Daniel Rutoryo.
BEI ya mchele imezidi kupanda Jijini Dar es Salaam kutokana na upatikanaji wa nafaka hiyo kuwa adimu kutoka kwenye vyanzo vyake na sasa bidhaa hiyo inauzwa kwa bei ya Sh2500 tofauti na Sh2200 iliyokuwa bei ya mwishoni mwa mwaka 2011.
Meneja Biashara wa Soko la Kariakoo, Mrero Mgheni amethibitisha hali hiyo na kusema kuwa imesababishwa na upatikanaji adimu wa bidhaa hiyo inayotegemea zaidi msimu na kwamba kwa sasa mahitaji ya mchele ni makubwa kuliko akiba iliyopo .
“Mchele umekuwa adimu kutokana na kipindi hiki si cha msimu wa zao hili, hali hii imepelekea upatikanaji wake sokoni kuwa wa shida sana ndiyo maana bidhaa hii imekuwa ikipanda kutoka mwishoni mwa mwaka jana”. Alisema
Mrero alisema ukilinganisha mchele na bidhaa nyingine zilizopanda mwishoni mwa mwaka jana kama nyanya, karoti, maharagwe, viazi mviringo, kabeji na vitunguu, zimeshuka bei na kuwa bei ya kawaida.
Mrero alielezea hali ya biashara katika soko la kariakoo na kusema kwa sasa hairidhishi kutokana na wateja kutokuwa wengi ukilinganisha na siku za nyuma, hali hii inayosababishwa na maandalizi ya wanafunzi na kupunguza baadhi ya mahitaji kama chakula.
“Hali ya biashara kwa sasa si nzuri sababu kaya nyingi zinafanya maandalizi kwa ajili ya wanafunzi kwenda shule, baadhi ya mahitaji kama chakula yamepungua”. Alisema Mrero.
Mfanyabiashara katika soko la Kariakoo, Aziza Juma kwa upande wake alisema ugumu wa upatikanaji mchele unatokana na bidhaa hiyo kutegemewa na wafanyabiashara wengi kwa kuwa mchele ndiyo chakula kikuu cha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
“Mchele ndiyo bidhaa inayouzika kwa wingi kwani haina Sikukuu wala nini lakini chakushangaza bidhaa hii imekuwa adimu na ghali kupita kiasi na ndiyo inayotulazimu kuuza kwa bei ya juu ili nasi tupate kurudisha faida, hali hii ikiendelea tutakuwa katika wakati mgumu”. Alisema Aziza
Vilevile aliongeza kuwa kusema kutokana na hali iliyopo wakazi wengi wa jijini itafika wakati watashindwa kumudu mahitaji ya familia zao kutokana kupanda kwa hali ya maisha huku thamani ya pesa ikishuka .“Lazima viongozi wetu wachukue hatua za makusudi ili kuimarisha uchumi”. Alisema Aziza.
No comments:
Post a Comment