Friday, December 2, 2011

Wafugaji watishia mgomo kuuza mifugo nchi ikose nyama

Muswada Katiba mpya
 
Paul Sarwatt
Arusha
Jamii ya wafugaji Tanzania

WAKATI Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, akitarajiwa kutia saini au la Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuashiria mwanzo wa mchakato wa kuandika Katiba mpya, baadhi ya wadau wameendelea kupinga Bunge kupitisha muswada huo.
Miongoni mwa wadau wa hivi karibuni kupinga muswada huo ni pamoja na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali, likiwamo Shirika la PINGOs Forum, ambalo wiki iliyopita iliandaa mdahalo wa siku mbili uliobeba maudhui ya miaka  50 ya Uhuru na changamoto ya mabadiliko ya Katiba kwa jamii za wafugaji, warina asali, waokota matunda na wakulima.
Shirika hilo lenye makao yake mjini Arusha lilifanya mdahalo huo kwa kushirikiana na shirika jingine la ALAPA (Association for, and Advocacy for Pastoralist) na uliwahusisha wadau kutoka jamii za wafugaji, wakusanya matunda, warina asali na wakulima.
Katika mdahalo huo wadau hao walipata fursa ya kuzungumzia masuala mbalimbali kuhusu haki watu wa jamii ya wafugaji, warina asali, wawindaji na wakusanya matunda pamoja na wakulima katika Katiba ya sasa na pia katika Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Moja wa wadau hao ni Kijolu Kakiya, mkazi wa kijiji cha Piayaya wilayani Ngorongoro ambaye alieleza kuwa Katiba  inayotumika sasa imewatenga watu wa jamii ya wafugaji hasa katika masuala ya umiliki wa ardhi kutokana na tabia ya Serikali kumega ardhi ya wafugaji kwa matumizi mengine.
Matumizi hayo yametajwa kuwa ni pamoja na uwekezaji bila ya kuwashirikisha au kuwapatia wafugaji hao ardhi mbadala.
“Kila mmoja wetu hapa ni shahidi wa matendo ya uporaji ardhi uliofanywa na Serikali katika maeneo mbalimbali ya wafugaji nchini mwetu, tumefukuzwa kama wahamiaji kutoka nchi nyingine bila ya kupewa hata nafasi ya kusikilizwa na hali hii haikubaliki,” alisema.
“Mimi nina watoto saba na wote hao wananitegemea kuwasomesha na mahitaji mengine ya kimaisha sasa nakosa nguvu za kiuchumi kuwasomesha kwa sababu  mifugo ambayo ndiyo njia kuu ya kujipatia kipato, imekufa kutokana na ukame uliotokea mwaka juzi  hivyo sina namna nyingine. Ni kama nimegeuka kuwa omba omba,” alieleza kwa masikitiko.
Mama huyo alieleza kuwa wakati wa ukame ukishika kasi katika Wilaya ya Ngorongoro, Serikali iliwazuia kuingiza mifugo yao katika eneo la pori tengefu la Loliondo ambalo liko chini ya kampuni ya Orttello Business Cooperation (OBC), inayofanya shughuli za uwindaji wa kitalii katika pori hilo na viongozi wa Serikali walijenga hoja kuwa wafugaji wangemsumbua mwekezaji.
“Matokeo ya uamuzi huo wa Serikali ni kufa kwa maelfu ya mifugo kutokana na ukosefu wa malisho, Serikali imesahau kuwa pori hilo tengefu ni eneo la wafugaji wa kimasai ambao wameishi hapo kwa miaka mingi,” alisema.
Alipendekeza kuwa iwapo  Rais Kikwete ataendelea na mipango yake ya kusaini muswada wa sasa kuhusu mchakato wa Katiba mpya na kupuuza maoni ya baadhi ya wananchi, jamii ya wafugaji inaweza kususia kuuza aina zote za mifugo kwa mwezi mzima kama njia ya kutaka kuishinikiza serikali iwasikilize.
“Tutafanya kampeni  nchi nzima kususuia uuzaji wa mifugo ya aina zote kama njia ya kufikisha ujumbe kwa Rais na Serikali yake kuwa hatujafurahishwa na hatua yake na tuone kama Serikali ina uwezo wa kuagiza nyama kutoka nje kuwalishwa watu wake,” alisema.
