Tuesday, December 27, 2011

Ufa wazidi kuongezeka CUF

Na Alfred Lucas


UFA ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), umezidi kuongezeka. Wakati idara ya usalama ya chama hicho ikisema Hamad Rashid Mohammed, anatumiwa na Edward Lowassa katika mbio zake za kutafuta uongozi, Maalim Seif Shariff Hamad, anasema yeye mwenyewe ndiye anayesaka urais.

Kuibuka kwa taarifa za Hamad kutumiwa na Lowassa, kumekuja wiki mbili baada ya gazeti hili kuripoti madai ya baadhi ya viongozi wandamizi wa CUF kuwa mwanasiasa huyo anatumiwa na waziri mkuu Mizengo Pinda kukivuruga chama hicho.

“Baada ya Lowassa kuona hali ya kisiasa ndani ya chama chake (Chama Cha Mapinduzi) ni mbaya kwake, akatengeneza mpango wa kumtumia Hamad kutaka kuja kugombea urais kwa CUF,” unaeleza waraka huo uliotoka idara ya usalama ya chama hicho 4 Desemba 2011, kwenda kwa Profesa Ibrahim Lipumba.

Waraka huo uliosainiwa na mkurugenzi wa usalama wa chama hicho aliyetajwa kwa jina la Khamis Khassani, pamoja na mambo mengine unasema, “Lowassa ameona dhahiri hawezi kupata nafasi ya kugombea urais CCM mwaka 2015, hivyo akaamua kutengeneza mkakati na Hamad ili aweze kugombea urais kupitia CUF, huku yeye Hamad akiwa mgombea mwenza wake.”

Anasema, “…kiini cha haya, ni kwamba Lowassa anajua hawezi kupata nafasi hiyo kupitia viongozi wa sasa wa CUF kwa kuwa wanamuunga mkono Rais Jakaya Kikwete.”

Haikuweza kufahamika mara moja hicho kinachoitwa, “viongozi wa sasa wa CUF wanamuunga mkono Rais Kikwete,” kimelenga nini.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, kauli hiyo inathibitisha madai ya wengi akiwamo Hamad Rashid, kwamba CUF kimelala kwenye mnyororo wa CCM na ndiyo maana kinaitwa na CCM B.

Akiandika katika hali ya kumtoa hofu mwenyekiti wake, mkurugenzi hiyo wa usalama wa CUF anasema, “Lowassa anaona ili aweze kupata nafasi hiyo lazima kuwe na viongozi ambao watakubaliana naye lakini pia kwa makubaliano ya Hamad Rashid kuwa mgombea wake mwenza mwaka 2015.”

Anasema Lowassa ndiye anayefadhiri mpango huo; Hamad Rashid hana hata senti moja inayotumika kwa kazi hiyo. Anasema kadri siku zinavyokwenda mbele ndivyo anavyojikuta hana pesa na hivyo ameanza utaratibu wa kutafuta mikopo kutoka maeneo mbalimbali ndani ya nchi.

MwanaHALISI limeshindwa kumpata Lowassa kujibu madai hayo ya CUF.

Bali Hamad Rashid ameliambia gazeti hili juzi wakati linakwenda mitamboni, Wanaonifahamu wanajua kuwa mimi si mtu wa kutumiwa. Wanajua sijatumiwa na siwezi kutumiwa.”

Alipoulizwa kama yeye si mtu wa kutumiwa kwa nini anabebeshwa madai hayo alisema, “Ndugu yangu, nakuambia akutukanaye hakuchagulii tusi.”

Kwa upande wake, Maalim Seif anasema, anachokiona yeye ni kuwa Hamad Rashid anapiga hesabu za kutaka kuteuliwa kuwania urais wa Zanzibar iwapo atapata nafasi ya kuwa katibu mkuu wa chama hicho.

Akiongea kwa tahadhari kwenye mahojiano yake ya ana kwa ana na gazeti hili jijini Dar es Salaam, juzi Jumatatu, ambayo yatachapishwa kwa ukamilifu kwenye toleo letu lijalo, Maalim alisema, “Kuna watu wamemdanganya Hamad kwamba mimi niko mbioni kurejea CCM.

Anasema, “Ni kweli, CUF na CCM zimeunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar, lakini huko si kuungana” na wala hakuna maana ya yeye kurejea ndani ya chama hicho.

Maalim anasema Hamad Rashid ana mkakati wake, ambao ni kuingia ikulu ya Zanzibar. Anasema, “Si vibaya kuwa na ambition (ndoto). Bali means (namna) ya kufikia ambition hizo ndiyo tatizo.”

“Hamad anawaza kama akikosa urais chama kitashika nafasi ya pili basi atakuwa makamu wa kwanza wa rais. Watu wanamfahamu Hamad, hawezi kufanikiwa,” anasema Maalim Seif.

