Friday, January 20, 2012
Mbunge mwingine afariki
NI JEREMIAH SUMARI WA CCM KUAGWA KESHO KARIMJEE
Fredy Azzah na Patricia Kimelemeta
SIMANZI nyingine imelikumba Bunge la Tanzania, kufuatia kifo cha Mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), Jeremiah Solomon Sumari (60),aliyefariki dunia usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa muda mrefu akipatiwa matibabu.
Kifo cha Sumari kimetokea siku moja tu, tangu kufanyika kwa mazishi ya Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema aliyefariki dunia kwa ajali ya gari, Jumamosi iliyopita katika eneo la Ruvu mkoani Pwani.
Sumari alianza kuugua kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hali ambayo ilimfanya aende kampeni katika mazingira magumu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mtoto wa kwanza wa marehemu, Sioi Sumari alisema baba yake alipatwa na mauti katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alipokuwa amelazwa.
“Baba amefariki saa 8.30 usiku katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu,” alisema Sioi.
Alifafanua kuwa, marehemu anatarajiwa kuzikwa Jumatatu ijayo kijijini kwake katika jimbo la Arumeru Mashariki.
Mtoto huyo wa marehemu alisema baba yake utaagwa kesho (Jumamosi ) jijini Dar es Salaam, kabla ya kusafirishwa kwenda Arusha.
Ofisi ya Bunge Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema ofisi ya Bunge imepokea kwa masikitiko msiba huo kwani umetokea muda mfupi tangu waliporejea kutoka kwenye maziko ya Mtema.Hata hivyo, alisema kutokana na hali hiyo shughuli za Bunge zitaendelea kama zilivyopangwa na kwamba, zitasimamishwa siku ya kuaga mwili wa marehemu.
“Leo (jana) na kesho tutaendelea na shughuli za bunge kama kawaida, lakini siku ya kuaga tutasitisha shughuli ili kutoa fursa kwa wabunge kushiriki kwenye mazishi ya marehemu Sumari,” alisema Dk Kashililah. Alisema kwa sasa wanafanya taratibu za mazishi ya marehemu kwa kushirikiana na familia yake.
Alifafanua kwamba kutokana na hali hiyo, bunge limepata pigo kubwa baada ya kuondokewa na wabunge wawili katika kipindi kimoja, jambo ambalo limesababisha wabunge kushikwa na butwaa.Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge itakutana leo kujadili namna ya kuratibu mazishi ya mbunge huyo.
Alisema kuna uwezekano mbunge huyo akaagwa katika ukumbi wa Karimjee, kama ilivyofanyika kwa mbunge wa Chadema Regia Mtema.
“Tunasikitika sana kwa kuwapoteza wabunge wawili ndani ya muda mfupi,” alisema Ndugai.
Kikwete amlilia
Kwa upande wake, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge, Anne Makinda kutokana na kifo cha Sumari.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilimnukuu Rais Kikwete ikisema; “Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Jeremia Solomon Sumari….”
“Alikuwa kiongozi aliyewatumikia vema wananchi wa Jimbo lake la Uchaguzi la Arumeru Mashariki na Taifa kwa ujumla katika wadhifa wake wa Waziri kwa umahiri na uhodari mkubwa.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete alisema kutokana na kifo cha Sumari, wananchi wa Arumeru Mashariki wamepoteza kiongozi wa kutegemewa. “Kwa moyo dhati, natuma salamu za rambirambi na pole kwa familia ya marehemu Jeremia Sumari kwa kumpoteza kiongozi na mhimili madhubuti wa familia,” taarifa hiyo ilimnukuu Rais Kikwete. Alifafanua akisema; “Ninawahakikishia kwamba nipo pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa na namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema aipumzishe roho ya marehemu Jeremia Solomon Sumari mahali pema peponi, Amina.”
Lowassa amlilia
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa alisema taifa limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na Sumari.
“Alikuwa mchapakazi sana.., hii imesababisha kuteuliwa kuwa Naibu Waziri katika serikali ya awamu ya nne, kutokana na umahiri wake,” alisema Lowassa.
Lowassa aliongeza kwamba, kutokana na hali hiyo, wananchi wa Arumeru Mashariki wamekosa mwakilishi wa kutetea maslahi yao bungeni.
Historia yake
Sumari alizaliwa Machi 2 mwaka 1943, katika kijiji cha Akeri wilayani Arumeru mkoani arusha.
Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Meru Magharibi kati ya mwaka 1950 na 1957. Kati ya mwaka 1958- 1964 alisoma katika shule ya sekondari ya Old Moshi, mkoani Kilimanjaro na baadaye aliendelea na elimu ya juu nchini Uingereza.
Taarifa zinaonyesha kuwa, Sumari alipata elimu ya masoko kwa ngazi ya cheti ACCA, CIS, (Certificatein Marketing and Lincesed Broker lr), nchini Uingereza na baadaye kupata CPA nchini.
Kwa upande wa utumishi wake, mwaka 1996 mpaka 2004 alikuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Boko la Disa Dar es Salaam (DSE).
Kisiasa , kuanzia mwaka 2005 mpaka mauti yalipomkuta alikuwa Mbunge wa jimbo hilo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CCM.
Januari 4 mwaka 2006, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana na mwaka 2008 mpaka 2010 alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment