Wednesday, December 28, 2011

Tume kuwakaanga vigogo wanaoficha mali

Geofrey Nyang’oro
TUME ya maadili ya viongozi wa umma, imeanza kuwashirikisha wananchi kwa lengo la kufichua viongozi wasio waadilifu ambao hutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu mali wanazomiliki.Kutokana na hali hiyo, tume hiyo imewatahadharisha viongozi wa umma kuepuka kutoa taarifa za uongo za mali na madeni yao na kwamba kufanya hivyo ni kosa kwa mjibu kifungu cha  15 (b) cha Sheria za maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.

Kamishina wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa wananchi wana haki ya kushirikiana na Sekretarieti ya maadili ya Viongozi wa umma kutoa taarifa juu ya uhalali wa mali wanazomiliki viongozi wao sababu  ndio wanaoishi nao.

“Kiongozi wa umma atahesabiwa kuwa ametenda kosa la kukiuka maadili endapo atatoa tamko huku akijua ni la  uongo au potofu katikia kipengele chochote muhimu na ikibainika atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma,” alisema Kaganda na kuongeza:

“Tumeamua kuwashirikisha wananchi katika hili sababu wao ndio wanaowachagua, wanaishi nao hivyo wanawafahamu zaidi na hili ni katika kutekeleza sera za kidemokrasia hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na tuhumu za ufisadi”.

Jaji Kaganda alifafanua kuwa viongozi watakaotoa taarifa za uongo  na watakaohindwa kutimiza matakwa ya sheria watashitakiwa katika baraza la maadili.

Alisema ikiwa itathibitika kiongozi kukutwa na hatia ya kutenda  kosa hilo pamoja na makosa mengine  anaweza kuchukuliwa hatua  za kufukuzwa kazi, kushauriwa kujiuzulu wadhifa unaohusu ukiukwaji huo, kusimamishwa kazi na kushushwa cheo.

Adhabu nyingine ni kupewa onyo kali, kuonywa na kupewa tahadhari, kupewa adhabu nyingine zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za nidhamu kwa kuzingatia wadhafa wa kiongozi na kuhimizwa kuchukuliwa hatua kwa kiongozi kwa mjibu wa sheria nyingine za nchi.

Tume hiyo imetaja Desemba 31 mwaka huu kuwa ni siku ya mwisho kwa viongozi kuwasilisha matamko ya mali na madeni wanayomiliki.

Chini ya utaratibu huo, viongozi wanatakiwa kuwasilisha kiwango halali cha mali wanazomiliki ndani na nje ya nchi pia madeni wanayodaiwa iwe Benki na maeneio mengine.

Jaji Kaganda alisema endapo hadi kufikia Desemba 31 mwaka huu viongozi hao watakuwa bado hawajatoa tamko la mali zao watakumbwa na mkondo wa sheria huku watakaorudiwa makosa wakikubwa na adhabu kali zaidi isiyo na msamahama.“Tunawasihi viongozi wa wa Umma kutoka katika Mamlala zote kuwasilisha mali wanazomiliki katika Tume ya maadili kabla ya Desemba 31 mwaka huu ili kuepuka hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao”alisema Kaganda.

Kaganda alifafanuwa kuwa viongozi zaidi ya 9000 wa serikali, Bunge na Mahakama ndio wanaohusika na sheria hiyo.Katika kikao cha kwanza kilichokaa kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu mashauri 41 yalifikisha mbele ya baraza la maadili ambapo viongozi viongozi 24 walipatwa na hatia.

Alisema kati yao sita walipewa onyo kali, 18 onyo la kawaida huku mmoja akipata faidia ya shauri lake kuwa na shaka.Katika hatua nyingine Jaji Kaganda ameeleza kuibuka kwa kundi la matapeli ambao wamekuwa wakijifanya kuwa maofisa wa tume hiyo.

Alisema matapeli hao wamekuwa wakiwapigia simu viongozi na kuwatisha kwamba majina yao yamo kwenye orodha ya kuhojiwa lengo likiwa kushinikiza wapewe fedha za hongo ili wasiwaadhibu viongozi hao.

Alisema matukio hayo yaliripotiwa siku chache baada Baraza la Maadili na  Sekretarieti ya maadili ya Viongozi wa umma, kukamilisha usikilizwaji wa mashauri mbalimbali dhidi ya viongozi.“Mara baada ya kumaliza kazi ya hiyo mwezi, Juni mwaka huu Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeletewa taarifa mara kadhaa na viongozi ambao wamedai kupigiwa simu na watu wanaojitambulisha kuwa ni watumishi wa tume ya maadili ya Viongozi wa Umma,”alisema Kaganda na kuongeza:

“Watu hao wamekuwa wakiwatisha viongozi kuwa majina yao yapo kwenye orodha ya viongozi wanaotarajia kufikishwa kwenye baraza la Maadili ya vuiongozi wa Umma na kuwataka kutoa fedha ili kwa lengo la kusaidiwa”alisema.

Alisema tume imesikitishwa ana taarifa hizo na kutoa tahadhari kwa viongozi wa umma pamoja na wananchi wote kuwa macho na matapeli hao na kwamba pindi wanapowabaini watoa taarifa Tume au Polisi ili hatua za ksheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.“Kimsingi sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kama chombo cha kikatiba chenye jukumu la kusimamia tabia na mienendo ya viongozi wa Umma nchini, hufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu”alisema Kaganda na kuongeza kuwa;

Chombo  kinautaratibu wake maalamu wa kuwasiliana na viongozi ambao kinataka kuwafikisha mbele ya baraza la maadili”.

No comments:

Post a Comment