Wednesday, December 28, 2011

‘Makundi maalum yasaidiwe ipasavyo’

Patricia Kimelemeta

JAMII imetakiwa kusaidia makundi maalum ya walemavu ili waweze kupata mahitaji muhimu ikiwemo vifaa vya kufanyia kazi kutokana na ulemavu wao, jambo ambalo litawawezesha kuondokana na utegemezi.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na walemavu ya Unity in Diversity Foundation (UDF) Enock Bigaye wakati wa kukabidhi baiskeli 400 za walemavu zenye thamani ya Sh120 milioni.
Alisema walemavu wanahitaji msaada wa hali na mali ili waweze kuendesha kazi zao, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kupunguza utegemezi katika maisha, hivyo jamii inapaswa kutambua na kuwa nao karibu.

“Jamii inapaswa kutambua kuwa walemavu ni kundi muhimu linalohitaji msaada wa ari na mali ili waweze kuendesha shughuli zao, jambo ambalo linaweza kuwapunguzia hali ya utegemezi, kutokana na hali hiyo wanapaswa kuwa nao karibu,” alisema Bigaye.
Aliongeza kuna baadhi ya taasisi zinashindwa kufanya kazi yake ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuchukua misaada kwa wafadhili na kushindwa kuwasilisha kwa walengwa, jambo ambalo limesababisha baadhi ya wafadhili kugoma, kutokana na hali hiyo jamii inapaswa kubadilika ili waweze kujenga uaminifu.
Alisema, mpaka sasa taasisi yake imeweza kuwafikia walemavu zaidi ya 3,500 kutoka mikoa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukadhibi misaada hiyo, jambo ambalo linafaa kuigwa na wadau wengine.
Alisema taasisi yake ni miongoni mwa taasisi zinazopata misaada mbalimbali kutoka kwa wafadhili na kuhakikisha kuwa misaada hiyo inafika kwa walengwa kwa wakati jambo ambalo limeweza kuwajengea uaminifu.

Alisema mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa wanashirikiana na wadau mbalimbali ili waweze kuwasaidia walemavu hao na kuwabaini walio majumbani ili waweze kuwasaidia

No comments:

Post a Comment