Tuesday, December 20, 2011

Mgogoro waikumba Manispaa ya Arusha

Paul Sarwatt
Arusha
Mji wa Arusha
Mji wa Arusha
 
Ni kuhusu zabuni ya ushuru wa maegesho ya magari
MANISPAA ya Arusha imeingia katika kashfa ya kutoa zabuni ya kukusanya ushuru wa maegesho ya magari katika  mji wa Arusha kwa Kampuni ya Barack Printers Ltd, bila  kampuni hiyo kutia saini mkataba wa kukusanya ushuru  kinyume cha sheria za Jiji.
Taarifa zilizopatikana mwishoni mwa wiki na kuthibitishwa na vyanzo kadhaa zinaeleza kuwa kampuni hiyo ilipewa zabuni ya kukusanya mapato ya ushuru wa maegesho ya magari kuanzia Desemba mosi, mwaka huu, lakini makataba wake haukuwa umesainiwa na pande zote zinazohusika.
Kwa mujibu wa  sheria zinazotawala Serikali za Mitaa, zabuni yoyote ya kukusanya ushuru kati ya halmashauri, manispaa au jiji na kampuni au wakala aliyeshinda zabuni, ni lazima mkataba  wake usainiwe na pande zote kabla ya kampuni husika kuanza kazi.
Kampuni husika pia inatakiwa kupitia mchakato wa kujadiliwa na Bodi ya Zabuni na baada ya machakato kukamilika, jina la kampuni iliyoteuliwa na bodi huwasilishwa katika Kamati ya Fedha na Uchumi ya Baraza la Madiwani,  ambako hujadili na baada ya kuridhia, meya au mwenyekiti wa halmashauri husika hutia saini  mkataba kwa niaba ya halmashauri yake.
Hata hivyo, pamoja na sheria hiyo kuwa wazi,  Halmashauri ya Jiji la Arusha imekiuka sheria hiyo na badala yake, imetoa zabuni kwa kampuni hiyo ya Barack Printers  Ltd kukusanya ushuru wa maegesho ya magari wakati haina makataba wa kutekeleza kazi hiyo.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya Manispaa zinaeleza kuwa, suala hilo liliwasilishwa katika kikao cha Kamati ya Fedha na Uchumi ya Baraza la Madiwani, ambayo Mwenyekiti wake ni Meya wa Jiji, Gaudance Lyimo, na kamati hiyo iliyakataa maelezo yaliwasilishwa na Mkurugenzi wa  Jiji, Estomih Chang’a kwamba hayakujitosheleza.
“Katika kikao hicho, Chang’a (Mkurugenzi wa Jiji) akiwa na timu yake ya wataalamu aliwasilisha mbele ya kamati taarifa za Kampuni ya Barack Printers kupewa zabuni ya  kukusanya ushuru wa halmashauri, lakini wajumbe wote walikataa na kuhoji mambo kadhaa,” anaeleza mtoa taarifa wetu.
Miongoni  mwa hoja za wajumbe wa kamati hiyo zilizoelekezwa kwa mkurugenzi ni pamoja wajumbe kutaka kufahamu kampuni hiyo ilishinda lini zabuni hiyo kwa vigezo gani vilivyotumika hadi kuipa wa zabuni husika.
“Mkurugenzi na watalaamu wake hawakuwa na maelezo ya kina baada ya kuhojiwa na wajumbe hao na ndipo kamati ilipopitisha azimio kumtaka meya asitie saini mkataba huo,” alieleza mtoa habari wetu.
Utata mwingine ulioibuka kuhusu kampuni hiyo ni umiliki wake, ikidaiwa kuwa inamilikiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Moshi Vijijini, Morris Makoi, ambaye ni diwani katika halmashauri hiyo na kwa mujibu wa sheria za zabuni katika Serikali za Mitaa, diwani, mtumishi au kiongozi wa Serikali haruhusiwi kuwa mzabuni katika halmashauri yoyote.
“Kwa ujumla suala hili la ukusanyaji wa ushuru wa maegesho ya magari limezingirwa na wingu zito na hata masuala ya ufisadi na rushwa yanadaiwa kutumika kabla na baada ya kukamilika kwa mchakato wake,” kilieza chanzo chetu cha habari.
