Friday, December 2, 2011

RC Kandoro: Ni shetani tu, sina mkono katika vurugu zile

Fujo za machinga Mbeya
 
Felix Mwakyembe
Mbeya
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, amevunja ukimya kuhusu vurugu za Mwanjelwa na kuweka wazi msimamo wake juu ya suala la wafanyabiashara ndogo ndogo, maarufu kama machinga.
Hatua hiyo ya Kandoro ni majibu dhidi ya shutuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kila kunapotokea vurugu za machinga katika mikoa aliyopata kuiongoza, ambayo ni Mwanza, Dar es Salaam na sasa Mbeya.
Akizungumza na viongozi wa madhehebu ya dini ya kikristo jijini Mbeya juma lililopita, Kandoro alisema; “Sijawahi kumwagiza mtu yeyote achukue hatua zilizosababisha ghasia zile. Unapofika mahali unachukua muda kusoma mazingira, nawahakikishia, sina mkono katika vurugu zile, ni shetani tu.”
Pamoja na kukanusha kuhusika na ghasia hizo, Kandoro alibainisha kwamba ni wajibu wao kama viongozi, kukubali changamoto kutoka kwa wananchi ambao kwa sasa kiwango cha uelewa miongoni mwao ni kikubwa.
Pamoja na ukweli kwamba vurugu hizo zilitokea akiwa ndio kwanza anajitambulisha kwenye wilaya na taasisi mbalimbali mkoani humo, mkuu huyo wa mkoa amekuwa akitajwa kutoa maagizo ya hatua za kuchukua. Ni maagizo hayo ndiyo yanayotajwa kuwa chanzo cha vurugu kubwa zaidi.
Wakati ghasia za Mwanjelwa zinatokea Kandoro alikuwa Kamsamba wilayani Mbozi katika ziara zake za kujitambulisha, hata hivyo alilazimika kukatisha ziara yake hiyo na kurudi jijini Mbeya saa kumi alasiri.
Taarifa za awali zilielezea kiini cha ghasia hizo kuwa ni hatua ya askari wa Jiji la Mbeya kuwaondoa kwa nguvu wafanyabiashara hao kwenye barabara inayoingia Kituo cha Afya cha Mwanjelwa na kwenye barabara za pembeni zilizopo eneo hilo.
Hata hivyo, mambo kadhaa yalibainika kujificha nyuma ya ghasia hizo ikiwemo wafanyabiashara wenye maduka wanaodaiwa kuwatumia machinga hao kuwauzia bidhaa zao, na kwa hiyo, kitendo cha kuwaondoa kilionekana kuathiri zaidi biashara zao.
Pamoja ushiriki wa wafanyabiashara hao kuthibitishwa na machinga wenyewe, lakini mazingira pia yanadhihirisha madai hayo, hii ni pamoja na machinga hao kupanga biashara zao kwenye mitaa yenye maduka ya nguo, masanduku ambayo ndio bidhaa maarufu za machinga walioko kwenye mitaa hiyo huku ile yenye maduka ya vifaa vya ujenzi hapo hapo Mwanjelwa ikiwa wazi bila machinga hata mmoja.
CCM lawamani
Mbali ya madai ya wafanyabiashara kuchochea ghasia hizo, baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi katika Jiji la Mbeya wameshutumiwa kuchochea hasira ya vijana jijini humo kutokana na tabia yao ya kuendekeza siasa za chuki, ubabe na vitisho dhidi ya wale wote wanaoonekana kupingana na chama hicho.
Miongoni mwa wanaotupiwa lawama hizo ni kigogo mmoja wa CCM ndani ya uongozi wa jiji hilo anayedaiwa kuvunja sheria alizoshiriki kuzitunga, akidaiwa kuwashawishi vijana kujiunga na chama hicho ili waachiwe kuendelea na shughuli zao.
Ofisa Afya mmoja wa jiji hilo, jina linahifadhiwa, aliliambia Raia Mwema kwamba kigogo huyo huwaeleza vijana wanaoondolewa kwenye maeneo yaliyozuiliwa kuendesha baadhi ya shughuli kama vile uoshaji magari na biashara ndogo ndogo, kuwa wanaondolewa kwa sababu ya kuunga mkono CHADEMA, hivyo ili awaruhusu inabidi wajiunge na CCM.
“Vijana wa pale kwenye car wash za Mafiati, kwa Karumuna, Iyunga na Ujenzi tulikubaliana nao watafute maeneo mengine yanayofaa kwa kazi yao, jiji liwajengee miundombinu ya sehemu ya kuoshea magari, walikubali na wakaondoka, wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani Nzovwe na Majengo wakarudi, tena wakiwa wamepandisha bendera za CCM, tunawauliza wanasema wameruhusiwa na kiongozi mmoja wa kisiasa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, amewaambia waliondolewa kwa sababu ni CHADEMA, wakitaka kurudi wachukue kadi za CCM, vijana wakachukua kadi na kupandisha bendera,” anasema ofisa afya huyo.
