Tuesday, December 27, 2011

Serikali hoi kifedha

Na Saed Kubenea


SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete iko taabani kifedha. Haina uwezo wa kuajiri watumishi wapya wala kupandisha vyeo wale waliopo, MwanaHALISI limegundua.

Sasa imeagiza ajira zote serikalini katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 zipunguzwe kwa asilimia 50. Vilevile upandishaji vyeo upunguzwe kwa kiwango kilekile.

Kwa hatua hii, serikali inabadilisha maamuzi ya bunge lililoidhinisha mapato na matumizi yake Juni mwaka huu.

Serikali imekiri kutokuwa na uwezo wa kutekeleza bajeti iliyopitishwa na bunge, kuwa na vipaumbele tofauti na mashaka na vyanzo vyake vya mapato.

“Baada ya serikali kutafakari uwezo wake kwa kuzingatia vipaumbele na vyanzo vya mapato, imeamuliwa bajeti iliyokuwa imependekezwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi wapya na upandishaji vyeo, ipunguzwe kwa takribani asilimia hamsini, umeeleza waraka wa ikulu.

Utekelezaji wa hatua hiyo ya serikali ulianza rasmi Novemba mwezi uliopita.

Waraka wa serikali umesainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma, Habu Mkwizu na kupelekwa kwa makatibu wakuu wote wa wizara, wakuu wa idara na taasisi zake nyingine.

Matokeo ya uamuzi huu, waraka unaeleza, “ni kwamba kila mwajiri sasa atalazimika kuandaa upya mahitaji yake ya ikama (taratibu za ajira na malipo) kwa kuzingatia ukomo uliorekebishwa wa bajeti uliotolewa na wizara ya fedha kwa mwaka 2011/12.”

Kila mwajiri amepelekewa jedwali la viwango vya ajira mpya, mishahara na nyongeza; na kutakiwa kufuata mkondo huo wakati wa kuwasilisha maombi mapya ya vibali vya ajira mpya kwa mwaka huuwa fedha.

Waraka unaagiza waajiri kuweka kipaumbele katika kutenga “nafasi za kutosha kwa ajili ya wataalam wa sekta za Elimu, Afya, Kilimo na Mifugo.”

Nakala ya waraka wa ikulu imepelekwa pia kwa Katibu Mkuu Kiongozi na Msajili wa Hazina.

Jedwali elekezi linaonyesha kila wizara, idara na asasi/taasisi ya serikali itapata shilingi kiasi gani kwa ajili ya nyongeza ya mshahara, idadi ya ajira kwa mwaka huu na ukomo wa kiwango cha kulipa mishahara yote yakiwa katika eneo la punguzo la asilimia 50.

Kwa mfano ikulu imebakiwa na Sh. 18,961,106 kwa ajili ya nyongeza za mishahara; itaajiri watumishi 10 na itapewa jumla ya Sh. 2,314,917,441, linaonyesha jedwali.

Miongoni mwa waliodhinishiwa kuajiri watumnishi wengi zaidi ni Polisi (1,351), Magereza (485), Wizara ya Elimu (417), Kilimo (294), Jamii, Jinsia na Watoto (247), Maliasili (152) na Kurugenzi ya Makosa ya Jinai (111).

Wale ambao hawataajiri hata mtumishi mmoja ni Ngome, Mahakama ya Ardhi, Mahakama ya Kazi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Lakini miongoni mwa waliobakiziwa fedha nyingi kwa mujibu wa ukomo matumizi kwa mwaka huu ni pamoja na Ngome (288,708,794,879), Polisi (153,274,299,225), Jeshi la Kujenga Taifa (65,562,775,137), Magereza (60,900,159,845) na Elimu (35,997,981,200).

Kuibuka kwa taarifa ya ikulu kumekuja wakati serikali inadaiwa mabilioni ya shilingi na makandarasi wanaojenga barabara sehemu mbalimbali nchini; madeni ya walimu; kilio cha vyama huru vya wafanyakazi juu ya nyongeze ya mishahara na mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini.

Aidha, upungufu huo wa kifedha, umeibua hofu ya kukwama kwa miradi ya maendeleo na ahadi nyingine zilizotolewa na Rais Kikwete wakati wa kampeni za urais muhula wa pili, zikiwemo ahadi za ujenzi wa barabara za ghorofa, ununuzi wa meli, viwanja vya ndege, bandari na reli.

Vilevile, kupatikana kwa habari hizi kumekuja wiki moja baada ya Rais Kikwete kunukuliwa akisema tatizo la ajira nchini, hasa kwa vijana, ni bomu linaloweza kulipuka muda wowote kuanzia sasa.

Kiongozi mmoja mwandamizi serikalini anasema kufutwa kwa ajira hizo mpya kutazidi kumuweka Rais Kikwete mbali na wananchi wake. Anasema wananchi wengi hawana imani na serikali kwa kuwa wanaona fedha nyingi za umma zinatumika kwenye semina na safari za viongozi.

Kwa mujibu wa waraka wa ikulu wa tarehe 18 Novemba 2011,wenye Kumb. Na. BC. 97/109/014/15, kila mwajiri sasa ametakiwa kuandaa upya mahitaji yake ya ajira kwa kuzingatia ukomo uliotolewa.

Waraka wa ikulu ambao umebeba kichwa cha maneno kisemacho, “Ajira mpya kwa mwaka wa fedha 2011/2012,” umetumwa pia kwa makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa na halmashauri za wilaya.

Miongoni mwa wizara ambazo zitakuwa zimeathirika vibaya na uamuzi huo wa serikali, ni pamoja na tume ya kurekebisha sheria ambayo imepewa mamlaka ya kuajiri wataalam wasiozidi wawili na tume ya haki za binadamu na utawala bora na mahakama ya kazi ambazo zimezuiwa kuajiri kabisa.

Waraka wa serikali unaonyesha pia kwamba katika mikoa mitano mipya iliyotangazwa na serikali mwaka jana, ni mkoa wa Katavi pekee, ambako anatoka waziri mkuu Mizengo Pinda, ulioidhinishiwa kuajiri watumishi wapya. Umeruhusiwa kuajiri wafanyakazi wapya 46.

Haikuweza kufahamika mara moja sababu zilizofanya serikali kuruhusu mkoa wa Katavi peke yake kuajiri na kuacha mikoa mingine mipya bila hata kutajwa.

No comments:

Post a Comment