JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imepanga kukarabati reli ya kati ili kuweza kuendeleza sekta ya reli nchini hapa kutokana na kutoridhishwa na maendeleo ya sekta hiyo. Reli hiyo ni moja ya miradi iliyopewa kipaumbele kati ya miradi 244 katika uendelezaji wa sekta ya miundombinu ya kiuchumi katika nchi wanachama wa EAC katika kipindi cha miaka 10.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii wa Wizara ya Afrika Mashariki, Dk Barthlomeo Rufunjo alisema kasi ya uendelezaji wa sekta ya reli nchini si ya kuridhisha kutokana na changamoto zilizopo.
“Kasi ya uendelezaji wa sekta ya reli ndani ya nchi yetu hairidhishi na hii inatokana na changamoto zinazoendelea kuikabili sekta hii, Baraza la Mawaziri wa sekta hiyo ndani ya EAC limeagiza kuchukua hatua za kuendeleza sekta hii nchini,” alisema Rufunjo.
Alisema baraza hilo liliridhia sekretarieti ya jumuiya hiyo ifuatilie kwa karibu msaada ulioahidiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ukiwa na lengo la nchi wanachama kuteua wataalamu wa masuala ya reli kufanikisha shughuli hiyo.
Rufunjo alisema wataalamu hao watasaidiana na sekretarieti iliyoteuliwa katika kuendeleza hatua mbalimbali za kuendeleza reli katika nchi tano ambazo ni wanachama wa EAC. Alisema miradi mengine iliyopewa kipaumbele ni sekta ya usafiri wa majini na bandari kutokana baada ya kuonekana haijapiga hatua ya kurudhisha katika ngazi ya jumuiya.
“Msukumo mpya wa kuiendeleza sekta hii ni pamoja na kuandaa mkakati wa uendelezaji kwa Baraza la Mawaziri kupitisha hadidu za rejea za maandalizi ya mkakati huo,” alisema Rufunjo.
Alisema katika kuimarisha sekta ya utabiri wa hali ya hewa wataalamu wa majanga, wataalamu wa hali ya hewa nchini watapata fursa ya kwenda kujifunza katika Kituo cha Utabiri na Majanga (ICPAC) kilichopo Nairobi nchini Kenya.
Alisema katika mkutano wa saba wa Baraza la Mawaziri uliofanyika Oktoba mwaka huu Mombasa ulijadili hali ya upatikanaji wa umeme na utekelezaji wa mpango kabambe wa umeme wa jumuiya na kupokea taarifa juu ya hatua mbalimbali zilizofikiwa na nchi wanachama. “Mradi huu utahusika katika uendelezaji wa sekta ya nishati na upatikanaji wa nishati endelevu ya mafuta na umeme ili kuweza kuondoa tatizo hilo katika nchi wanachama,” alisema Rufunjo.
Alisema kuwa katika uchunguzi ilibainika kwamba changamoto zilizokuwepo katika sekta hiyo ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, ukuaji wa matumizi kutokana na ongezeko la mahitaji na uwekezaji mdogo katika sekta hiyo.
Pamoja na miradi hiyo mkutano huo pia ulipokea upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kampala hadi Kigali na kuendelea hadi Bujumbura.
No comments:
Post a Comment