Tuesday, December 27, 2011

Vita vya urais na kimya cha rais


Na Saed Kubenea

MJADALA wa kutafuta mgombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), unazidi kupamba moto. Jarida la Kimataifa la Uchunguzi nchini Uingereza (Economic Intelligence), limesema mrithi wa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2015 atatoka Tanzania Zanzibar.
Jarida halikutaja jina la yule anayedaiwa atakuwa mrithi wa Kikwete na ambaye anatoka Zanzibar. Badala yake, Economic Intelligence limesema mwanasiasa mmoja mashuhuri kutoka miongoni mwa wale waliojitokeza kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005, ndiye atakayekuwa mrithi wa kiongozi huyo.
Pamoja na kwamba hadi sasa, hakuna mwanachama wa chama hicho aliyetangaza hadharani dhamira ya kugombea nafasi hiyo, minong’ono imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku.
Orodha ya wanaotaka kuwania nafasi hiyo ni ndefu. Lakini la muhimu ni hili: Kila anayetamani kuwa rais anasema, “Liwalo na liwe…”
Miongoni mwa wanaotajwa, ni viongozi wastaafu na wale waliopo bado madarakani; mawaziri na naibu mawaziri, rais wa sasa Zanzibar na yule aliyemaliza kipindi chake; makatibu wakuu na mabalozi walioko nje.
Baadhi ya wale wanaoutamani urais, tayari wameunda hadi makundi ya kuwafanyia kampeni – yale ya kumchafua yule na kumjenga huyu. Wengine wameunda hata mitandao ya kupanga safu ya kuingia ikulu. Wengine wameanza safari ya kutembelea baadhi ya mikoa na wilaya ili kutafuta uungwaji mkono.
Wengine wameanza kutafuta viongozi mashuhuri kutoka mikoa yenye wapigakura wengi – hasa eneo la kanda ya Ziwa Viktoria – kushawishi na ikibidi hadi kutumia “nguvu za giza” kutafuta uungwaji mkono. Baadhi yao tayari wameanza kupita mikoani na kujitambulisha kama “rais mtarajiwa.”
Kutokana na hali hii, sasa CCM inaonekana kuwa chama cha migogoro na kilichobeba watu wanaogombea madaraka.
Aidha, kuna wanaokiona kama chama cha watu wenye uchu wa madaraka; na chochote wanachokihubiri hakiwezi kwenda nje ya mstari huo. Wengine wanasema, hata mkakati wa chama kujisafisha, kupitia kilichoitwa “kujivua gamba,” umesukumwa na vita vya urais.
Swali la kujiuliza ni hili: Yuko wapi mwenye uwezo wa kuiokoa CCM kutoka katika hatari ya kusambaratika kutokana na vita hivi vya urais? Njia gani anayoweza kuitumia? Uwezo wake ukoje? Anaungwa mkono na nani?
Jibu ni moja: Anayeweza kuiokoa CCM na hatari ya kusambaratika, ni Rais Jakaya Kikwete pekee. Huyu ndiye mwenye uwezo wa kukinusuru chama hiki. Sababu ni nyingi.
Kwanza, pamoja na udhaifu wa Kikwete na kupoteza mvuto kwake ndani ya CCM, lakini kwa mfumo wa uendeshaji wa chama hiki, uwezo wake wa kuweka mgombea na chama kikabaki salama, bado ni mkubwa. Mgombea yeyote ambaye atakuwa mbali na Kikwete, fursa ya kushinda kinyang’nyiro ndani ya chama hicho ni ndogo mno.
Kikwete anajua kwamba hakuna mwanasiasa hata mmoja ndani ya chama chake, mwenye ujasiri wa kuthubutu kuhama CCM.
Hivyo basi, yeyote atakayetaka kumweka – awe dhaifu au jasiri; awe fisadi au mpinga ufisadi – atapita. Wale wote waliokuwa wamekasirika na wale waliokuwa wamefurahi wataungana kumpigia kampeni.
Hata chaguo lake hilo likishindwa, haitakuwa kwa sababu ya nongwa za ndani ya chama bali itakuwa ni kwa kukataliwa na wananchi. Hii ni kwa kuwa Kikwete anajua kuwa wengi wa wale wenye chuki kali dhidi ya ufisadi, wako nje ya chama chake.
Kwa mfano, Kikwete anafahamu jinsi Samwel Sitta alivyoshindwa kuondoka ndani ya chama hicho mara mbili. Pale alipotaka kufukuzwa hadi akaamua kuunda chama chake – Chama cha Jamii (CCJ), ambacho nacho kiliishia njiani; na pale alipoondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uspika.
Pamoja na kufanya mazungumzo mara kadhaa na Dk. Willibrod Slaa, katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Sitta alishindwa  kupata ujasiri wa kukata minyororo ya CCM.
Hata pale alipoteuliwa kuwa waziri wa Afrika Mashariki, Sitta aliendelea kuwasiliana na viongozi wa CHADEMA na kujiapiza kuwa hataenda kula kiapo cha uwaziri. Dakika chache baadaye alionekana kwenye runinga akiapa kulinda katiba na “kutii rais” aliyemteua.
Naye Edward Lowassa hana ujasiri wa kuthubutu kuondoka. Anachoweza kufanya ni kuishia kulalamika na kisha kufia humohumo ndani. Ni kwa sababu, Lowassa hawezi kukubaliwa na CHADEMA kwa jinsi alivyo sasa.
Angalia jinsi Rostam Aziz alivyokishambulia chama chake wakati alipojiondoa kwenye chama hicho mapema mwaka jana. Alisema ameamua kuondoka ndani ya chama hicho baada ya kuona siasa uchwara zimetawala. Akajiapiza hatakisaidia kwenye kampeni.
Rostam alikwenda ughaibuni kupumzika. Lakini alihudhuria mkutano wa ufunguzi wa kampeni Igunga katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi yake ya ubunge. Ni yeye aliyetafuta na kulipia helkopta iliyotumiwa na CCM jimboni humo.
Lakini kuna hili pia. Pamoja na Kikwete kuwa na uwezo wa kukiokoa chama chake na mpasuko, lakini hana ubavu wa kuwalazimisha wananchi kuchagua mgombea anayemtaka yeye.
Hii ina maana kwamba yeyote anayetaka kumbeba, sharti awe mgombea safi, jasiri na mwenye uwezo wa kuhimili mikikimikiki ya siasa za ushindani.
Wala Kikwete na chama chake, wasije kufanya makosa kuwa mgombea mwanamke au mwanaume kutoka Zanzibar anaweza kunusuru chama.  Ukiondoa Dk. Salim Ahmed Salim, hajapatikana mwanasiasa mwingine mwenye ubavu wa kushindana na wagombea wa vyama vingine.
Hata hivyo, Dk. Salim – miaka sita baada ya Kikwete kuingia madarakani –  serikali ya CCM haijamsafisha Dk. Salim kwa madai ya viongozi wa chama hichohicho kwamba aliua rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.
Hadi leo hii, CCM hakijamsemea kuwa hicho kilichodaiwa hakikuwa na ukweli. Mtoto wa Rais Karume, rais mstaafu Amani Abeid Karume, hadi anaondoka madarakani, hakukana tuhuma kuwa baba yake aliuawa kutokana na njama za Dk. Salim.
Wachunguzi wa mambo ya siasa wanasema huenda viongozi wa CCM hawataki kujisahihisha na kumwondolea tuhuma Dk. Salim kwa kuwa hawataki awe rais.

No comments:

Post a Comment