Friday, January 6, 2012

Slaa amshukia Rais Kikwete


ASEMA AMESHINDWA KUTATUA MATATIZO YA UCHUMI, AMTUHUMU KUTUMIA SIASA KWA MAMBO MAZITO ASHANGAA MAFISADI EPA WAKITAMBA
Leon Bahati
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa ametoa tathmini ya mwaka mmoja tangu Rais Jakaya Kikwete alipoingia kuongoza nchi katika ngwe ya pili, na kusema mkuu huyo wa nchi ameshindwa kutatua mambo mengi mazito yanayohusu uchumi na maisha ya Watanzania.Akitoa tathimini hiyo jijini Dar es Salaam jana, Dk Slaa aliorodhesha baadhi ya  matukio aliyoita ya kuhujumu uchumi wa nchi pamoja na athari mbalimbali za maisha ya Watanzania.

Dk Slaa ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi aliangushwa na Rais Kikwete, alisema wakati matatizo hayo yakionekana kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania, bado utatuzi wake umekuwa ni wa kisiasa, usiozingatia utaalamu.

Alifafanua kwamba udhaifu katika kukabiliana na matatizo hayo ya kiuchumi, umezidi kuongeza ugumu wa maisha kwa watu wa kipato cha chini huku neema ikielekezwa kwa wachache, wakiwamo watuhumiwa wa ufisadi ambao pamoja na kuwapo na ushahidi wa kuwashitaki, wamekuwa wakikingiwa kifua.

"Tumesikitishwa na hali tete na mwelekeo mbovu wa uchumi wa nchi yetu na kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi kunakoendelea kusababishwa pamoja na mambo mengine, mfumuko wa bei na thamani ya shilingi kutokuwa imara. Hali hii siyo tu ni tishio kwa maisha ya wananchi bali pia kwa usalama wa nchi kwa ujumla," alisema Dk Slaa.

Alisema hata hotuba ya mwaka mpya aliyotoa Rais Kikwete, alishindwa kueleza hatua thabiti na za haraka za Serikali katika kukabiliana na hali mbaya na uchumi.

"Badala yake aliendelea na utaratibu uleule wa hotuba zake za kuorodhesha visingizio vya nje vya uchumi wa dunia bila kuweka mkazo katika kuelekeza hatua za kuinua uchumi wa ndani pamoja na kulinda wananchi dhidi ya misukosuko ya nje," alilalamika Dk Slaa.

Huku akisisitiza kuwa ana nakala ya hotuba ya Rais Kikwete na ameisoma kwa makini, alisema  siyo kweli kwamba hali ya mbaya ya uchumi imesababishwa na tatizo la uchumi wa dunia kama alivyosema mkuu huyo wa nchi, bali ni uzembe unaotokana na watendaji wake.

Kutokana na Chadema kutoridhika na hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii iliyopo nchini kwa sasa, Dk Slaa alisema Kamati Kuu ya chama hicho imeitisha kikao kitakachofanyika Januari 22, mwaka huu kuangalia njia za kuchukua kuwalinda Watanzania.

Alisema matatizo yote ya kiuchumi yatajadiliwa na kufanya uamuzi wa hatua muafaka za kuchukua, ili kusimamia uwajibikaji wa Serikali kwa maslahi ya umma.

Mtendaji mkuu huyo wa Chadema, alisema kwa sasa hali inaonekana kuwa Serikali inatatua matatizo ya nchi kisiasa zaidi kuliko kutumia wataalamu wake katika kuweka mikakati imara iliyobuniwa kisayansi.

Alitoa mfano kwamba, uhaba wa sukari unaolikumba taifa kwa sasa hauwezi kutatuliwa kwa kununua sukari nje na kuitoa kwa mgawo kwani kunaongeza tatizo badala ya kuliondoa.

Dk Slaa alidai kwamba ana vielelezo vingi vya siri vinavyohusu Serikali, na kwamba utawala wa Rais Kikwete unaogopa kusema ukweli kuhusu sababu zinazosababisha uchumi wa nchi kudorora huku gharama za maisha zikipanda kila kukicha.

