Wednesday, December 21, 2011

Viongozi dhalimu komeni

Na editor
 
Maoni ya Mhariri
TAARIFA za viongozi wa serikali ya wilaya ya Meatu “kufungia wananchi” ili wasitoe malalamiko yao kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kapteni George Mkuchika zinasikitisha sana.
Kwa kuamini kwamba siri waliyoitunza haitafichuka kwa namna yoyote ile, viongozi hao chini ya Mkuu wa Wilaya yao wakajikuta wanaadhirika. Wananchi walivujisha “siri” hiyo kwa waandishi wa habari ambao walimsimulia waziri kama anafahamu suala hilo.
Zaidi ya askari polisi 30 waliobeba silaha za moto pamoja na mabomu ya kutolea machozi, walizingira kijiji cha Mwangudo kabla ya kuwasili kwa Waziri Mkuchika, na kuwaweka mahabusu kwa saa kadhaa kwa madai kuwa kulipangwa njama za kuvuruga ziara ya waziri huyo.
Siri ikafichuka kwamba polisi waliwataka wananchi hao wema wasieleze kile walichotendewa wakati wa operesheni ya serikali kuhamisha kwa nguvu wakazi katika maeneo yanayodaiwa kuwa ni ya hifadhi ya taifa. Wananchi walitoa siri hiyo kwa waandishi wa habari na kumweleza Waziri Mkuchika.
Tangu mwanzo kulikuwa na mipango ya kuzuia uhuru wa wananchi kujieleza. Hizo ni hatua za kidikteta na zisizofikirika za kuficha ukweli wa mambo.
Kwa jinsi viongozi walivyokuwa mahayawani, baada ya kuwafungia katika mahabusu wananchi wenye akili zao na familia zao, viongozi hao wakapanga wananchi waliowashurutisha maelezo ya kuyatoa mbele ya Waziri Mkuchika. Maelezo ya kupanga yaliashiria kuwa eneo hilo hakuna tatizo lolote na kwamba operesheni hamisha wakazi iliendeshwa vizuri.
Huu ni uhuni usio na sababu kwa viongozi wanaojiheshimu na kutambua wajibu wao. Sasa zimefichuliwa taarifa kwamba wakati wa operesheni hiyo, nyumba za wananchi zilichomwa moto, vyakula vyao vikateketea pamoja na mali nyingine mbalimbali.
Kitendo kilichofanywa na viongozi wa wilaya ya Meatu ni kibaya na kinachohitaji uchunguzi makini. Wananchi wamekuwa wakilalamikia vitendo vya kinyama wanavyotendewa na operesheni mbalimbali za serikali, kumbe bado kuna viongozi wanadhani wanayo haki ya kudhalilisha raia kwa visingizio visivyo mashiko.
Mpaka sasa serikali haijalipa fidia wananchi wa Mbarali na maeneo mengine waliodhalilishwa kwa kufukuzwa na mifugo yao hadi ikaporwa na mingine kufa njiani kwa njaa. Vivyo hivyo kwa wananchi wa Kimasai wa maeneo ya Loliondo waliochomewa makazi yao na polisi wa serikali. Udhalilishaji wa namna hiyo umefanywa pia Kilosa na miezi miwili iliyopita kijijini Njedengwa, mkoani Dodoma ambako polisi wa serikali walisimamia uvunjaji wa nyumba za raia bila ya uhalali wowote wa kisheria.
Ni wapi serikali inajificha na kujivuna kuwa inaongoza kwa misingi ya utawala bora na kuzingatia sheria? Wakati tunataka uchunguzi ufanywe katika tukio la Mwangudo, wilayani Meatu, tunataka pia viongozi wa serikali, wa ngazi yoyote ile, wakome kudhalilisha raia. Tunajua hatuna polisi wala waendesha mashitaka wala mahsakama au gereza la kushughulikia viongozi madhalimu kama hawa, lakini tunaahidi kuwafichua kadiri tunavyopata taarifa ili waone aibu machoni kwa wananchi. Huenda hiyo itakuwa dawa yao baada ya kuridhika kwamba serikali ngazi za juu haiguswi na udhalimu wa viongozi wake.

No comments:

Post a Comment