Friday, December 30, 2011

Vita urais yazidi kutikisa CCM


VIGOGO HAWAAMINIANI, KAMBI ZAPIGANA VIKUMBO KUJIIMARISHA

Mwandishi Wetu
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikihaha kutibu makovu yanayotokana na harakati za kuwania urais wa 2015, imethibitika kwamba vigogo wa chama hicho wakiwamo wale wa kundi la wanamtadao linalodaiwa kwamba lilimwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani mwaka 2005 hawaaminiani katika harakati za kugombea urais kupitia CCM.Uchunguzi wa Mwananchi wa kabla na baada ya vikao vya Nec vilivyomalizika hivi karibuni unaonyesha kwamba vigogo wa CCM kutoka kambi zote wamekuwa wakiendesha kampeni za chini kwa chini kwa ajili ya kujiimarisha na kisha kuweza kuteuliwa kugombea kupitia chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.

Taarifa ambazo Mwananchi imezipata zinaonyesha kwamba hata baadhi ya vigogo wanaosadikiwa kuwa kundi moja sasa hawaaminiani jambo ambalo linaashiria kuwa vita ya urais CCM itatawala kwenye uchaguzi mkuu wa chama hicho unaoanza mwakani katika ngazi zote nchini.

Wakati wa vikao vyake vya juu vilivyomalizika Novemba 24 mwaka huu mjini Dodoma, CCM kilipokea na kupitisha taarifa ya hali ya siasa ambayo kimsingi ilibainisha kuwa hali ya siasa ndani ya chama sio shwari kutokana baadhi ya viongozi kupigana vikumbo kuwania madaraka.

Katika taarifa hiyo, CCM kilisema chanzo kikubwa cha migawanyiko ndani ya chama hicho ni harakati za kugombea urais mwaka 2015.

Sasa ni mwenzi mmoja tangu kumalizika kwa vikao hivyo, minyukano yenye lengo la kuwania urais wa 2015 imeendelea ndani ya CCM pia ndani ya makundi yenye lengo la kuwaweka wagombea wao katika nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.

Hata hivyo, wimbi hilo la urais limeendelea kutikisa kambi ya wanamtandao ambayo taarifa za ndani zinasema huenda suala la urais likaibua mtafaruku mkubwa siku zijazo hivyo kutoa mwanya kwa kundi jingine kuibuka kidedea.

“Kuna hali ya kutoaminiana ndani ya CCM, kila kundi sasa liko mstari wa mbele kujijega ili kuweza kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutoa mgombea urais. Hata ndani ya kundi la mtandao ambalo ndilo lenye nguvu kwa sasa wakubwa hawaaminiani,” alisema mtoa habari mmoja kutoka kundi la mmoja wa kiongozi anayetajwa kutaka kuwania urais ndani ya CCM.

Wachunguzi wa mambo wanautazama mgogoro huo ndani ya kambi hiyo tishio kwamba unaidhoofisha dhidi ya kambi zilizopo na nyingine zinazotarajiwa kuibuka kadri siku zinavyokwenda kuelekea 2015.

Wanaotajwa kwa urais

Ndani ya CCM, kinyang’anyiro cha urais kinawahusisha wanasiasa vijana ambao umri wao ni kati ya miaka 40 na 50, wanasiasa wenye umri kati ya miaka 50 na 60 na kundi la wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 ambao wametumikia nchi tangu uhuru.

Wanasiasa vijana wanaotajwa ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye.

Katika kundi la umri wa kati wapo Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye,  Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha-Rose Migiro.

Kundi hilo pia linawajumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.

Katika kundi la wenye umri zaidi ya miaka 60 wanaotajwa ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Vikao vya CCM
Taarifa ya hali ya siasa iliyowasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vya CCM mwishoni mwa Novemba mwaka huu, inaweka bayana kwamba:
“Kumekuwapo na migogoro ya kiuongozi na migawanyiko, kutokuelewana, kutopendana na kuhasimiana baina ya viongozi wa CCM katika mikoa kadhaa na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa”.

Taarifa hiyo iliyowasilishwa na January Makamba ambaye ni Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje wa chama hicho, iliendelea kuweka wazi kuwa hali hiyo imesababisha kuhujumiana na kuchafuana na kutengeneza magenge ya wapambe kwa ajili hiyo.

