotoa na kuwataka wale ambao wanataka urais wa 2015 ikiwa ni pamoja na Sumaye waseme sasa badala ya kuwababaisha Watanzania kwa kuzungumza mambo mbalimbali ili wawapende.

Alisema wakati Sumaye anazungumzia posho za wabunge, sheria ya kuwalipa viongozi wastaafu mafao ilipitishwa wakati akiwa kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni na hakuipinga kwa kuwa alikuwa anajiandalia mazingira ya kustaafu.
“Kwa sasa analipwa asilimia 80 ya mshahara wa waziri mkuu aliyepo madarakani, ni fedha nyingi kuliko hata mshahara wa Naibu Spika (Ndugai kwa sasa), wakati sheria hii inapitishwa alikuwa kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni (Waziri Mkuu), alikuwa anajiandalia mazingira ya kustaafu,” alisema Ndugai na kuongeza:

“Sitaki kuendelea kusema sana jinsi ambavyo ananufaika, lakini ninachosema viongozi wastaafu duniani kote inatakiwa wawe makini na kauli zao. Wakianza kwenda kwenye vyombo vya habari na kusema maneno haya haipendezi.”
Alifafanua kwamba badala ya kuzungumzia posho za wabunge pekee ni vyema pia likazungumziwa suala la posho kwa viongozi wote wa umma.

“Kwa watu wanaotaka kugombea urais mwaka 2015 ni bora waseme sasa. Waache kutubabaisha Watanzania… nasema viongozi wastaafu lazima wawe makini kwa kauli zao, mimi Sumaye ninamheshimu sana na ninatambua haki yake ya kikatiba ya kujieleza,” alisema na kumshauri kuwa makini na kauli zake anapozungumza juu ya Bunge kwa sababu yeye pia alikuwa sehemu ya mhimili huo.

“Yeye ni kama mchezaji mstaafu wa timu hii (Bunge), inatakiwa awe makini sana hawezi kuizungumzia hii timu kama mshabiki mwingine,” alisema Ndugai.

Ndugai alisema posho zilikuwepo tangu enzi za Sumaye akiwa mbunge, naibu waziri na hatimaye waziri mkuu na kwamba kama hoja ni kiasi cha fedha... “Aseme ni kiasi gani wabunge wanapaswa kulipwa.”
Sumaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 1985 baada ya kushinda ubunge katika Jimbo la Hanang na mwaka 1987, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo hadi mwaka 1994 alipoteuliwa kuwa waziri kamili katika wizara hiyo.

“Mimi nakwambia kitu ambacho nakijua na wakati huo nilikuwa bungeni kama mbunge na Sumaye alikuwa akizipokea hizi posho, Rais (Ali Hassan) Mwinyi aliwahi kusema kila zama na kitabu chake, hebu na yeye (Sumaye) atuache na sisi tuandike kitabu chetu,” alisema Ndugai.

Dk Bana abeza
Akizungumzia kauli ya Sumaye, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema mambo aliyozungumza si mapya na huku akimtaka kutazama kila neno linalotoka mdomoni mwake.

Dk Bana alisema kauli ya Sumaye kuhusu matumizi ya taasisi ya urais, inaweza kutafsiriwa kwamba inatokana na yeye kuwa na uchungu wa kuikosa alipogombea na Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi wa ndani wa CCM.

Sumaye katika kinyang’anyiro cha kupenya kura za maoni kwa ajili ya kupeperusha bendera ya CCM baada ya Mkapa, alishika nafasi ya tano na kushindwa kuingia hata tatu bora ambayo waliingia Rais Kikwete, Dk Salim Ahmed Salim na Profesa Mark Mwandosya.

“Kwanza anavyozungumzia taasisi ya urais hatujui kama ni hii au ni zilizopita, lakini ikumbukwe kuwa aligombea nafasi hiyo akaikosa kwa hiyo kuna uwezekano kuwa ni roho inamuuma,” alisema Bana.

Kuhusu suala la rushwa katika uchaguzi alisema: “Suala hili lilikuwepo kwa muda mrefu na limepigiwa sana kelele, yeye hakuweza kumshauri Rais (Benjamin) Mkapa kuwa watunge sheria ya kupambana na hali hii, lakini sasa hivi Serikali imejaribu inatakiwa aipongeze kwa hilo,” alisema Dk Bana.

Alisema hata baada ya kuundwa kwa sheria hiyo, viongozi wengi wakubwa ikiwa ni pamoja na wale wastaafu hawaonekani kuipigia debe.

Dk Bana alisema kuundwa kwa sheria ni jambo moja na kinachotakiwa sasa ni utekelezaji wake kufanyiwa kazi.
Alisema pia ingekuwa jambo jema endapo viongozi wastaafu wangeunda taasisi yao ili waweze kushauri Serikali ili busara zao ziweze kutumika vyema huko... “Yeye ana nafasi kubwa sana ya kuzungumza haya mambo ndani ya chama na pia hata kumshauri Rais moja kwa moja.”

Kuhusu suala la posho kwa wabunge, alisema Sumaye alilizungumza vizuri na inatakiwa aungwe mkono na watu wengine.

Alichosema Sumaye
Akizungumza kupitia kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, Sumaye alisema ongezeko la posho za wabunge linaweza kuchochea makundi mengine kama wanajeshi, polisi, Mahakama na walimu nao kutaka nyongeza, hivyo kumweka Rais katika wakati mgumu kufanya uamuzi.

“Mwanasiasa mzuri akifanya jambo akiona limewaudhi wananchi anatakiwa aliache, lakini pia kwenye hili huu mkanganyiko wa Spika na Katibu wake na huu ukimya wa Ikulu ni tatizo, tungependa waseme ili umma ujue hali ikoje?” alisema Sumaye.

Alisema hatua ya Bunge kujipandishia posho ya kikao kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku haliingii akilini na kwamba, inakiuka utaratibu uliowekwa na Serikali katika kulipa gharama kwa maofisa wake ikiwa ni pamoja na gharama hizo za fedha za kujikimu.

“Siyo kwamba napinga posho, wabunge wanastahili posho, lakini kwa kweli kujiongezea kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 siyo sahihi,” alisema Sumaye.

Alisema wakati alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kwa Awamu ya Pili kushika wadhifa wa Waziri Mkuu, aligoma kwa sababu alikuwa amekwaruzana na wabunge kuhusu nyongeza ya posho.

“Nilimwambia wabunge watanikataa kwa sababu nimegombana nao sana juu ya suala la posho lakini akasema lazima uwe na mimi ndipo nikakubali, lazima hili suala liangaliwe mara mbilimbili… leo wabunge mmejiongezea kesho jeshi, polisi na walimu nao watataka, tutafanyaje tusifanye mambo ambayo yatamuweka Rais pabaya,” alisema Sumaye.

Alisema posho ni jambo ambalo kwa sasa limekuwa tatizo kwa serikali na kwamba imefika wakati ofisi za Serikali zimehamia hotelini, lengo likiwa ni watumishi wa umma kutafuta mwanya wa kulipana posho.

No comments:

Post a Comment