Kwa upande wake, mfugaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kooya Timman, mkazi wa Kijiji cha Ololosokwan, wilayani Ngorongoro anasema; “Wafugaji wana tofauti kidogo na watu wa jamii nyingine kwa hiyo, waangalie Katiba ya zamani na watathmini masuala ambayo hayakuainishwa katika Katiba hiyo. Haki za msingi za kijamii kama elimu, afya na maji ziangaliwe katika Katiba hiyo mpya.”
Mkazi wa Kijiji cha Endulen, wilayani Ngorongoro, Noolosho Nakuta, naye aliunaga na wenzake akieleza kushangazwa kwake na kitendo cha Serikali kutotambua uwepo wao ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Analalamika kuwa Serikali kupitia mamlaka hiyo wamewanyima hata maeneo ya kwa ajili ya uanzishaji miradi ya kijamii, kama zahanati na shule.
Anasema; “Wakati wananchi wanabanwa katika hilo, wawekezaji wanapewa vibali vya kujenga majengo makubwa kama hoteli za kitalii ambayo yamekuwa chanzo uharibifu wa mazingira na mfumo wa asili wa maisha ya viumbe na wanyama katika  kreta ya Ngorongoro.”
Awali, akizungumza  katika   mdahalo huo  Rais wa  Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fransis Stolla,   alisema watachukua hatua za kisheria kwa kuifikisha Serikali mahakamani kupinga Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, iwapo Rais Kikwete atausaini tayari kuanaza kutumika kama sheria rasmi.
“Tunamwomba Raia Kikwete atumie hekima yake  kwa kuurejesha upya muswada huo bungeni ili usomwe kwa mara ya kwanza na wananchi wapewe fursa pana zaidi ya kuujadili kwa kina,” alisema Stolla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa asasi binafsi ya Jukwaa la Taifa la Katiba, Deus Kimbamba, alisema hawakubaliani na muswada huo wa mabadiliko ya Katiba mpya kwa kuwa umejaa upungufu mwingi kuliko hata Katiba ya sasa.
“Tunapoulalamikia muswada huo si kwamba tunataka kujifurahisha, tunaupinga kwa sababu hata jina lenyewe limekosewa na vipengele vingi havijazingatia mahitaji ya kweli ya Katiba mpya kwa jamii ya Watanzania,” alisema
Alitaja miongoni mwa kasoro hizo kuwa ni pamoja na muswada kuwa na kipengele kinachowanyima haki watu wasio wajumbe wa tume ya Katiba kuaandaa mikutano au majumuiko kwa lengo la kujadili, kutoa au kukusanya maoni au mapendekezo yao kuhusu Katiba mpya.
Alisema kifungu hicho kinaweka wazi kwamba anayepatikana na kosa la kuzuia tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya kufanya kazi yake atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au faini isiyozidi milioni 15 au vyote kwa pamoja.
“Hii maana yake ni kwamba kunzia tarehe moja Desemba mwaka huu  kama Rais atakuwa amesaini muswada huo basi tunaojadili masuala ya Katiba mpya hapa tumevunja sheria na tunapswa kufikishwa mahakamani na kwa tafsiri nyingine ni kwamba, magereza yetu ambayo tayari yamesheheni watuhumiwa na wafungwa yatafurika zaidi,” alisema Kibamba.
Mwenyekiti wa mkutano huo, Elfuraha Laltaika, ambaye  pia ni Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Tumani, tawi la Makumira, alisema malengo na maudhui ya mdahalo huo ni kufanya tathmini na marejeo kuhusu haki ya ardhi kwa jamii za wafugaji na wakusanya matunda, katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru na pia nafasi yao katika Katiba mpya itakayotungwa sasa.

No comments:

Post a Comment