Friday, December 30, 2011

Polisi atoweka, akwepa tuhuma

ASKARI Polisi anayedaiwa kuhusika na wizi wa dola za Marekani 50,000 za kidhibiti katika kituo kikuu cha Polisi jijini hapa, ametoroka na familia yake.

Askari huyo (jina limehifadhiwa) anadaiwa kutoroka usiku wa manane wakati Tume maalumu ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Said Mwema, ikiwa inaendelea kuhoji polisi na raia juu ya upotevu wa fedha hizo.

Awali askari huyo, aliwekwa rumande na mwenzake, lakini walipewa dhamana baada ya kuandika
maelezo kwa viongozi hao wa juu wa Polisi mkoani hapa juu ya wizi huo.

Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, alipoulizwa alikiri kuwekwa ndani kwa askari hao, lakini alikataa kutaja majina yao kwa sababu za kichunguzi juu ya suala hilo.

Mbali ya askari huyo kutoweka, askari kanzu mwingine mwenye cheo cha Konstebo (jina tunalo), alikamatwa juzi jioni na anashikiliwa katika kituo kikuu cha Polisi kwa madai ya kufahamu mtandao mkubwa wa wizi jijini hapa na kuhusika na wizi wa fedha hizo.

Mpwapwa alipoulizwa jana kwa njia ya simu juu ya kutoweka kwa askari huyo na familia yake, na mwingine kukamatwa, alisema yeye yuko nje ya mji, labda inawezekana ikawa kweli au la, lakini kwa kuwa yuko nje ya ofisi hilo hatalizungumzia.

‘’Mimi niko Karatu kikazi labda huyo askari alitoroka wakati nikiwa huku na kama kuna mwingine, nikirudi kesho (leo) nitapata taarifa kwa ukaribu zaidi na kupata ukweli wake,’’ alisema Mpwapwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, kukamatwa kwa askari kanzu huyo kulitokana na taarifa kutoka kwa raia wema kuwa askari huyo alihusika moja kwa moja na upotevu wa dola hizo.

Habari zilisema kuwa konstebo huyo piaanadaiwa kumiliki magari ya kisasa jijini Arusha, zaidi ya 10 yakiwamo yaliyokodishwa na mengine kubeba abiria - teksi.

Vyanzo vya habari vilisema kwamba baadhi ya askari kanzu ambao wanafanya kazi karibu na Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Arusha (RCO) ambao walikuwa zamu siku ya upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa nao tayari wamehojiwa na Tume hiyo ya IGP.

Fedha hizo za kigeni sawa na Sh milioni 90 zinazodaiwa kuwa sehemu ya dola za Marekani
200,000 zilizoporwa zilioneshwa mahali ziliko na mmoja wa watu watatu wanaosadikiwa
kuhusika na ujambazi wa kutumia usafiri aina ya pikipiki maarufu jijini Arusha kwa jina la
Toyo ama Bodaboda.

Fedha hizo dola 50,000 ziliyeyukia mikononi mwa polisi katika mazingira ya kutatanisha.

Watuhumiwa hao wa ujambazi walifanya uhalifu huo hivi karibuni kwa kumpora dereva wa gari la hoteli maarufu ya kitalii ya jijini hapa ya Kibo Palace, Onesmo Joseph (28), dola
200,000 sawa na zaidi ya Sh milioni 340.

No comments:

Post a Comment