Thursday, November 17, 2011

OCD wa Arusha kikaangoni

Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD) Zuberi Mwombeji
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD) Zuberi Mwombeji
 
Achunguzwa kuhusu kauli ya panya
Watu 700 wajitokeza kutaka kumshitaki
Lema alakiwa na maelfu akitoka lupango
WAKATI waandamanaji waliokuwa wakiupinga  utawala wa kiongozi wa muda mrefu wa Libya, Muammar Gaddafi, walipoibuka kwa mara ya kwanza, kiongozi huyo alishindwa kuchagua  maneno  ya staha katika hotuba yake na badala yake alitumia kejeli kwa kuwafananisha  wapinzani wake kuwa ni kama “panya na mende” wanaotumiwa na nchi za kigeni.
Maandamano ya kumtoa  madarakani  Gaddafi  yalianza mapema Februari mwaka  huu wakati zilipoibuka vurugu za kisiasa  nchini mwake na baadaye kugeuka kuwa vita iliyomwondoa madarakani na hatimaye kuuawa na waasi ambao awali aliwaita panya.
Wakati dunia ikiwa imeshaanza kusahau kauli hiyo ya Gaddafi baada ya kifo chake, mjini Arusha yameibuka madai mazito dhidi ya Kamanda wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD)  Zuberi Mwombeji anayedaiwa kutoa lugha mbaya  ya kuwaita wananchi  ”panya”  na  tayari amefunguliwa jalada la uchunguzi na Polisi kuhusu kauli yake hiyo.
Kutokana na kauli hiyo anayodaiwa kutoa Mwombeji ambayo imezua mgogoro mkubwa baina yake na wananchi hasa wafuasi na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao ndio wanaodaiwa kulengwa, ”upepo mbaya” umeanza kuvuma dhidi yake na huenda akachukuliwa hatua za kinidhamu iwapo madai hayo yatathibitishwa.
OCD Mwombeji anadaiwa kutoa kauli hiyo mbaya Oktoba 28 mwaka huu ndani ya ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha wakati wa usikilizwaji wa kesi inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Arusha Godbless Lema (CHADEMA) iliyofunguliwa na wanachama watatu wa CCM.
Pamoja na kufunguliwa jalada hilo Kamanda huyo wa Polisi pia huenda akakabiliwa na mashitaka kutokana na hatua ya wananchi zaidi ya 700 kutia saini hati maalumu ya kupelekea maombi mahakamani kufungua kesi dhidi yake kwa kumtumia wakili wa kujitegemea  kwa kauli yake hiyo.
Chanzo cha kauli hiyo

Taarifa za awali zilizofikia Raia Mwema  zinaeleza kuwa Mwombeji alitoa kauli hiyo  ndani ya ukumbi wa Mahakama Kuu wakati wa usikilizwaji wa kesi ya Lema akijaribu kuwatoa nje ya ukumbi wananchi waliokuwa wamejazana kwa lengo la kusikiliza kesi hiyo.
Akizungumza na Raia Mwema mmoja wa walioshuhudia tukio hilo ambaye  ni kada  maarufu  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyeomba jina lihafadhiwe, alieleza kuwa siku hiyo ukumbi ulikuwa umefurika hatua iliyosababisha mawakili wa upande wa mashitaka na ule wa utetezi kukataa kuendelea na kesi hiyo hadi watu watakapopunguzwa ndani ya ukumbi.
“Kutokana na maombi hayo ya mawakili wa pande zote ndipo Polisi wakiongozwa na OCD Mwombeji  walipoanza jitihada za kuwataka watu waondoke ndani ya ukumbi wa Mahakama  ili kesi iendelee lakini watu wengi walipinga hatua hiyo ndipo Mwombeji alipomwambia Lema  awatoe “panya wake” ndani ya ukumbi  akimaanisha wafuasi wake”, alieleza kada huyo wa CCM.
Kada huyo  aliongeza kuwa kwa kauli hiyo OCD Mwombeji alirushiana maneno makali na Mbunge Lema ndani ya ukumbi huo na nusura  washikane mashati hadi walipoamuliwa huku Lema akimtaka kamanda huyo afute kauli hiyo.
Baada ya mvutano huo kesi hiyo iliahirishwa na Lema aliondoka  eneo la Mahakama kwa miguu  hadi ofisini kwake katika majengo ya Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Arusha  huku akiambatana na umati mkubwa wa wafuasi wake waliokuwa wanamfuata  nyuma.
Hata hivyo, wakati mbunge huyo akiwaaga wafuasi wake hao ghafla walivamiwa na Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia waliokuwa kwenye magari  wakioongozwa na OCD Mwombeji ambapo pamoja na kupigwa virungu watu kadhaa walikamatwa na kesho yake walifunguliwa mashitaka ya kufanya maandamano bila ya kibali pamoja na Mbunge  Lema.
Kufunguliwa kwa kesi hiyo ndicho kiini cha Lema kukataa dhamana Mahakamani na kuamua kwenda  mahabusu kwa hiari yake mwenyewe kupinga kila alichokiita kuwa ni unyanyasaji na uonevu unaofanywa na OCD Mwombeji akitumia Jeshi la Polisi.
Uamuzi huo wa Lema ulifuatiwa na mlolongo wa matukio  kadhaa ya uvunjifu wa amani ambapo wafuasi wake walifanya vurugu kushinikiza migomo ya magari yanayotoa huduma za usafiri wa umma.
Taharuki kubwa iliukumba Mji wa Arusha Novemba 7 mwaka huu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi kukataa ombi liliwasilishwa na wakili wa Lema, Method Kimomogoro, la kutaka kumtoa Lema kutoka mahabusu kwa hati ya dhamana ya dharura (remove order).
Kwa uamuzi huo  wa Mahakama, uongozi wa juu wa CHADEMA ulifanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Viwanja vya NMC na kutangaza ulichokiita kuwa mkesha wa ukombozi  ambao hata hivyo, ulivunjwa na Polisi alfajiri ya  Novemba 8 na vingozi wa juu wa chama hicho walikamatwa na kufikishwa kortini.
Waliofunguliwa mashitaka ni pamoja na Katibu Mkuu Dk.Willbrod Slaa, wenyekiti Freeman Mbowe, Mbunge wa  Singida Kaskazini Tundu Lissu na wafuasi wengine 27.
Polisi kufungua jalada