Alifafanua kwamba Serikali inashindwa kueleza ukweli wananchi kuhusu, "Hali mbaya ya kifedha ambayo inalikabili Taifa hivi sasa kwa kupungua kwa mapato ya ndani na nje, ukilinganisha na bajeti iliyopitishwa."

Dk Slaa alisema Serikali imeshindwa kueleza mpango wake wa kuongeza uzalishaji na kupunguza matumizi yake.

Alionya kwamba, baadhi ya viongozi wa Serikali wameendelea kujineemesha kwa kujiongezea malipo huku wakizidi kuongeza bei ya huduma za msingi, zinazotolewa na taasisi zake.

Ingawa Dk Slaa hakuweka wazi suala hilo, lakini nyongeza ya posho za wabunge kwa sasa zimekuwa zikitikisa taifa. Posho za vikao za wabunge ziliongezeka kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku kwa kigezo cha kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma.

Dk Slaa alirejea kuonya, "Hali hii ikiachwa iendelee itakuza pengo la wenye nacho na wasio nacho katika taifa na wakati huo huo itaongeza zaidi gharama za maisha kwa wananchi hususani wa kipato cha chini, tofauti na ahadi ya Rais Kikwete na CCM ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania."

Ufisadi
Dk Slaa alisema Serikali imeonyesha udhaifu mkubwa katika kushughulikia matatizo ya ufisadi, ambayo yamelikabili taifa na kusababisha mabilioni ya fedha za umma kuchukuliwa na wachache.

Alisema licha ya watuhumiwa kufahamika wazi na kwamba chama hicho kiliwatangaza hadharani, hakuna hata mmoja aliyechukuliwa hatua.

Alisema Sh70.7 bilioni zilizorejeshwa na waliozichota kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), hadi sasa hazijulikani zilikoenda jambo ambalo tayari taasisi za kimataifa zimeingilia kati na kuitaka Serikali itoe maelezo.

Dk Slaa alisema Watanzania wengi, wakiwepo waandishi wa habari wanaelekea kusahau sakata la marejesho ya fedha za EPA, lakini mataifa yanayochangia bajeti ya Serikali wamekuwa wakihoji suala hilo.

Alisema ana barua iliyoandikwa kwa Serikali ikihoji ziliko fedha hizo ambazo ni sawa na asilimia 54 ya fedha zote zilizochotwa kwenye akaunti hiyo ya EPA, mwaka 2004/05.

Katika kuthibitisha kwamba Serikali imekuwa ikiwakingia kifua watuhumiwa wa ufisadi ili wasichukuliwe hatua, alitoa mfano chama chake kiliwasilisha kwa Mkurugezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ushahidi dhidi ya mtuhumiwa wa ufisadi wa ununuzi wa rada.

Kwenye ushahidi huo ambao uliambatanishwa na vielelezo vya uchunguzi wa Taasisi ya Uingereza ya Kuchunguza Makosa ya Jinai (SFO), Dk Slaa alisema zilionyesha jinsi mtuhumiwa alivyojipatia Sh1 bilioni na kuziweka kwenye akaunti nchi za nje.

Alisema hali hiyo inashangaza kwani  watu wa kawaida wanaotenda makosa hata kwa kuhisiwa tu wanakamatwa na kupelekwa mahabusu kabla ya kufikishwa mahakamani, lakini vigogo wa Serikali wanaonekana kulindwa.

 Dk Slaa alisema wananchi wanataabika kutokana na migogoro mbalimbali ikiwepo ya ardhi, elimu, afya na maji.

Alisema migogoro hiyo inashindwa kutatuliwa kwa sababu badala ya kushughulikia chanzo, Serikali imekuwa ikitafuta ufumbuzi wa matokeo yake.

Dk Slaa alitoa mfano wa migogoro hiyo ya ardhi kuwa ni ile kati ya wananchi na wawekezaji, wakulima na wafugaji na ile ambayo Serikali yenyewe imejikuta ikipambana na raia wake.

Migogoro mingine, alisema ni ya wanafunzi wa vyuo vikuu, lakini akasema tayari amewasiliana na Umoja wa Vijana wa chama hicho (Bavicha) kufuatilia kwa ukaribu suala hilo ili kuweka wazi hatua muafaka zinazopaswa kuchukuliwa.

No comments:

Post a Comment