Mabadiliko ya Katiba
MAKUBALIANO kati ya Serikali na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayosubiri idhini ya Rais Jakaya Kikwete, yamekiweka chama hicho njia panda kisiasa, Raia Mwema, imebaini.
Hakuna muda rasmi ulioafikiwa wa utekelezaji wa makubaliano hayo kati ya Serikali na CHADEMA kuhusu muswada huo, ambao tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekwishaupitisha na hivyo, kumaliza kazi yake kwa mujibu wa Katiba iliyopo sasa.
Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika akiwakilisha upande wa chama hicho walitiliana saini na Serikali ikiwakilishwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi. Katika makubaliano hayo, wameahidi kuendelea kuuboresha Muswada huo wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, ili kukidhi mahitaji ya kuaminiana na mwafaka wa kitaifa.
Makubaliano hayo pia yanataka kuwashirikisha wadau wengine katika kuboresha sheria hiyo, uamuzi ambao unatajwa kuunga mkono ule ushauri uliotolewa na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi, ambao hata hivyo ulitaka tu kushirikisha vyama vya siasa vyenye wabunge tu.
CHADEMA awali walipinga uamuzi wa kuwashirikisha katika mazungumzo ya pamoja kati yao na Rais na vyama vingine vyenye wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kwa sasa CHADEMA kipo njia panda kisiasa ingawa msimamo wake kuhusu mchakato wa Katiba kuwashirikisha wananchi wengi unaweza kubaki kama awali.
Harakati za kisiasa za CHADEMA mwenendo wake sasa unategemea zaidi utekelezaji wa makubaliano hayo ambayo pia yanategemea namna Ikulu itakavyoshughulikia.
“Inawezekana kabisa Rais anaweza kutia saini muswada huo ili uwe sheria lakini katika uamuzi huo anaweza kutekeleza matakwa ya makubaliano hayo wakati wa maandalizi ya kanuni ambazo hutungwa na Baraza la Mawaziri kwa kumshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Lakini katika makubaliano yale tumeona kinachopaswa kufanyiwa mabadiliko ni sheria na si muswada. Kwa hiyo kwa lugha nyingine, CHADEMA wamekubali Rais asaini muswada lakini mara utakapokuwa sheria basi ifikishwe bungeni kwa ajili ya mabadiliko,” alisema mmoja wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, hatua hiyo ya CHADEMA sasa imeanza kutofautiana na ile ya NCCR-Mageuzi ambao wabunge wake waliungana na wabunge wa CHADEMA kususia muswada huo, baadhi wakisusia hata mjadala na wengine wakishiriki mjadala lakini wakisusia upitishaji wake.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, tayari amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema; “Tulitoka nje ya Bunge ili kupinga muswada na si kutafuta njia ya kwenda kumwona Rais Ikulu. Hoja yetu ilikuwa wananchi hawajashirikishwa na bado hoja hiyo imebaki hivyo.”
Kafulila anaungwa mkono na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ambao kwa pamoja wanataka muswada huo urudishwe bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza.
Katika muswada huo, kati ya mambo yanayolalamikiwa ni pamoja na wananchi kutoshirikishwa kikamilifu katika kutoa maoni yao kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kaitba na Sheria, malalamiko ambayo hata hivyo, yamepingwa na uongozi wa Bunge, kupitia kwa Katibu wake, Dk. Thomas Kashilila.
Katika maelezo yake kwa vyombo vya habari ambayo pia yamechapishwa katika gazeti hili kurasa za 16 na 17, Dk. Kashilila anathibitisha kuwa muswada huo umefuata hatua zote, kinyume cha malalamiko yanayoelekezwa kwa Bunge kama taasisi.
Kikao kati ya Kikwete na CHADEMA kimeelezwa kuwa ni muendelezo wa mazungumzo ya chini kwa chini ya kidiplomasia yaliyokuwa yakifanywa na viongozi wastaafu na wanataaluma mbalimbali, ambao walionekana kutaka suluhu ya kisiasa kwa maslahi ya Taifa zaidi badala ya muelekeo wa awali uliokua umejikita kwenye siasa za vyama.
Mawaziri Wakuu Wastaafu, Dk. Salim Ahmed Salim na Joseph Warioba, ambao ni wana CCM, waliripotiwa kufanya juhudi binafsi za kufanya mazungumzo na wanasiasa wa CHADEMA kuhusiana na suala la mjadala wa katiba, mazungumzo ambayo hayajawahi kurasimishwa, kabla ya kikao rasmi cha Kikwete na CHADEMA.
Tayari kumekuwa na wasiwasi kutoka kwa baadhi ya wafuasi wa CCM na CHADEMA kuhusu mazungumzo kati ya Kikwete na CHADEMA, kila mmoja ukihofia hatima ya mazungumzo hayo itakua nini na kwa maslahi ya nani kisiasa, hofu ambayo imeyakumba pia makundi mengine ya kijamii, ambayo hayakushirikishwa.
No comments:
Post a Comment