Katibu mkuu huyo wa CUF anasema, Hamad Rashid ambaye ni mbunge wa Wawi, kisiwani Pemba hatafanikiwa kwa sababu ya kuingia vibaya kwenye harakati hizo.

Waraka wa idara ya usalama uliokwenda kwa Profesa Lipumba unasema, sakata linaloendelea ndani ya chama hicho lilianza rasmi kwenye uchaguzi wa Igunga ambapo karibu wajumbe wengi wa baraza kuu walikuwepo huko, walishawishiwa na Hamad “kufanya uasi” kwenye kikao cha BKT cha mwezi wa tano hawakumuunga mkono Hamadi.

Anasema hali hiyo ilisababisha kuwapo chuki kati ya wajumbe waliokuwa Igunga na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Tanzania Bara, Julius Mtatiro.

Anasema chuki hiyo iliongeza nguvu katika suala zima la Hamad ambaye hapo mwanzo alikuwa na wabunge wachache; siku za mwisho kuelekea upigaji kura kulifanyika vikao kadhaa vilivyowajumuisha baadhi ya wajumbe wa baraza kuu wakiwamo baadhi ya wabunge.

Anasema mara baada ya kurejea kutoka Igunga, wajumbe kadhaa wakiwemo Khassan Doyo, walijipanga kuhakikisha wanatengeneza hoja ambazo zingesababisha agenda zilizowasilishwa zikataliwe na hatimaye kuwa na agenda moja ya kutokuwa na imani na viongozi wakuu wa chama hicho kwa kisingizio cha kushindwa uongozi.

Anasema agenda hizo zingesababisha kuundwa kwa uongozi wa muda kuelekea mkutano mkuu.

Waliotarajiwa kuwa viongozi, ni mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwani aliyetajwa kuwa angekuwa mwenyekiti, mbunge wa Ole, Pemba, Rajab Mbarouk Mohammed, makamu wa mwenyekiti, Hamad Rashid katibu mkuu, Doyo naibu katibu mkuu Bara na Masoud kuwa naibu katibu mkuu Zanzibar,” anaeleza.

Awali akiandika kwa Maalim Seif, 10 Desemba 2011, saa 1:03 adhuhuri, Profesa Lipumba alisema, “…ubinafsi ni hatari sana. Anawapa watu kudhani ndani ya CUF kuna mgogoro…”

Ujumbe wa Profesa Lipumba ulilkuwa ukijibu ule wa Maalim Seif wa 9 Desemba 2011 ulioeleza juu ya Jubeir Shamte ambaye Hamad Rashid alimtumia ujumbe alioutuma kwa Profesa Lipumba kuhusiana na kushamiri kwa mgogoro ndani ya chama hicho.

Aidha, Profesa Lipumba alitaka kujua kutoka kwa Maalim Seif iwapo vyombo vya habari vimeripoti lolote juu ya barua hiyo.

“Ni kweli, gazeti la MwanaHALISI limeandika… Mwenyewe anawafanya wanachama wamuone ni msaliti,” anasema.

Anasema, Hamad Rashid amekutana na na Sheikh Issa Ponda na Sheikh Basaleh, na kwamba mazungumzo yao yamemfika yeye Maalim Seif.

Maalim akiandika kwa Profesa Lipumba anasema, “…jamaa yako (Hamad Rashid) amekutana na Sheikh Issa Ponda na amezua mambo mengi. Sasa anamtafuta Sk Basaleh (Sheikh Basalehe). Ponda anasema yeye anafahamu sana jamaa yako na ni muongo. Wameomba baadaye mimi nikutane nao ili kuwaleza ukweli. Nakwenda Lindi na Kilwa kuanzia kesho (10 Desemba 2011). Nikirudi inshallah nitawarafuta,” anasisitiza.

Maalim anasema, hii ndiyo hali, na kwamba Profesa Lipumba asiwe na wasiwasi inadhibitiwa.

Wiki mbili zilizopita, gazeti hili liliandika kwa ufasaha mvutano uliyopo kati ya Maalim Seif na Hamad Rashid. Mvutano huo ulifikia kuibuka kwa vurugu kubwa kwenye maeneo ya Manzese jijini Dar es Salaam, ambako Hamad Rashid alizuiwa kufungua matawi ya chama hicho kwa madai hakutoa taarifa makao makuu ya chama Buguruni.

Hamad Rashid amekuwa akikisitiza, CUF kinaendeshwa kama chama cha familia, na kwamba ukatibu mkuu ambao yeye anataka kuugombea umekuwa kama utume ndani ya chama hicho.

No comments:

Post a Comment