Ibrahim Yamola
MAMLAKA ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji (Ewura) , imesema imekamilisha taratibu zote zinazohitajika za kutangaza bei mpya ya umeme na kwamba sasa inajipanga kufanya hivyo, mwanzoni mwa Januari. Ofisa Habari wa Ewura, Titus Kaguo alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa hiyo ni baada ya Bodi ya wakurugenzi kukaa na kupitia hoja za Tanesco na wadau mbalimbali kuhusu suala hilo na kujiridhisha.
“Bodi ya Wakurugenzi ilikutana Disemba 15 na 16 mwaka huu ili kupitia maombi ya Tanesco na wadau hivyo bodi imeamuru kufanyika kwa uchunguzi ambao utatoa majibu sahihi kwa lengo la kutomuumiza mwananchi na mwekezaji,” alisema Kaguo.
Kaguo aliongeza kuwa mchakato uliopo sasa ni mgumu kwani ni hatua ambayo itaamuru hatma ya nini kifanyike kwa makusudi ya kutoathiri wadau wa huduma hiyo na kwamba bei hiyo itatangazwa mwakani na siyo mwisho mwa mwaka huu kama awali alivyosema. Alifafanua kuwa nia ya Ewura ni kuhakikisha wananchi wake na wawekezaji wanakuwa na usawa katika ufanisi wa kutoa na kupokea maoni kwa pande zote na kwamba ndiyo maana bodi ikaamua kufanyike uchunguzi huo.
“Tuko makini kuhakikisha usawa wa huduma hii muhimu kwa jamii haiathiri pande hizi mbili ambazo kimsingi zinategemeana katika utendaji wake wa kazi hivyo nawaomba wananchi wawe wavumilivu wakati tukikamilisha zoezi zima la uchunguzi,” alisema Kaguo.
Hatua hiyo inafanyika kufuatia Tanesco kuwasilisha Ewura mapendekezo ya kupandisha gharama za umeme kwa bei ya wastani ya kuuza umeme iliyopo sasa ya Sh141 kwa uniti hadi Sh359 kwa uniti kuazia Januari mwakani ambapo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 155 ya bei ya sasa.
Mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando alisema sababu ya kutaka kupandisha bei hiyo ya umeme ni kuliwezesha shirika hilo kukabiliana na ongezeko la gharama za uendeshaji ili kuondokana na mgao wa umeme.
Mhando alisema athari ambazo zitapatikana ikiwa bei haitaongezwa ni pamoja na Shirika kushindwa kufanya uwekezaji na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya kuuganisha wateja wapya.Hata hivyo wadau mbalimbali wa umeme walipinga hatua hiyo wakisema nyongeza itayumbisha uchumi wa taifa na kulitaka Shirika liimarishe kwanza uzalishaji wa umeme ili liweze kupata faida.
Wadau hao walisema Tanesco ina hali ngumu ya kifedha kutokana na mgawo na kwamba mkakati uwe ni wa kuongeza uzalishaji ili watu wautumia na hapo ndipo wataweza kujiimarisha na kujikusanyia mapato mengi kuliko njia hii wanayo taka kuitumia ya kupandisha bei.
No comments:
Post a Comment