Tuesday, December 20, 2011

Ikulu kuwafutia posho wabunge

Mwandishi Wetu
Rais Jakaya Kikwete, Spika Anna Makinda
Rais Jakaya Kikwete, Spika Anna Makinda
 
Matanuzi yao sasa kutegemea mshahara
Upembuzi wa athari wafanyika
Siku nne tu za ‘wikiendi’ walilipwa milioni 129/-
SAKATA la nyongeza ya posho kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeingia katika sura mpya, na sasa uchunguzi wa Raia Mwema, umebaini kuwa si tu Rais Jakaya Kikwete hatasaini nyongeza hiyo mpya kama tulivyoripoti wiki iliyopita, bali posho hizo za ‘kukaa kitako’ (sitting allowance) zitatangazwa  kufutwa rasmi wakati wowote.
Vyanzo vya habari vya gazeti hili ndani ya Ikulu vimethibitisha ya kuwa Rais Kikwete amepewa ushauri wa kufuta posho hizo kutoka kwa baadhi ya watalaamu wake na uamuzi unaweza kufanyika na kutangazwa wakati wowote.
Inaelezwa kuwa upembuzi wa kina wa athari za kufuta posho hizo kwa wabunge na hasa kujua kama zitaathiri majukumu yao umekwishakufanyika na kukamilika na taarifa zinasema kati ya waliowasilisha takwimu za ‘kihasibu’ Ikulu, ni pamoja na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila.
“Suala lililopo mezani kwa Rais si kusaini au kutosaini waraka wa mapendekezo ya nyongeza ya posho, bali ni kufuta sitting allowance zote kwa wabunge. Huo ndio ushauri wa kitaalamu unaohusisha hesabu za wahasibu na ambao, Rais ameukubali na unatarajiwa kutangazwa karibuni.
“Kama akitangaza kufuta posho hizi maana yake, masuala mengine ya wabunge yanaweza kufanyiwa marekebisho katika mshahara, ambayo nchi itanufaika kwa kukata kodi pia, unajua walikuwa hawakatwi kodi kwenye posho.
“Wabunge hawastahili malipo ya sitting allowance, kwa sababu wanakuwa wanatekeleza wajibu wao na stahili yao ni kulipwa mishahara tu,” alisema mtoa habari wetu.
Lakini wakati hayo ya Ikulu yakiwa hivyo, uchunguzi wa Raia Mwema umebaini ya kuwa wakati wa jaribio la kutaka nyongeza ya posho mpya, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alizungumza tu na Rais Jakaya Kikwete akiamini kuwa angeridhia wito wa wabunge na hivyo, mchakato wa malipo ya posho mpya ukianza si tatizo.
Mbali na Spika kuzungumza tu na Rais Kikwete bila kufikia muafaka, inaelezwa kuwa akishirikiana na Tume ya Bunge, walimshinikiza Katibu, Dk. Kashilila, kulipa posho mpya, naye akagoma.
Taarifa zaidi zinasema hata Spika Makinda mwenyewe aliwekwa katika shinikizo kubwa la wabunge wakitaka posho mpya na kama angeshindwa, walimtisha kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye na hivyo, kumng’oa madarakani.
Taarifa za uchunguzi zilizotufikia zinaeleza kuwa wabunge karibu wote waliunga mkono posho mpya na kupitia Tume ya Bunge, azimio la nyongeza likapitishwa kutoka Sh 70,000 hadi 200,000.
Kutokana na azimio hilo kupitishwa, wajumbe wa Tume hiyo kwa kushirikiana na Spika, walimtaka Katibu Dk. Kashilila kuanza kuwalipa katika mkutano uliopita wa Bunge.
Lakini, kwa mujibu wa taarifa hizo, akikariri mchakato unaofutwa katika malipo ya aina hiyo ambayo yanahitaji mamlaka husika iridhie, na katika suala hili mamlaka hao ni Rais Kikwete ambaye alikuwa hajaridhia, Dk. Kashilila aligoma kuwalipa akisema bado mamlaka husika (Rais) hajaidhinisha kwa vile hakuna instrument  ama waraka idhinishi kwa ajili hiyo ambao lazima usainiwe na Rais kabla ya kwenda Hazina kuomba fungu.
