Tuesday, December 27, 2011

IGP aingilia kati dola kuyeyukia Polisi

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Saidi Mwema, ameunda Tume maalumu
kuchunguza sakata la upotevu wa fedha za kigeni, dola za Marekani 50,000 (takriban Sh milioni 90) katika mazingira ya kutatanisha katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya kipolisi katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Tume hiyo tayari imeshaanza kazi siku tatu zilizopita na baadhi ya askari kanzu wameshahojiwa juu ya upotevu wa fedha hizo.

Habari zilisema mbali ya askari Polisi wawili waliowekwa ndani kwa kutuhumiwa kuiba fedha hizo na kutoa maelezo yao, pia wako askari wengine wanne wametoa maelezo, lakini hawakuwekwa rumande.

Waliowekwa rumande wako nje kwa dhamana.

Vyanzo vya habari vilieleza kuwa kuundwa kwa Tume hiyo na IGP ni kutokana na majibu ya utata kwa baadhi ya viongozi wa Polisi mkoani Arusha kwa mmiliki wa Hoteli ya Kibo Palace aliyetambuliwa kwa jina moja la Laswai, juu ya upatikanaji wa dola hizo kwani viongozi hao hawatoi ushirikiano kupatikana kwa fedha hizo.

Fedha hizo dola 50,000 zilizooneshwa mahali ziliko na mmoja wa watu watatu wanaosadikiwa kuhusika na ujambazi kwa kutumia usafiri aina ya pikipiki maarufu jijini Arusha kwa jina la ‘toyo ama bodaboda’ zimeyeyukia mikononi mwa polisi katika mazingira ya kutatanisha.

Habari zilisema askari waliokwenda eneo ambako dola ziliko, walirudisha majibu kuwa dola zilizopatikana ni dola 900 tu, hatua ambayo inadaiwa kupingwa na mtuhumiwa wa ujambazi aliyeongozana na askari hao.

Kutokana na utata huo uongozi wa hoteli hiyo ulitaka kujua kwa kina juu ya upatikanaji ama kutopatikana kwa fedha hizo kwa maandishi na sio maneno.

Kwa mujibu wa nakala ya barua hiyo ambayo gazeti hili ilifanikiwa kuiona yenye kumbukumbu
KPH/VOL 1/06-09 ya Desemba 21, mwaka huu kwenda kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, ilitaka kupata ufafanuzi wa maandishi juu ya dola za Marekani 50,000.

Nakala ya barua hiyo iliyosainiwa na R. H. Mbaga kama Meneja wa Utawala yenye kichwa cha habari ''Kukamatwa majambazi watatu na dola za Marekani 50,000,'' inamtaka Kaimu Kamanda kujibu kwa maandishi juu ya kuwa askari hawakukamata kiasi hicho kwa mmoja wa watuhumiwa wa ujambazi kwani Bodi ya Hoteli hiyo haiwezi kufanya kazi kwa mdomo, hivyo inataka maandishi.

“Ni matumaini yangu utatupa majibu kwa haraka ili niweze kuyawasilisha kwa Bodi ya Wakurugenzi kama nilivyoagizwa,” ilisema sehemu ya barua hiyo ya Mbaga.

Ujambazi huo ulifanyika kwa kutumia toyo na kumpora dereva wa gari la hoteli maarufu ya kitalii ya Arusha ya Kibo Palace, Onesmo Joseph (28) dola za Marekani 200,000 (zaidi ya Sh milioni 340).

Awali Mpwapwa alikiri kuwekwa ndani kwa askari hao na kuomba kuacha kutaja majina ya askari hao kwani uongozi wa Polisi unafanya upelelezi zaidi kwa sababu kuna taarifa kuwa kuna askari wengine wamehusika katika tukio hilo la kuiba fedha hizo kama ushahidi kwa watuhumiwa.

“Kwa sasa hata kama unayo hayo majina usiyataje acha kwani ukiwataja wengine wanaweza kuharibu ushahidi na mimi na wenzangu tutakuwa na wakati mgumu wa kuwatia hatiani wengine waliohusika kulichafua Jeshi la Polisi,” Kaimu Kamanda aliliambia gazeti hili wiki iliyopita.

No comments:

Post a Comment