Wednesday, December 21, 2011

Waziri kumkimbia Lowassa CCM

Na Alfred Lucas

WAZIRI mmoja mwandamizi ndani ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete, yuko mbioni kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM), imefahamika.
MwanaHALISI limeelezwa kuwa hatua ya kigogo huyo kutaka kuondoka CCM, inatokana na “kukasirishwa na hatua ya rais Kikwete kushindwa kufukuza mafisadi” ndani ya chama chake.
Mtoa taarifa wa gazeti hili ambaye amezungumza kwa sharti la kutotajwa gazetini amesema, waziri huyo tayari ameanza mazungumzo na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yanayolenga kutafuta njia ya kujiunga na chama hicho.
Kwa sasa, gazeti hili linahifadhi jina la waziri mhusika na kiongozi wa ngazi ya juu wa CHADEMA anayesimamia mazungumzo hayo.
Taarifa zinasema waziri anayedaiwa kutaka kuondoka CCM, anaungwa mkono na baadhi ya viongozi wenzake waandamizi wakiwamo wabunge, viongozi wastaafu na wale waliopo madarakani.
Kuibuka kwa taarifa hizi mpya, kumekuja wiki tatu baada ya chama hicho kushindwa kutekeleza mradi wa “kujivua gamba” uliolenga kuwafukuza wanaowaita watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini, ambao wamechangia kukiporomosha chama mbele ya jamii.
Kulingana na taarifa hizo, waziri huyo na kundi lake wamekatishwa tamaa na hali inayoendelea ndani ya CCM na hasa pale chama hicho kilipoamua kurejesha kwenye ngazi ya chini suala la watuhumiwa ufisadi.
“Hapa haifai kudanganyana. Ngoma imekuwa nzito kwa rais na mwenyekiti wetu. Nguvu aliyokuwa nayo awali imeanza kupotea hasa baada ya wajumbe wa kamati kuu kugoma kufukuzwa kwa Lowassa (Edward Lowassa) na wenzake ambao ndio walionadiwa kwa miezi saba kutakiwa kuondoka,” kimeeleza chanzo chetu cha habari.
Mpango uliopo ni kujipanga ikiwemo kuimarisha upinzani ili kuja kuikabili vilivyo CCM wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Unajua, sisi wengine hatuko tayari kuongozwa na Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015. Hatutaki yeye ashike bendera halafu sisi tunamfuata nyuma. Ndio maana tunaondoka mapema ili kukabiliana naye kutokea upinzani,” ameeleza.
Anasema, “Kwa hali ya sasa ya uongozi dhaifu kwenye serikali na chama, hatuamini kama chama chetu kinaweza kumfukuza tena Lowassa. Kuna kila dalili kuwa badala ya kufukuzwa, sasa anatengenezewa njia.”
Tangu kumalizika mikutano ya CCM iliyofanyika Dodoma, wiki tatu zilizopita, mgawanyiko mkubwa na ulio wazi umezidi kuonekana kati ya makundi mawili hasimu ndani ya chama hicho – kundi la watuhumiwa wa ufisadi na wale wanaojiita wapinga ufisadi.
Aidha, tangu kumalizika vikao hivyo, vita vya makundi yanayowania urais vimezidi kushika kasi; baadhi ya viongozi “wakiweka kambi” makanisani kuusaka urais.
Wanaotajwa hadharani kusaka urais, ni pamoja na Lowassa, Samwel Sitta, waziri wa Afrika Mashariki, na Benard Membe, waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.
Hata hivyo, Sitta na Lowassa ndiyo wanaonekana zaidi kutumia makanisa kujijenga kisiasa na wakati mwingine wakipigana vijembe.
Jumapili iliyopita, Sitta aliongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu jijini Arusha, ambako alimtuhumu Lowassa kutumia makanisa kujisafisha.
Akiongea kwa tahadhari, Sitta alisema, “Wananchi mnawatambua viongozi wenu ambao ni waadilifu na pia mnawatambua wale wengine, ambao wanatumia makanisa kujisafisha.”
Sitta alionya waamini wa kanisa hilo kujihadhari na dhambi ya unafiki na kile alichoita, “kusengenyana.”
Sitta hakumtaja Lowassa kwa jina.
Kuhusishwa kwa Lowassa kwenye kauli yake, kunatokana na pale aliposema, “Sitarajii kulitumia kanisa kujisafisha kwa kuwa mimi si mchafu kama wale wengine wanaokuja huku kujisafisha.”
Alisema ingawa anayo mengi ya kusema, lakini hapo si mahali pake. Alisema, “Wananchi mnatujua hata tukisemaje.”
Katika harambee hiyo, waziri Sitta na familia yake walitoa mchango wa Sh. 2 milioni.
Wengine waliochangia, ni waziri mkuu, Mizengo Pinda, aliyetoa kitita cha Sh. 5 milioni, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, aliyetoa Sh. 10 milioni, waziri mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye aliyetoa Sh. 1 milioni na naibu waziri wa viwanda na biashara, Lazaro Nyalandu aliyetoa Sh. 1 milioni.
Nyalandu anayedaiwa kuwa katika moja ya kambi inayowania urais huku yeye akiahidiwa uwaziri mkuu, alitajwa kwenye mkutano huo wa kidini na Sitta, kama kijana mahiri na mchapakazi shupavu.
Kabla ya kuhudhuria hafla hiyo, Nyarandu alihudhuria harambee nyingine katika Kanisa la St. James, ambako Waziri Membe alikuwa mgeni rasmi.
Wakati Sitta akijitokeza kwenye makanisa na kusema hayo, Lowassa tayari ametua kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Amani, mjini Singida, Kanisa Katoliki Parokia ya Nyakato, jijini Mwanza na Kanisa la Anglikana Segerea, jijini Dar es Salaam.
Akiwa Singida, mwanasiasa huyo alichangia Sh. 10 milioni, jijini Mwanza, Sh. 11 milioni na Segerea Sh. 20 milioni.
Akizungumza wakati wa Harambee hiyo iliyofanyika jijini Mwanza, Lowassa alikemea “kulala” kwa serikali akionya tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, ni miongoni mwa mambo yanayoweza kulilipua taifa.
Akirudia kauli yake kuhusu ajira, Lowassa alijifananisha na Yohana Mbatizaji.
Alisema, “Ninapozungumzia hili (uhaba wa ajira) siyo nia yangu kumlenga mtu. Mimi ni Yohana Mbatizaji, hii ni sauti inayolia nyikani.”
Hatua ya Lowassa kuhaha kujisafisha hadi kufikia hatua ya kumchafua Rais Kikwete kuwa anahusika na mkataba tata wa Richmond na hatua ya rais kunyamazia tuhuma hizo, ndiko kunaelezwa na wachambuzi wa mambo kuliko wakatisha tamaa wale wote waliokuwa mstari wa mbele kutaka kiongozi huyo afukuzwe kwenye chama.

No comments:

Post a Comment