Kamanda mkuu wa kikosi cha Umoja wa mataifa cha kulinda amani nchini Sudan, amesema kuwa jeshi la nchi hiyo lilihusika na shambulio la anga dhidi ya kambi moja ya wakimbizi iliyoko nchini jirani ya Sudan Kusini.
Akiongea na BBC, kamanda huyo Herve Ladsous amesema Umoja wa mataifa umethibitisha kuwa ndege za serikali ya Sudan, zilirusha mabomu katika kambi hiyo ya wakimbizi siku ya alhamisi.Ladsous amesema wamepokea habari nyingi kutoka kwa wale walioshuhudia tukio hilo, kuthibitisha kuwa jeshi hilo la Sudan lilifanya mashambulio hayo ya mabomu.
Lakini msemaji wa serikali ya Sudan, Khalid al Mubarak, amekanusha madai hayo na kusema kuwa serikali yake haikufanya mashambulio ya mabomu katika kambi hiyo ya wakimbizi nchini Sudan Kusini.
Kamishna mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na haki za kibinadam Navi Pillay, ameitisha kufanyika uchunguzi huru kufuatia tukio hilo.
Awali, shirika moja la marekani lilidai kuwa serikali ya Sudan ilikuwa ikikusanya wanajeshi wake katika kituo kimoja cha kijeshi karibu na mpaka wake na Sudan Kusini, madai yaliyopingwa vikali na utawala wa Khartoum.
No comments:
Post a Comment