Wednesday, December 28, 2011

Boti yazama baharini, 20 wahofiwa kufa

Nora Damian
WATU 20 wanahofiwa kufa maji, baada ya jahazi walilokuwa wakisafiria kutoka Mafia kwenda Dar es Salaam kugonga mwamba katika eneo la Nyororo, Bahari ya Hindi. Jahazi hilo lijulikanalo kama Zulkani, lilikuwa na abiria 25.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Ahmed Kilima alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo juzi na kusema ni watu watano tu kati ya abiria wote waliookolewa.

Alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 4:00 usiku na kwamba watu hao watano waliokolewa na chombo kimoja kilichopita eneo hilo. “Bado hatuna taarifa kuhusu watu wengine waliokuwa wamesalia, lakini tunafuatilia na tutatoa taarifa zaidi,” alisema Kilima. Alisema bado kuna tatizo la kuitikia na kutoa msaada pindi yanapotokea majanga akisema hilo ni tatizo la kitaifa.

Ajali hiyo imekuja miezi mitatu baada ya taifa kukumbwa na msiba mzito wa kuzama baharini kwa meli ya MV Spice Islanders Septemba 10 mwaka huu.Mv Spice ilizama katika eneo la Nungwi na kusababisha zaidi ya watu 200 kupoteza maisha huku maelfu wakijeruhiwa na mali nyingi kuteketea baharini. Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Pemba ilizama katika eneo la mkondo wa maji Nungwi.

Mbali ya Mv Spice, ajali nyingine mbaya ya majini ni ile ya MV Bukoba ambayo ilitokea katika Ziwa Victoria eneo la Mwanza Mei, 1996 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800.

No comments:

Post a Comment