Boniface Meena
WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amepuuza msimamo  wa wabunge wa Dar es Salaam wa kumtaka awaombe radhi, akisisitiza kuwa  kauli yake ya kupandisha nauli katika kivuko cha Kigamboni  hataibadilisha na wabunge hao, waache kupiga siasa.
Dk Magufuli  alijikuta kwenye mvutano na wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam kufuatia  kauli yake aliyotoa Jumapili iliyopita kwa wakazi wa Kigamboni, kuwa  kama wakishindwa kulipa nauli ya Sh200, wapige mbizi habarini au wapite  Kongowe ili kuingia katikati ya Jiji vinginevyo, warudi vijijini  wakalime.  
Kauli hizo za kejeli ziliwafanya wabunge hao kupitia  Mwenyekiti wao Abbas Mtemvu, kumtaka waziri huyo aombe radhi huku  wakiwambia wao wanalijua jiji la Dar es Salaam kuliko Magufuli.
Pia walimtaka akafanye ubabe katika Jimbo lake la uchaguzi
Lakini  jana akizungumza jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli hakutaka kujibu  maswali yaliyomtaka aeleze msimamo wake kuhusu msukumo huo wa wabunge,  badala yake alisisitiza tu kwamba nauli mpya aliyoitangaza  haitabadilika.
 "Waambieni (wabunge wa Dar es Salaam ) waache  kupiga siasa, kama wanaona gharama ni kubwa wakajifunze kivuko cha Chato  au waombe kukiendesha kivuko hicho kwa kuwa sheria inaruhusu," alisema.
Alisema  Ibara ya 26 Ibara ndogo ya 1 na ya 2 inampa kila mtu wajibu wa kufuata  sheria na kuongeza kwamba  yeye amefuata sheria kufanya ongezeko hilo la  nauli za vivuko na hivyo  nauli hiyo halitabadilika.
"Kwa mujibu  wa Farries Act iliyotungwa na kupitishwa na wabunge wenyewe  inanipa  nguvu mimi waziri kufanya hivyo kwa hiyo hakuna sheria inayosema  nikitaka kupandisha nauli nikawaulize wabunge," alisema Magufuli.
"Dar  es Salaam itajengwa na watu wa kuja, Mtemvu na wenzake wajue hilo na  tuache  siasa tufanye kazi. Nawaambia wakitaka kuendesha kivuko hicho  nitashangilia sana kwani kwa mujibu wa sheria inaweza kuwa hivyo na kama  wanapinga wakajifunze Chato watu wanakovuka kwa Sh 3,000," alisisitiza.
Dk  Magufuli alisema wakazi wa Kigamboni wametii sheria kwa kuendelea  kulipa nauli hiyo ambayo imefanya makusanyo katika kivuko hicho kutoka  Sh9 milioni hadi kufikia Sh 18 milioni, fedha ambazo zitasaidia kivuko  kujiendesha.
"Hao wanaolalalamika nawashangaa, Kigamboni zamani  kitumbua walikuwa wakinunua Sh 50 sasa hivi ni Sh 250 na wananunua.  Mnyika katika jimbo lake la Ubungo kuna kituo cha mabasi ya mikoani  ambako ukimsindikiza tu mtu kuingia pale ni Sh 200 ananishangaza kweli  kwa kupinga ongezeko hili,"alisema Dk Magufuli.
Alisema ni muhimu  wabunge hao na wakazi wa Kigamboni wakafahamu kuwa Dar es Salaam ni ya  watu wote na si ya watu wakuja tu hivyo ni muhimu ikajengwa kwa  mshikamano.
"Ambacho wangetakiwa kikufanya wabunge hawa ni  kutupongeza tulivyopambana na mafuriko ya Dar es Salaam na mimi  kusitisha likizo kuja kuhakikisha madaraja yaliyoharibika yanajengwa  haraka na si kupinga hili," alisema Dk Magufuli.
Mbunge wa  Ubungo, John Mnyika alipotakiwa kuzungumzia kauli hiyo ya Dk Magufuli  alisema hawezi kusema chochote mpaka atakapopata taarifa kamili ya  kilichozungumzwa.
Jumapili, Dk Magufuli alitsema Serikali  imeamua kupandisha nauli kutoka Sh 100 hadi sh 200 kwa safari moja ya  kivuko hicho na kwamba hiyo inatokana na gharama za uendeshaji kuwa za   juu.
Magufuli alisema kivuko cha Magogoni kimekuwa kikitoza nauli  za chini ikilinganishwa na Chato, kinachotoza sh 300, Pangani Sh 200,  Kisorya Sh 300, Lugolora Sh 500, Nyakarilo Sh 3000, Chato-Bukombo Sh  2,000, Kirambo sh 500 na Utete Sh 300, huku wanafunzi wakisafiri  bure.Lakini, mbunge wa Kigamboni Dk Faustine Ndugulile alitoa hoja  kupinga ongezeko hilo.
No comments:
Post a Comment