Saturday, January 21, 2012

Mchakato kutafuta mrithi wa Regia Mtema waanza


Aziza Masoud na Ellen Manyangu
WIKI moja tangu kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema kilipotokea, mchakato wa kumtafuta mrithi wa nafasi yake umeanza.

Regia alifariki dunia Jumamosi iliyopita kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu mkoani Pwani na kuzikwa Jumatano wiki hii nyumbani kwao Ifakara, mkoani Morogoro.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zinasema tayari maofisa husika ndani ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wameanza kushughulikia suala hilo la kuziba nafasi ya mbunge huyo kijana ambaye pia alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Mallaba alisema jana kwamba ofisi yake itatumia orodha ya majina yaliyopendekezwa na Chadema mwishoni mwa mwaka juzi.

“Nadhani tunayo orodha ya mapendekezo ya Chadema, basi kwa jinsi taratibu zilivyo, tutarejea katika orodha hiyo na pale tulipopitisha msitari ndipo tutakapoanzia, lakini lazima huyo anayefuata katika orodha awe na sifa za kuwa mbunge,” alisema Mallaba kupitia simu yake ya kiganjani.

Hata hivyo, Mallaba alisema hivi sasa ni mapema mno kufahamu ni lini uteuzi huo utafanyika na kwamba taratibu za ndani zikikamilika, mamlaka husika zitaarifiwa ili umma pia uweze kufahamu.

Awali, Mallaba alikataa kuonana na waandishi wa habari na mmoja wa maofisa wa Tume hiyo alisema: “Amesema majina yametoka hukohuko Chadema ndipo yakaja huku kwa hiyo kama mnayahitaji mnapaswa kwenda katika ofisi za Chadema ili muweze kupata majina hayo.”

Dk Slaa, Zitto wanena
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema chama chake hakifahamu atakayechukua nafasi hiyo na kwamba hiyo inatokana na ukweli kwamba jukumu hilo liko mikononi mwa NEC.

“Majina ya wagombea wa viti maalumu yapo NEC na wao ndiyo wanaoangalia kuchagua nani anayefuata katika orodha iliyopo Tume, kwa utaratibu, mgombea anayefuata ndiye atakayechukua nafasi hiyo,” alisema Dk Slaa.

Alisema Chadema kilipeleka NEC orodha ya majina 28 ya wabunge wa viti maalumu, Desemba 30, 2010 na kati ya hayo majina 25 tayari wameshachaguliwa ni jukumu la NEC kuangalia jina gani linalofuata kwenye orodha hiyo iliyopo.

Alisema kati ya hayo majina matatu yaliyobaki yeyote atakuwa na uwezo wa kuchukua nafasi hiyo kulingana na vigezo vya NEC na kulingana na utaratibu na Katiba ya Chadema.

“Sina mamlaka ya kujua nani anayefuata na ofisini kwangu hata majina sina majina yapo NEC mimi nawategemea wao waniletee  jina kwa mujibu wa taratibu zao nitaliangalia kama muhusika bado ni mwanachama hai nitawajibu na nitawarudishia na ndiyo watalitangaza kwa wananchi,” alisema Dk Slaa.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, jina watakalopewa kama muhusika atakuwa amefukuzwa katika chama, basi jina litakalofuata baada ya huyo mwanachama ndilo litakaloandikwa na kufanyiwa kazi.

Alisema si rahisi kwa NEC kumtangaza mrithi wa nafasi hiyo bila kuwasiliana kwanza na chama na kuthibitisha kuwa bado ana sifa za kushika nafasi hiyo.

Alisema NEC inajua wazi kuwa haiwezi kumtangaza mtu moja kwa moja pasipo baraka za chama kwa sababu siku hizi kumekuwa na wimbi la migogoro ndani ya vyama vya siasa nchini na wengine kujivua uanachama au kufukuzwa.

Wakati Dk Slaa akisema jukumu hilo ni la NEC, Naibu Katibu wake,  Zitto Kabwe alitaja jina la mmoja wa madiwani wa viti maalumu wa chama hicho kuwa ndiye anayefuata katika orodha iliyopelekwa NEC.

Akizungumza jana, Zito alisema kwa mujibu wa orodha yao ya viti maalumu anayefuata baada ya wabunge walioteuliwa mwaka juzi ni diwani huyo ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa.

“Kwa mujibu wa orodha tuliyonayo ya wabunge wa viti maalumu anayefuata baada ya Regia ni diwani kutoka (anataja wilaya na jina lake), ndiye atakayechukua nafasi ya kiti hicho kilichoachwa na marehemu,” alisema Zitto.

No comments:

Post a Comment