Kamati pia ilimtaka mkurugenzi huyo kutoa maelezo kuhusu vigezo vilivyotumika kuipa zabuni kampuni hiyo, inayodaiwa hata hivyo kuingia kwenye ushindani wa zabuni kwa kiwango cha chini cha fedha, ikilinganishwa na kampuni nyingine mbili zilizoshiriki na kuweka kiwango cha juu zaidi.
Kampuni nne zinaelezwa kuomba zabuni hiyo  na fedha viwango vya fedha walivyotumia wakati wa ushindani wa zabuni kwenye mabano ni pamoja na Ecco Consultant (Sh milioni 48).
Kampuni nyingine ni Consard Ltd (Sh. milioni 46), Makumira Filling Station (Sh. milioni 42) na Barack Printers (Sh. milioni 42), ambayo ndiyo imepewa ushindi unaotiliwa shaka.
Kabla ya kampuni hiyo kupewa zabuni kazi ya kukusanya mapato ilifanywa na Kampuni ya Jamahedo, iliyomaliza mkataba wake Novemba 30, mwaka huu, na mkataba huo ulikoma baada ya uongozi wa manispaa kukubaliana na kampuni hiyo kusitisha mkataba kutokana na mgogoro uliozikumba pande zote mbili.
Mgogoro huo uliodumu kwa miaka miwili na kuathiri kwa ujumla shughuli za ukusanyaji mapato, ulianza baada ya uongozi wa manispaa kuzuia Kampuni ya Jamahedo isikusanye ushuru katika maeneo tisa, kinyume cha mkataba uliosainiwa awali.
Kutokana na hatua hiyo ya manispaa, kampuni ya Jamahedo ilifungua shauri Mahakama Kuu katika kesi iliyokuwa chini ya Jaji Sambo, lakini baada ya mvutano wa muda mrefu walikubaliana kumaliza suala hilo nje ya mahakama na Jamahedo kupewa miezi minne kukusanya ushuru bila kupeleka fedha zozote manispaa ili kufidia hasara waliyopata na mkataba huo ulimalizika Novemba 30.
Habari zaidi zinaeleza kuwa Bodi ya Zabuni ilitangaza kampuni zilizoshinda zabuni mbalimbali za kukusanya ushuru katika Jiji la Arusha mapema Juni, mwaka huu, ambapo kwa upande wa ushuru wa magari, kampuni nne ziliomba kazi hiyo.
Hata hivyo, hakuna kampuni iliyopewa zabuni kutokana na mgogoro uliokuwepo mahakamani wakati huo, baina Jamahedo na manispaa hivyo, Jamahedo waliendelea kukusanya ushuru huo wa maegesho hadi walipomaliza mkataba wao Novemba 30.
“Wakati muda wa mkataba wa Jamahedo ukifikia tamati, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, aliushauri uongozi wa manispaa kujipa muda wa kutafakari kabla ya kuingia mkataba na kampuni nyingine na pia kupitia kwa kina makataba husika, ili kuondoa matatizo yaliyotokea awali” alisema moja wa maofisa wa jiji (jina linahifadhiwa) aliyezungumza na gazeti hili.
“Mkurugenzi na wataalamu wake wala hawakujipa muda wa kutafakari kama walishauriwa na Mkuu wa Mkoa. Badala yake,  walimpuuza RC na kuidhinisha Barack Printers Ltd, waanze kazi bila hata mkataba kupitiwa na Kamati ya Fedha na Uchumi, matokeo yake wananchi wa Arusha wanalipa ushuru wa maegesho kwa mkataba batili, kinyume cha sheria” alieleza ofisa huyo.
Meya wa Jiji la Arusha, Gaudance Lyimo alithibitishia Raia Mwema kuwa, mkataba huo haujasainiwa na kamati yake ilikuwa bado haijapata maelezo ya kutosha kuhusu kampuni iliyopewa zabuni na halmashauri.
“Ni kweli bado hatujasaini mkataba kutokana na sababu kadhaa kuhusu kampuni husika na tumeomba maelezo ya kina kutoka kwa mkurugenzi na watu wake na tunatarajia watafanya hivyo haraka iwezekanavyo,” alieleza Lyimo.
Meya Lyimo alisema kuwa kwa muda mrefu mikataba ya kukusanya mapato ya halmashauri imekuwa na migogoro na kwamba, mawakala waliifungulia mashtaka halmashauri kutokana na udhaifu wa watendaji wake wanaodaiwa kushiriki katika hujuma na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mapato.
“Kutokana na uzoefu wa mikataba tulioupata na kesi mbalimbali tulizofunguliwa ni lazima tuwe makini na suala hili ili tutakapokubaliana basi kusiwe na dosari ambazo zinaweza kuingiza halmashauri yetu katika hasara ya kulipa fidia na gharama zisizo za lazima,” alisema Lyimo.
Kwa mujibu wa meya huyo, suala hilo sasa litajadiliwa katika kikao cha Baraza la Madiwani kinachotarajiwa kukutana Desemba 16, mwaka huu, katika ukumbi wa mikutano wa Jiji. Katika kikao hicho,  madiwani watapata fursa ya kujadili kwa kina utata kuhusu kampuni hiyo.
Akizungumzia utata huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Estomih Chang’a, alikanusha taarifa hizo.
“Si kweli kuwa hakuna mkataba ila tumewapa barua kuwa wameteuliwa kufanya kazi ya ukusanyaji wa ushuru na barua hiyo ina halalisha wao kufanya kazi wakati tunaandaa mikataba  ya kisheria unayoizungumzia,” alisema Chang’a.
“Nawashangaa sana nyie mnaofutilia suala dogo kama hili, kuna kitu gani kipya hapa? Halmashauri imeingia mkataba na kampuni hiyo kihalali baada ya kupitishwa na Bodi ya Zabuni, kwa hiyo, hakuna tatizo,” alisema mkurugenzi huyo ambaye amekuwa akitajwa kuwa ni mtendaji dhaifu wa kazi.
Akijibu tuhuma dhidi ya kampuni hiyo inayotajwa kuwa ni mali yake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, Morris Makoi, alisema ni kweli wanatekeleza kazi ya kukusanya ushuru huo baada ya kampuni yake ya Mkomilo Trading, kuingia mkataba wa kibiashara na Barack Printers Ltd, kuwasaidia kazi hiyo kwa kuwa hawana uzoefu.
“Hawa Barack Printers wametu-sub contract sisi Kampuni ya Mkomilo Trading, ili tukusanye ushuru kwa niaba yao kwa sababu hawana uzoefu, lakini kazi hii wamepwa kihalali baada ya kushinda zabuni iliyotangazwa,” alieleza Makoi.
Hata hivyo, sheria za halmashauri pia zinazuia kampuni iliyopewa zabuni kuingia makataba na kampuni nyingine kutekeleza kazi walizokubaliana na maelezo hayo ya Makoi yamezidi kuongeza utata kuhusu uhalali wa zabuni hiyo ya ushuru wa maegesho.
Makoi anasema; “Tayari tumelipa bondi ya shilingi milioni 46 kwa halmashauri na tumekubaliana kuwasilisha Sh milioni 42.5, kila mwezi na makataba wetu unaisha Juni 30, mwaka 2012 na wanaolalamika ni washindani wetu wa kibiashara ambao wamekosa zabuni hii”.
Halmashauri ya Jiji la Arusha ni kati ya halmashauri zinazolalamikiwa nchini kutokana na kushamiri wa vitendo vya ufisadi. Hivi karibuni, Serikali iliwahamisha watumishi 19 wakiwamo wakuu wa idara sita, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kushamiri kwa vitendo vya ufujaji wa fedha za miradi.
Halmashauri hiyo imekuwa ikipata hati chafu kwa miaka zaidi ya mitano mfululizo baada ya hesabu zake kukaguliwa na mabilioni ya fedha yaliyotengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali, zinadaiwa kupotea kutokana na usimamizi duni kutoka kwa watendaji.

No comments:

Post a Comment