SHIRIKISHO la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata),  limeiomba Serikali katika mchakato wa kupata Katiba mpya, wapewe Jimbo  la Uchaguzi. 
Pia wametaka watu wenye ulemavu nchini wateuliwe katika Tume ya Maoni ya Katiba mpya, 
Bunge la Katiba na uongozi wa ngazi za juu serikalini kama Ukatibu Mkuu na Ukuu wa Wilaya. 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, katika Ofisi za Waziri Mkuu,  Dar es Salaam, katika mkutano wao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri  Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, waliipongeza Serikali kwa  kuwa sikivu.  
Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Viungo Tanzania, Shida Salum  akichangia hoja katika mkutano huo kuhusu ushiriki wao katika mchakato  wa Katiba mpya, alisema wabunge wenye ulemavu walioko bungeni hivi sasa  wengi wapo kupitia viti maalum na hivyo wanawakilisha 
vyama vyao na si shirikisho. 
“Tunaomba tushirikishwe kwenye Tume na Bunge la Katiba, lakini pia  Serikali itupatie Jimbo letu kama wanavyofanya mataifa mengine kama  Afrika Kusini, hii itaongeza uwakilishi wa masuala yetu ipasavyo,”  alisema Salum ambaye ni mama wa mwanasiasa kijana machachari, Zitto  Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema). 
Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania, Ernest Kimaya, alisema kwa  muda mrefu Serikali imepambana kumaliza mauaji ya albino nchini na  kuomba iteue albino na walemavu wengine wenye sifa kuwa wakuu wa wilaya,  makatibu makuu na nafasi nyingine ili kumaliza vifo na unyanyapaa. 
Awali akisoma tamko la Shivyawata kwa Lukuvi, Mkurugenzi wa  shirikisho hilo, Novath Rukwago aliiomba Serikali pia kuongeza ruzuku  kwa vyama tisa vya walemavu ambayo ni Sh milioni 2.5 kwa mwaka.  
Waliiomba serikali pia kushirikiana nao kufanya utafiti kupitia pia asasi za kiraia kuhusu 
idadi ya walemavu katika mikoa yote nchini baada ya utafiti  mbalimbali kuonesha kuwa baadhi ya mila na tamaduni za mikoa kadhaa  ukiwemo Manyara, zinaashiria watu wenye ulemavu wanauliwa.
No comments:
Post a Comment