Tuesday, January 3, 2012

Bunge halijamalizana na Luhanjo, Jairo


Fredy Azzah
LICHA ya aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kung’atuka kwenye nafasi zao, Bunge limesema linasubiri ripoti ya utekelezaji wa maagizo yake juu ya kuwajibishwa kwao.
Msimamo huo wa Bunge umekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Balozi Ombeni Sefue kuwa Katibu Mkuu Kiongozi na Eliakim Maswi, ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya Jairo, kushika nafasi hiyo rasmi. Luhanjo alistaafu kwa mujibu wa sheria Desemba 31 mwaka jana.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema juzi kwamba pamoja na hatua hiyo ya Serikali, bado Bunge linasubiri utekelezaji wa maazimio yake ambayo yanapaswa kuwasilishwa bungeni na Serikali katika Mkutano wake wa mwezi ujao.
“Kamati teule ilisoma ripoti yake bungeni na Serikali ikaomba ipewe muda wa kutekeleza maazimio ya Bunge. Tunasubiri katika Bunge la Februari pamoja na mambo mengine, Serikali isome utekelezaji wake juu ya maazimio ya Bunge,” alisema Ndugai.
Hii si mara ya kwanza kwa Serikali kupiga danadana maazimio ya Bunge. Wakati wa sakata la Richmond, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika na aliyekuwa Katibu wa Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, walishindwa kuwajibishwa kama Bunge lilivyoazimia hadi walipostaafu.
Pia hadi sasa, Serikali haijatekeleza azimio la Bunge kuhusu Richmond lililotaka mamlaka ya juu kumwajibisha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah.
Alipoulizwa Ndugai endapo kustaafu kwa Luhanjo na kuondoka kwa Jairo katika nafasi zao kama hakutaathiri utekelezaji wa maazimio ya Bunge kama ilivyokuwa kwa Richmond, alijibu: “Sitaki kuzungumza chochote juu ya hilo, lakini siku zote mtu muungwana huwa anakuwa na subira. Tusubiri muda tuliopeana na Serikali uishe na sasa hata hayo maswali nitaweza kuyajibu.”
Lissu: Tunasubiri ripoti
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, alisema kambi hiyo haitafumbia macho hali yoyote itakayoonyesha nia ya kutaka kutoyatekeleza maazimio ya Bunge.“Tunasubiri wailete hiyo ripoti yao bungeni, wakija na maelezo ya ubabaishaji sisi kambi ya upinzani tutapambana nao,” alisema.
Alisema Serikali inafanya siasa katika jambo hili na inataka kuwaamisha wananchi kwamba viongozi hao wameondoka kwenye nyadhifa zao katika utaratibu wa kawaida.“Ukweli ni kuwa hawa watu wameondoka katika nafasi zao kwa aibu wakiwa na kashfa ripoti ya Bunge inaonyesha wazi hilo,” alisema Lisu.
Hata hivyo, wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe alisema Serikali itawasilisha utekelezaji wa maazimio ya Bunge katika Mkutano wa Februari kama ilivyoahidi.

Sakata lilivyokuwa
Novemba 19, mwaka jana Kamati Teule ya Bunge, ilipendekeza Serikali imchukulie hatua za kinidhamu Jairo kwa matumizi mabaya ya madaraka, kukusanya na kutumia fedha za Serikali kinyume cha sheria.
Kamati hiyo, iliundwa na Bunge kwa ajili ya kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini, kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti ya 2011/12, bungeni.
Pamoja na Jairo pia Kamati ilipendekeza Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na watumishi wote wa wizara hiyo, waliotajwa kwenye taarifa hiyo, nao wawajibishwe na hasa Ngeleja, kwa kuwa kwa mujibu wa Mwongozo wa Baraza la Mawaziri, ndiye Msimamizi Mkuu wa Wizara.
Kwa upande wa Luhanjo, Kamati hiyo ilielezea kusikitishwa kwake na kitendo chake cha kutoa kwenye vyombo vya habari taarifa za kumsafisha Jairo kabla ya kuifikisha kwanza ripoti yake bungeni, kwa kuwa huko ndiko hoja ilikoanzia.
Ilisema Katibu Mkuu Kiongozi aliamua kwa makusudi kumsafisha Jairo kwa kuficha ukweli na kutangaza kuwa hakuwa na kosa la kinidhamu, kitendo ambacho kimeupotosha umma.
Kamati hiyo iliundwa baada ya Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), kuibua hoja kwamba Jairo alichangisha takriban Sh bilioni moja kutoka taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa ajili ya bajeti bungeni huku akiwa na ushahidi wa barua.

No comments:

Post a Comment