Hatua ya watunga sheria wa jiji hilo na madiwani, kuwazunguka watendaji wanapotekeleza uamuzi uliofikiwa kwa pamoja ni kati ya sababu za kuzingirwa kwa askari wa jiji hilo waliofika Mwanjelewa kusimamia eneo la barabara hiyo kutovamiwa tena na machinga, ambapo ikawa sababu ya kuanzisha ghasia.
Kwa mujibu wa ofisa afya huyo wale vijana waosha magari walifikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake, hivyo kuchochea zaidi hasira miongoni mwa vijana hao kwani walibaini kuchuuzwa na mwanasiasa huyo.
Mtazamo wa viongozi dini
Viongozi wa madhehebu ya dini ya kikristo wamechambua sababu zaidi kuhusu ghasia hizo, ambazo ni pamoja na mfumuko wa bei ambao umesababisha maisha kuwa ghali zaidi kiasi cha wananchi walio wengi kushindwa kuyamudu.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Israel Mwakyolile alizitaja sababu nyingi kuwa ni pamoja na kufa kwa viwanda vya nguo (Mbeya Textile), Zana za Kilimo (ZZK) na kiwanda cha sabuni cha Hisop, ambavyo alisema kwa kiasi kikubwa vilikuwa vikichangia kutoa ajira kwa vijana.
Askofu Mwakyolile anasema pamoja na kuwepo kwa rasilimali ardhi na watu, bado kilimo hakiwavutii vijana kutokana na bei duni za mazao ya kilimo, hali inayosababisha vijana wengi wajihusishe na umachinga na baadhi yao hata kufanya vitendo vya uhalifu.
Viongozi hao wamezidi kulia na hatua ya serikali kuyauza mashamba ya Kapunga na Mbarali kwa wawekezaji ambapo wanatoa mfano wa Kapunga wakisema wakati likilimwa na wakulima wadogo lilizalisha zaidi na uchumi kusambaa kwa wananchi walio wengi zaidi.
Wanasema hali ni tofauti sana na hivi sasa ambapo uzalishaji umeshuka na kwamba mwekezaji anadaiwa na baadhi ya wakazi mkoani hapa kuwageuza wananchi manamba wake kwa kuwakodisha mashamba huku yeye akikusanya mapato tu.
Kandoro na machinga
Baada ya ghasia hizo za Mwanjelwa, sasa ni dhahiri kwamba ule mkakati ulioandaliwa tangu mwishoni mwa mwaka jana kuboresha mazingira ya wafanyabiashara ndogo ndogo jijini humo utatekelezwa muda si mrefu kuanzia sasa.
Matumani hayo yalitolewa na Mkuu wa Mkoa huo siku hiyo aliyozungumza na baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini ya kikristo, ambapo katika maelezo yake alibanisha kwamba machinga wapo hata katika mataifa yaliyoendelea hivyo ni suala lisilokwepeka.
“Jiji linajiandaa kuanzisha utaratibu wa kufunga baadhi ya barabara katika muda maalumu ambapo linakuwa eneo la biashara kwa wakati huo, ni utaratibu unaotumika hata na mataifa makubwa kama Marekani, utake usitake machinga ni sehemu ya jamii, unawatoa waende wapi na tukumbuke kuwa wataongezeka,” anasema Kandoro.
Pamoja na utaratibu huo, Kandoro anasema soko jipya la Mwanjelwa linalojengwa hivi sasa litakuwa na mchanganyiko wa wafanyabishara wakubwa, wa kati na wadogo na ni kwa bidhaa zote.
Kwa mujibu wa Kandoro, kipaumbele watapewa wafanyabiashara wale waliokuwepo kabla ya soko hilo kuungua.
Kauli kuhusu Soko la Mwanjelwa ilikuja kutokana na ombi la viongozi hao wa  madhehebu ya dini ya kikristo la kujengwa soko maalumu kwa ajili ya machinga.
Pamoja na Mwanjelwa Jiji la Mbeya liko katika maandalizi ya kujenga soko jingine la kisasa katika eneo lilipokuwepo soko kuu ambalo liliteketea kwa moto Desemba mwaka jana.
Ghasia za machinga wa Mwanjelwa jijini Mbeya zimesababisha hasara kubwa mkoani humo ikiwemo maisha ya watu wasio na hatia, mali, miundombinu hususani barabara kuu iendayo nchi jirani ya Zambia inayopita eneo hilo ambapo imeungua na kuchimbika na kusimama kwa shughuli mbali mbali zikiwemo biashara kwa muda wa siku mbili mfululizo.

No comments:

Post a Comment