“Matokeo yake ni kwamba umma umeanza kukiona chama chetu kuwa ni chama cha migogoro, na chama cha watu wanaogombea madaraka badala ya utumishi. Taswira hii ya migawanyiko na ugomvi, ikiwemo kutupiana maneno kwenye vyombo vya habari mara kwa mara, inawakwaza wanachama na wapenzi wa CCM na inapunguza imani ya wananchi kwa chama chetu,”inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ambayo Mwananchi limeiona.

Taarifa hiyo inasema chanzo kikubwa cha migawanyiko ndani ya CCM ni harakati za kugombea urais kwa mwaka 2015.

“Licha ya kwamba hadi sasa hakuna mwana-CCM aliyetangaza nia ya kugombea urais kwa mwaka 2015, wana-CCM wengi na Watanzania kwa ujumla wanaamini kwamba moja ya vyanzo vya migawanyiko ndani ya Chama ni kuibuka kwa makundi ya harakati za kugombea urais mwaka 2015,”ilisema taarifa hiyo na kuongeza:

“Inaaminika kwamba baadhi ya wana-CCM wenye nia ya kuomba nafasi hiyo, wameanza harakati za kutengeneza makundi ya kuwaunga mkono miongoni mwa viongozi na wanachama na katika jamii kwa ujumla. Vilevile, wana-CCM wengi wanaamini kwamba vitendo vya kuchafuana na kushutumiana na kutuhumiana baina ya viongozi wa CCM vinasababishwa na harakati hizi”.

January katika taarifa hiyo iliyopitishwa, pia alisema migogoro katika  baadhi ya Jumuiya za CCM, kama vile Umoja wa Vijana na baadhi ya mikoa inatafsiriwa kwamba inatokana na harakati za urais 2015.

“Umoja na mshikamano ndani ya Chama Cha Mapinduzi utaendelea kuhatarika iwapo wana-CCM wenyewe wataendelea kuaminishwa na kuamini kwamba ni lazima wachague upande katika watu wanaotajwa kugombea urais mwaka 2015,”alionya January katika taarifa yake.

Alisema pamoja na kwamba ni jambo la kawaida wana-CCM kuwa na maoni ya nani anafaa kuongoza taifa, lakini harakati za urais zimeanza mapema, kwani bado miaka minne kabla ya kipindi cha sasa kuisha.

Siasa za makundi ndani ya CCM pia zimekuwa tishio kwa uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kuanza mapema mwakani.

Viongozi wengi wa CCM na baadhi ya wanachama wanaamini kwamba uchaguzi huo kwa mtazamo wa kimakundi, ndio utatoa taswira ya mwelekeo wa uchaguzi wa 2015.

Hatua za CCM
Kutokana na hali hiyo, January alipendekeza CCM kidhibiti harakati za kisiasa zenye mwelekeo wa kuwagawa wana-CCM kimakundi katika Uchaguzi wa Chama na Jumuiya mwaka kesho na kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Harakati za kusaka urais kabla ya mchakato rasmi haujaanza, aidha kwa kujitangaza au kwa kuchafua na kuhujumu wana-CCM wengine, ziwekwe bayana na zichunguzwe kwa uwazi, na pale zinapothibitika zina ukweli, hatua kali zichukuliwe kwa vinara na wapambe wao,”anasema sehemu ya taarifa ya katibu huyo.

Kadhalika, alipendekeza utengenezwe utaratibu madhubuti wa kupata mgombea urais kwa tiketi ya CCM ambao hautategemea nguvu za kimakundi wala uwezo wa fedha, huku akitaka viongozi wa CCM na wa Serikali wanaoacha shughuli zao na kujihusisha na kuusaka urais au kunadi wagombea urais pia wadhibitiwe.

Taarifa hiyo ilikwenda mbali zaidi na kupendekeza kwamba CCM kijizatiti kuhakikisha uchaguzi wake wa mwaka ujao hauharibiwi kwa  kutumiwa kupanga safu za kusaidia watu au mtu kwenye uchaguzi wa udiwani, ubunge au urais mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment