Tuesday, December 27, 2011

Mbatia ampiku Kikwete


Na Kondo Tutindaga
 
Uchambuzi

WIMBI la migogoro katika vyama vya siasa nchini limezidi kutanda. Inavyoonekana kwa sasa ni kuwa hakuna chama chenye ubavu wa kumcheka mwenzake. Kwa hatua hii, ni vigumu kulisemea kwa usahihi. Kwamba huku dalili ya kukua kwa demokrasia ndani ya vyama au kukua kwa udikteta.
Tumeshuhudia kwa macho yetu vyama vilivyofukuza wanachama kama njia ya kumaliza migogoro kutofanikiwa kutatua migogoro hiyo. Hali kadhalika vile vilivyoshindwa kuwafukuza wanachama wasio na nidhamu pia havikufanikiwa kumaliza matatizo yaliyopo. Kufukuzana au kutofukuzana si suluhisho la migogoro.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kwa miaka mingi kilikuwa kinavizomea vyama vya upinzani kuwa havijakomaa na ndiyo maana vinafukuzana mara kwa mara, kimejikuta katika mgogoro usiokwisha unaotokana na kutaka kuwafukuza wanaowaita mafisadi. Mgogoro wa ndani ya chama hiki ni mkubwa kwa sababu kuu tatu.
Kwanza, ni chama kikubwa na kwa hiyo mgogoro wake lazima uwe mkubwa. Pili, kwa mara ya kwanza, chama hicho kinakabiliwa na ombwe la uongozi kiasi cha hata kushindwa kutunza kumbukumbu za vikao vyake na wakati mwingine kulazimika kutumia magazeti ili kukumbuka kiliamua nini katika vikao vilivyopita.
Tatu, mgogoro ndani ya CCM umegeuka mgogoro ndani ya serikali. Kutumia mtindo wa kufukuzana ni sawa na kuivunja serikali; na kusita kufukuzana ni sawa na kuuboresha mgogoro ili uenee hata katika vyombo vingine na hatimaye nchi nzima. Kimsingi, huu si mgogoro unaoweza kutatuliwa na Rais Jakaya Kikwete tunayemfahamu.
Wimbi hili la migogoro kwa sasa linachemka kwa kasi katika vyama viwili vya upinzani – Chama cha Wananchi (CUF) na chama cha NCCR-Mageuzi. Hivi ni vyama vilivyowahi kuwa vyama vikuu vya upinzani nchini. Vilifanya makosa kadhaa vilipokuwa kileleni na kusababisha kuporomoka kwake.
Baada ya kuporomoka vikafanya kosa jingine linalovigharimu kwa sasa. Vikajiruhusu kuingia katika ubia wa wazi na wa siri na CCM. Ubia huu haujavisadia vyama hivi, badala yake umewatumbukiza kwenye mgogoro mkubwa wa kiimani mbele ya wananchi.
Baadhi ya wanasiasa wazoefu ndani ya CCM wanasema bila kumung’unya maneno kuwa CUF na NCCR-Mageuzi vilifanya makosa makubwa kukiamini chama hicho kwa sababu usaliti wa vyama hivyo kwa agenda ya upinzani ni dalili kuwa vinaweza kukisaliti hata CCM yenyewe. Usaliti huo ndiyo kiini cha fukuzana iliyotokea NCCR- Mageuzi na ndiyo unaoinyemelea CUF.
Ndani ya NCCR-Mageuzi wameweza kuwafukuza uanachama baadhi ya viongozi wake mashuhuri akiwamo mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila; navutika kusema uamuzi huo hata kama haupendwi na wengi, una fundisho muhimu kisiasa.
Mafundisho ya kisiasa yaweza kuwa mabaya au mazuri. Hili la NCCR-Mageuzi lina fundisho zuri kwa CCM. Fundisho hilo linaweza kugeuka kuwa pigo kwa CCM pia.
NCCR-Mageuzi kilikuwa na wabunge wanne tu wa majimbo na wote wanatoka mkoa wa Kigoma. Kwa bahati mbaya wabunge wake hawa wamejikuta ni maarufu kuliko chama chao na maarufu kuliko hata uongozi wa chama chao kitaifa. Umaarufu na ujana ni kama petroli na moto. Yako makosa mengi kisiasa yanaweza kufanywa na wanasiasa vijana waliofanikiwa kuwa maarufu. Hata wabunge hawa wa NCCR wamejikuta katika mtanange huo.
Chama chao kilitegemewa kitambue mgogoro huu na kuwasaidia lakini kimeamua kutanguliza maslahi ya chama kuliko umaarufu wa wanachama wake. Hatua hii ni ya msingi na kwa hili nakipongeza chama hiki. Suala la kama uamuzi huu umefanywa ili kulinda maslahi ya chama au kulinda viongozi walioishiwa mvuto na maono tuliache kwa muda, lakini uamuzi wa kuwapa adhabu wanachama wanaokihujumu chama ni wa kupongezwa.
Wakati CCM kina wabunge zaidi ya mia tatu na madiwani wengi sana, kimeshindwa kufukuza wabunge wake wawili ili kurudisha nidhamu ndani ya chama chake – ambayo imeporomoka tangu awamu ya nne iingie madarakani.
Ndani ya chama hiki, kila mwanachama amegeuka msemaji. Waadilifu ni wasemaji na hata mafisadi wana sauti pia. Imefikia wakati hata viongozi wanaogopa kuitisha vikao kwa sababu ya kutotabirika kwa matokeo ya vikao hivyo.
Mwenyekiti wa chama, Rais Kikwete aliasisi kauli mbiu ya kujivua gamba ili kukinusuru chama na viongozi walio mzigo kwa chama hicho. Lakini wanachama wake wakagawanyika kuhusu azma hii na kumfanya mwenyekiti ama akwepe kuongoza hatua za kuchukua au ajute ni kwa nini alianzisha kauli mbiu hii.
Siyo tu kwamba aligeuziwa kibao na kuonekana yeye pia ni “gamba la kuvuliwa,” ispokuwa vikao vya maamuzi vya chama chake vilimeguka vipande vipande na kukifanya chama kishindwe mpaka sasa kuchukua hatua dhidi ya wanachama wanaokichafua chama hicho mbele ya jamii.
Katika hali ya kushangaza sana, makundi yote yaliyo ndani ya CCM, hakuna hata kundi moja linalopingana na hoja ya kuwa ufisadi umekithiri ndani ya chama hicho. Karibu makundi yote yanakubaliana na malalamiko ya mwenyekiti wao kuwa chama chao kimepoteza mvuto mbele ya wapiga kura kutokana na viongozi walio mzigo kwa chama (mafisadi) na kuna haja ya kuwaondoa ili kukipa chama sura inayowapa watu matumaini mapya.
Kinachoyafanya makundi kutofautiana, ni juu ya nani hasa ni fisadi na mzigo kwa chama. Wapo wanaonyosheana vidole na kutuhumiana kuwa ni mafisadi. Lakini wapo wanaosema makundi yote ni mafisadi ama wa fikra au matendo. Hali hii ndiyo inayoweza kuwa imesababisha kushindikana kuchukuliwa hatua dhidi ya mafisadi.
Kutofautiana maoni juu ya; ni nani hasa fisadi; na nani si fisadi, ni jambo la kawaida katika maisha ya chama cha siasa. Tatizo ni pale inaposhindikana kufikia muafaka na kusonga mbele. Ikitokea hali ya namna hiyo kama ilivyotokea ndani ya CCM, tatizo linakuwa si ufisadi tena, bali uongozi. Chama kikubwa kukosa uongozi ni balaa na kimsingi ni afadhali ya kuwa na chama kidogo kama NCCR-Mageuzi lakini chenye uongozi unaofanya maamuzi.
Hii ndiyo sababu nadiriki kusema kuwa uamuzi wa NCCR-mageuzi kuwafukuza uanachama wake akiwamo mbunge mmoja ni pigo na fundisho kwa CCM.
Kwamba CCM kimeendelea kukumbatia viongozi wabovu katika ngazi zote kwa kutishiwa nyau na viongozi hao kila kinapoonyesha dalili za kuwafukuza au kuwapa adhabu. Wakati mwingine udhaifu wa kiuongozi ndani ya chama hicho umeshindwa kuwachukulia hatua makada wake na kuwaona kuwa ni maarufu sana kuliko chama chenyewe na kuhofia kuwa kikiwafukuza wataondoka na wanachama wengi.
Aidha, CCM kimeshindwa kufanya upembuzi yakinifu na kugundua kuwa umaarufu wa kiongozi wa chama siasa mara nyingi ni pale anapokuwa bado ni kiongozi. Akifukuzwa umaarufu wake hupungua na hata baadhi ya watu aliodhani watamfuata huwa wanaingia mitini na kupotea. Kufukuzwa uongozi ni pigo kwa kiongozi kuliko kuwa pigo cha chama kinachomfukuza hata kama uamuzi wenyewe umefanywa kimakosa.
Hii ni kwa sababu dhamana ya uongozi ikishaondolewa, sababu ya watu kumfuata kiongozi huyo huwa haipo tena. Kimsingi mpaka hapa, CCM inazidi kuwapa umaarufu wanachama wake inaochelea kuwafukuza. Watu hawa wameendelea kuwa maarufu zaidi kuliko walivyokuwa kabla CCM haijatangaza azma ya kuwafukuza.
Kufukuzana ni silaha muhimu hata kama wakwale wanaodai si muhimu. CCM watakuja kugundua siku moja, kwamba kuendelea kukumbatia mafisadi na kuwa na kigugumizi kutawagharimu na hawatakusahau.
Uamuzi uliofanya na NCCR-Mageuzi ni wa kishujaa hata ukiwagharimu huko mbele chama hicho kichanga katika siasa za mizengwe. Kama chama hiki kingeamua kubaki na Kafulila na wenzake kingeendelea na migogoro isiyokwisha na mwisho wa siku kingepotea kwenye lamani ya kisiasa.

No comments:

Post a Comment