Wednesday, December 21, 2011

Mvua ya radi yaua watano


MVUA kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana mkoani Dar es Salaam ikiambatana na radi,
imesababisha maafa ya vifo vya watu watano na kuwaacha wengine wengi wakiwa hawana makazi kwa sasa.

Mvua hiyo iliyonyesha kwa zaidi ya saa tatu, mbali na vifo pamoja na majeruhi hao, pia imesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na madaraja pamoja na mali
yakiwemo magari, ambapo hata hivyo thamani yake haijajulikana.

Hali imeonekana kuwa mbaya zaidi kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mabondeni ambao baadhi yao walinusurika kupoteza maisha yao baada ya vikosi vya Uokoaji na Zimamoto vya
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kufika katika maeneo hayo na kutoa msaada wa kuwaokoa.

Mvua hiyo iliyoanza kunyesha kuanzia saa 10 alfajiri, pia imesababisha mamia ya watu kukosa
mahali pa kulala baada ya nyumba zao kujaa maji kutokana na mvua hiyo.

Akizungumza matokeo ya mvua hiyo ambayo pia ilisababisha tatizo kubwa la usafiri jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Said Mecky
Sadiki alisema hadi kufikia saa 10 jioni, maiti wanne akiwemo ya mtoto mchanga walipatikana.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Ibrahim Tulihama (65), mkazi wa Ubungo Msewe, Maganga Said (10-15) mkazi wa Mbagala aliyekufa baada ya kudondokewa na nguzo ya umeme, Gathi Mseti (39) wa Mburahati pamoja na mtoto mchanga ambaye hata hivyo hajatambulika.

Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alimtaja mtu
mwingine aliyekufa kuwa ni Viane Maxmillia (13) ambaye alikutwa chini ya uvungu wa kitanda
katika eneo la Mburahati.

Aidha, Kova alisema mtoto mchanga ambaye jina na umri wake havijafahamika, aliokotwa katika eneo la Mtogole, Tandale akiwa amesombwa na maji.

Mkuu wa Mkoa Sadiki alisema majeruhi wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ilala ya
Amana wakiendelea na matibabu.

Aidha, alisema kutokana na taarifa walizozipata kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), mvua hizo zitaendelea kunyesha na hivyo kuwataka wakazi wa maeneo ya mabondeni kuondoka ili kuepuka madhara zaidi yanayoweza kuendelea kutokea.

Aliyataja maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua hiyo ambayo pia yalishuhudiwa na gazeti hili
kuwa ni Jangwani, Mburahati, Kigogo, Tabata, Buguruni Mnyamani, Tandale, Mtogole, Manzese, Ubungo External, Loyola, Msasani Bonde la Mpunga, Riverside na Magomeni Chini.

Eneo la Jangwani na Kigogo pamoja na Mburahati, ndiyo yaliyoathirika zaidi na mvua hiyo, kwani ilisababisha nyumba za wakazi wa maeneo hayo kuzingirwa na maji yaliyowafanya
baadhi ya wananchi wanaoishi katika makazi hayo kujiokoa kwa kupanda juu ya mapaa ya
nyumba.

Katika eneo la Kigogo, gazeti hili lilivishuhudia vikosi vya Uokoaji na Zimamoto vya Jiji vikinusuru maisha ya mama mmoja na watoto wake sita, waliokuwa wameanza kuzama baada ya nyumba waliyokuwa wamekaa juu ya paa kubomoka.

“Hali ni mbaya sana, hapa tunapozungumza bado kuna watu wapo ndani ya nyumba zao
wamezuiliwa na maji kutoka, wanahitaji msaada ili kuokolewa,” alisema mmoja wa wananchi
aliyekuwepo eneo hilo ambaye hata hivyo hakuwa tayari kujitambulisha jina lake.

Polisi waliokuwa katika magari na helikopta pia waliungana na vikosi vya Uokoaji kufanya
doria katika maeneo yaliyokumbwa na madhara ili kuangalia namna ambavyo wangeweza kutoa msaada katika tukio hilo.

Mkuu wa Mkoa amewataka wakazi waliopo katika maeneo yote ya mabondeni kuondoka
haraka ili kuepuka madhara yanayoweza kuwakuta kabla ya hatua zaidi za kuwahamisha kwa nguvu hazijachukuliwa dhidi yao.

Mkoani Dodoma, Sifa Lubasi anaripoti kuwa mvua kubwa iliyoambatana na upepo imeziacha
kaya zaidi ya 74 zenye watu 269 katika kata za Ntyuka na Iyumbu katika Manispaa ya Dodoma,
zikiwa hazina mahali pa kuishi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma, Nicolaus Buretta mvua hiyo ilinyesha usiku wa kuamkia juzi.

Alisema kutokana na hali hiyo, tayari Kamati ya Maafa ya Halmashauri imejipanga kwa ajili ya
kuwasaidia waliopatwa na maafa hayo kwa kutoa chakula na mahema kwa ajili ya kujihifadhi.

Alibainisha kuwa zaidi ya wakazi 269 kutoka katika vitongoji vitano vya Kata ya Ntyuka
wameachwa katika mazingira magumu baada ya mali zao ikiwemo vyakula kuharibiwa. Pia nyumba ya Mganga wa Zahanati ya Kata ya Ntyuka pamoja na zahanati hiyo zimeezuliwa na upepo.

Wakati huohuo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Fulgence Ngonyani
amesema kutokana na mvua kubwa hiyo kubwa daraja na reli eneo la Gulwe wilayani Mpwapwa limeharibika.

Shirika la reli nchini jana lilitangaza kuahirisha safari ya treni kutokana na uharibifu huo.

No comments:

Post a Comment