“Katibu alishinikizwa sana, alipowaeleza hana instrument Spika akamwambia yeye ameongea na Rais na amekubali, lakini Katibu anajua kukubali kwa Rais si kwa maneno bali ni kutia saini waraka.
“Kwa hiyo, naye Katibu akamwambia Spika, kama Rais amekubali naomba niandikie rasmi kwa maandishi ili nifanye malipo...hapo Spika hakuandika.
“Lakini pamoja na Spika kutoandika, alisisitiza kwamba amekwishakuzungumza na Rais, na pia Tume ya Bunge iliweka shinikizo kali dhidi ya Katibu alipe posho mpya.
“Alichofanya Katibu hakulipa posho isipokuwa amelipa malipo ya wabunge kwa siku walizofanya kazi mwishoni mwa wiki, kuanzia kwenye kamati na vikao vya Bunge, si wabunge wote waliopata malipo hayo,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.
Raia Mwema ilizungumza na Katibu wa Bunge, Dk. Kashilila kujua kama alishinikizwa lakini katika majibu yake akasisitiza akisema; “Sikulipa mbunge yeyote posho mpya, mimi ndiye mlipaji...nasema sijalipa.
“Nilicholipa ni malipo wanayostahili waheshimiwa wabunge waliofanya kazi siku za mwisho wa wiki, wengine kwenye vikao vya kamati na wengine vikao vya Bunge Dodoma.
“Tunaandaa taarifa za mchanganuo na kuwatumia wahusika wote, halafu mkawaulize nilichowalipa ni ongezeko la posho au nini?” alisema Dk. Kashilila.
Hata hivyo, gazeti hili limebaini kuwa malipo yanayotajwa kufanyika kwa wabunge kama anavyoeleza Katibu wa Bunge, yamefanywa kwa wabunge 307, kila mmoja akilipwa Sh. 420,000 zinazohusisha siku nne za mwisho wa wiki walizofanya kazi, wakati wa mkutano wa Bunge uliopita na baadhi ya vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, kabla ya kuanza kwa mkutano huo uliofanyika Novemba, mwaka huu.
Taarifa zinaonyesha kuwa jumla ya Sh. 128,940,000 (takriban milioni 129) ndizo zilizolipwa kama fungu la ziada ambalo limesababisha wabunge kuhisi ongezeko kwenye akaunti zao.
Takwimu hizo zinapingana moja kwa moja na kauli ya Spika kuwa wabunge walilipwa posho mpya tangu mkutano uliopita.
Utata kuhusu kauli ya Spika
Uchunguzi zaidi wa gazeti hili umebaini kuwa kauli ya Spika kuwa posho zimelipwa haina ukweli isipokuwa kilichofanyika kwa wakati huo ni agizo alilotoa (Spika) kutaka hesabu za malipo ya posho mpya ziandaliwe na kama Rais angesaini, basi walipwe kwa kuongezea juu ya  posho za Sh 70,000 kwa siku walizolipwa mkutano uliopita wa Bunge.
“Spika kule bungeni aliagiza hesabu za malipo ya posho kwa viwango vipya zifanyike. Kwa hiyo, wabunge wangelipwa hizo Sh.70,000 lakini baada ya Rais kusaini, wangeongezewa (kufidiwa) ili ifikie Sh 200,000. ndiyo maana alisema wabunge wameanza kulipwa mkutano uliopita, kilichopo ni kwamba waliamini Rais angesaini tu kiurahisi,” anasema mtoa habari wetu.
Juhudi za gazeti hili kumpata Spika kuzungumzia suala hilo zimegonga mwamba kwa siku kadhaa sasa, ikiwa ni pamoja na kumpigia kwa simu yake ya mkononi iliyokuwa ikiita bila majibu.
Njama kumng’oa Katibu zasukwa
Kutokana na suala hili kuonekana kuibua mvutano wa kiutawala ndani ya Bunge, sasa kuna taarifa kwamba mkakati maalumu umeanza kusukwa ili kumng’oa Dk. Kashilila.
Mpango huo ambao Raia Mwema imeunasa, unatajwa kuhusisha baadhi ya viongozi wa Bunge, wakiwamo baadhi ya wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge.
Wenyeviti hao (majina yanahifadhiwa) wanadaiwa kuchukizwa na uamuzi wa Katibu wa Bunge, wakiamini ni kati ya wasiotaka wabunge kuongezewa posho na kwa hiyo, wanadhani ni kikwazo kwa mafanikio ya Spika Makinda.
