Wednesday, December 21, 2011

Milionea Afariki na Kumrithisha Paka Wake Utajiri

  
Bibi Maria Assunta, milionea wa nchini Italia amefariki dunia huku akiwa ameishamrithisha paka wake utajiri wa dola za Kimarekani dola milioni 15. (Zaidi ya Tsh. bilioni 20).

Paka huyo anayejulikana kwa jina la Tommasino amekuwa paka tajiri duniani akishika nafasi ya tatu kwa utajiri duniani.

Bibi Maria alifariki mwezi uliopita akiwa na umri wa miaka 94 akiwa hana ndugu yeyote anayefahamika.

Mirasi yake aliiandika miaka miwili iliyopita ambapo aliandika maelekezo kuwa mali zake zote ziende kwa paka wake Tommasino.

Chini ya sheria za Italia, mnyama haruhusiwi kurithi mali kwa sababu hiyo wanasheria wa bi Maria wameamua kuwa nesi wa bi Maria apewe majukumu ya kutumia mali hizo kumtunza paka Tommasino.

Ni wanyama wawili tu ndio waliorithi mali nyingi zaidi kuliko paka Tommasino.

Mnyama tajiri kuliko wote duniani ni mbwa anayejulikana kwa jina la Gunter ambaye alirithishwa dola milioni 138 na mmiliki wake tajiri wa Ujerumani bi Karlotta Liebenstien.

Naye bi Patricia O'Neill, mke wa bingwa wa zamani wa mashindano ya kuogelea nchini Australia, Frank O'Neill, aliamuachia urithi wa dola milioni 61, sokwe wake anayejulikana kwa jina la Kalu.

No comments:

Post a Comment