Thursday, November 17, 2011

Al-Shabab waingia nchini


WATANZANIA 10 wamekamatwa katika maeneo mbalimbali nchini Somalia, wakituhumiwa kushirikiana na kikundi cha kigaidi cha wanamgambo wa Al-Shabab. Aidha, serikali imetahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea kwa mashambulio ya kigaidi nchini, hivyo wananchi kutakiwa kuwa macho na kutoa ushirikiano kwa serikali.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, alitoa tahadhari hiyo jana, alipozungumza na waandishi wa habari juu ya uwezekano wa kutokea mashambulio ya kigaidi kama yaliyotokea nchi jirani za Kenya na Uganda.

Alisema Watanzania hao walikamatwa na wanajeshi wa Kenya walioingia nchini humo wakiwa katika harakati za kuwasaka wanamgambo wa Al-Shabab.
Hata hivyo, alisema baada ya kufanya mawasiliano na Kenya na kukabidhiwa Watanzania hao, walihojiwa na kuchukuliwa taarifa muhimu, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole kisha kuachiwa.
Kwa mujibu wa Nahodha, watuhumiwa hao waliachiwa kwa kuwa taarifa muhimu ziko mikononi mwa vyombo vya usalama, wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Nahodha alisema kutokana na kushambuliwa kwa nchi za Kenya na Uganda, Tanzania haiko salama kwa kuwa wakati wowote linaweza kutokea lolote.
"Tumejiandaa vya kutosha kukabiliana na hali yoyote itakayotokea, lakini ni muhimu wananchi wakatusaidia kwa kutoa taarifa kuhusu mienendo ya watu wanaowatilia shaka," alisema Waziri Nahodha.
Akifafanua jinsi wananchi wanavyoweza kutia shaka mienendo ya watu wasiowajua, alisema ni pamoja na kuhoji mambo na kutaka kupata taarifa ofisi za kibalozi na maeneo mbalimbali ya ofisi nchini.
Mbali na hilo, alisema endapo watajitokeza raia wa kigeni wanaowarubuni vijana kwa kuwadanganya watawapeleka nje ya nchi na kuwapatia kazi watoe taarifa haraka, kwani ni moja ya viashiria vya magaidi hao.
"Kukamatwa kwa vijana hao na kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji haramu kutoka nchini Somalia, yote hayo yanaashiria uwezekano wa kuingia Al-Shabab na kufanya vitendo vya kigaidi," alisema.
Alisema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za mienendo ya hali ya usalama, kulinda mipaka na kushirikiana na nchi jirani kukabiliana na ugaidi.
Wakati huo huo, Waziri Nahodha, alisema amepata majina manane ya maofisa wa juu wa Idara ya Uhamiaji nchini wanaotajwa zaidi kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Kutokana na hilo, alisema amewaeleza maofisa hao kuhusu tuhuma hizo ili wakae wakijijua pamoja na kuwapa muda wa mwezi mmoja kujirekebisha kabla ya hatua dhidi yao hazijachukuliwa.
Hata hivyo, hakutaja majina ya maofisa hao kwa maelezo kwamba muda wa kufanya hivyo bado haujafika.
Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana na serikali kuwafichua wahamiaji haramu wanaoingia nchi.
Kwa upande wa serikali alisema imechukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuwatimua nchini raia wawili wa Pakistan waliokuwa vinara wa uingizaji wageni kinyume cha taratibu.
Kikundi cha Al-Shabab kimekuwa tishio kwa ulinzi na usalama wa nchi za Afrika Mashariki, kutokana na mashambulizi kadhaa yaliyofanyika katika nchi za Kenya na Uganda.
Hivi sasa Kenya inaendelea na mapambano na kuwatafuta wafuasi wa Al-Shabab katika maeneo mbalimbali, ikiwemo nchini Somalia.

No comments:

Post a Comment