Raia Mwema imetajiwa baadhi ya wenyeviti hao akiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mahesabu ya Serikali Kuu, Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Momose Cheyo ambaye alikataa kuzungumzia jambo hilo alipoombwa aeleze maoni yake wiki hii na mwandishi wetu.
Cheyo, ama maarufu kama Bwana Mapesa, alisema ya kuwa kama ana mawazo yake kuhusu posho anajua sehemu sahihi pa kuyawasilisha.
Kikwete awajibu kupitia CCM
Wachambuzi wa mambo wanasema ya kuwa taarifa ya Rais Kikwete ya kuukataa mpango huo wa posho kwa wabunge imejieleza wazi katika hatua ya wiki hii ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutangaza kwamba hakiafiki posho hizo ziendelee kulipwa na kwamba ni busara suala hili liachwe kwa sasa.
CCM kupitia kwa Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, mwishoni mwa wiki iliyopita ilitoa tamko ikisema: “Tunaamini busara itatumika kuachana na jambo hili, kwani kuendelea  nalo kunaweza kutafsiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine, wakiwamo askari, walimu na madaktari.
“Kwa kuongeza kiwango hicho cha posho kwa wabunge ni kuongeza pengo la tofauti ya kipato kati ya wenye nacho na wasionacho katika jamii yetu hasa kwa kuegemea baadhi ya makundi.
“Swali kubwa hapa linakuwa je, maisha yanapanda Dodoma peke yake na kwa wabunge tu? Kuongoza ni kuonyesha njia hivyo si sahihi kwa wabunge kuonyesha njia kwa kujiongezea posho peke yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha.”
Kauli ya Zitto Kabwe
Miongoni mwa wabunge, Ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, pekee mwenye msimamo wa wazi kupinga si tu ongezeko la posho za sasa, bali hata posho nyingine zinazolipwa kwa wabunge kwa kutimiza majukumu yao ya kawaida, ambayo kipato halali kwa mujibu wa tasiri ya Kabwe ni mshahara.
Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu tafsiri yake kutokana na tofauti ya msimamo na kauli kati ya Spika Makinda na Katibu wa Bunge, Dk. Kashilila, Zitto alisema Spika amewekwa katika shinikizo na wabunge.
Speaker is under pressure (anashinikizwa), wabunge wamemtisha ili ahakikishe kunakuwapo posho mpya na asipofanya hivyo kuna vitisho kwamba anaweza kupigiwa vote of no confidence (kura ya kutokuwa na imani), ushauri wangu hapa ni kwamba Spika anatakiwa awe bold enough (imara), akatae shinikizo na aseme hakuna posho mpya.
“Najua amewekwa kwenye pressure na Tume ya Bunge na wabunge wengine, lakini kama kibali cha Rais hakuna aseme, awe jasiri,” alisema Zitto.
Waziri Mkuu achukizwa
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kati ya viongozi walioshitushwa na kauli ya Spika Makinda kuhusu ongezeko la posho kwa kuzingatia ugumu wa maisha Dodoma, ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Pinda ananukuliwa akisema; “Hili suala bado lilikuwa katika mchakato ambao uamuzi wa mwisho hautokani na Bunge, sasa kwa nini amekwenda (Spika) kueleza kabla ya kujua majibu ya mwisho?
Kuhoji huko kwa Pinda kumetafsiriwa na baadhi ya viongozi kuwa, Spika alichofanya ni kucheza mchezo wa kisiasa kwa kujivua pressure iliyokuwa ikielekezwa kwake na wabunge na kutua mzigo huo kwa Ikulu, na hususan Rais Kikwete, ambaye naye sasa amecheza ‘siasa’ kwa kutumia CCM.
Inaelezwa kuwa Spika Makinda amekuwa akishinikizwa na baadhi ya wabunge ambao wanamzongazonga wakihoji kwa nyakati tofauti; “Mbona Sitta (Samuel,  Spika aliyepita)  aliweza, wewe unashindwa nini?”

No comments:

Post a Comment