Lakini  sasa upepo wa sakata hilo umenza kumgeukia OCD Mwombeji ambapo  taarifa za hivi karibuni zilizothibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa,  zilieleza kuwa Kamanda Mwombeji  tayari meshaandika maelezo yake mbele ya Makamishana watatu wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu.
Makamishna hao ambao walikuwa mjini Arusha wiki iliyopita kujaribu kumshawishi Lema akubali kutoka mahabusu ni pamoja na Paul Chagonja,  Naibu DCI Peter Kivuyo na Simon Sirro.
Kamanda Mpwapwa alieleza kuwa ni kweli suala hilo limefunguliwa jalada la uchunguzi kufahamu ukweli wake kama OCD huyo alitoa kauli ya aina hiyo  na baada ya uchunguzi huo Jeshi la Polisi litatangaza hatua za kuchukua.
“Kwa sasa ni mapema mno kuzungumzia suala hilo na kulitolea majibu ila taarifa hizo tunazifanyia kazi na tutaujulisha umma kitakachofuata baada ya uchunguzi wetu kukamilika,” alisema Kamanda Mpwapwa.
Majibu ya Mpwapwa hayakueleza uchunguzi huo utachukua muda gani, utakuwa ni wa kiwango gani na kama utaweza kutenda haki kwa mantiki kuwa anayechunguzwa ana wadhifa mkubwa katika Jeshi la Polisi.
Taarifa zaidi hapa zinasema ili kuweka mambo shwari, huenda OCD Mwombeji kahamishwa hiyo ikimsaidia yeye binafsi lakini pia ikiweka mambo sawa kwa viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakimlalamikia.
Hayo yakiendelea wananchi zaidi ya 700 wametia saini hati ya kutaka kufungua mashitaka dhidi ya OCD Mwombeji.
Taarifa zinaeleza kuwa hadi juzi Jumatatu waliosaini hati hiyo ni watu zaidi ya 700 na lengo la wanaharakati wanaondesha mpango huo ni kupata saini za watu 2000 ili wafungue kesi itakayosimamiwa na mwanasheria wa kujitegemea (jina linahifadhiwa).
Mmoja wa waratibu wa mpango huo, Ephata Nanyaro, ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CHADEMA Mkoa wa Arusha (Bavicha) alisema wanatarajia kukamilisha kazi ya kukusanya saini za watu wanaohitajika kabla ya mwisho wa wiki hii na wiki ijayo mwanasheria wao atawasilisha hati ya mashitaka mahakamani.
“Hadi sasa kila kitu kinakwenda vizuri, tumekwishakukusanya saini za wananchi zaidi ya 700 na tunarajia kukamilisha kazi hiyo kabla wiki hii kumalizika na baada ya hapo wiki ijayo mwanasheria atakamilisha hati ya kuwasilisha mashitaka mahakamani dhidi ya OCD Mwombeji,”alisema Nanyaro.
Hii si mara ya kwanza kwa OCD Mwombeji kuingia matatani. Alilalamikiwa sana wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kutokana na kupigwa mabomu ya machozi kwa misafara ya  kampeni za mgombea wa CHADEMA wakati huo, Godbless Lema alilalamikiwa pia na CHADEMA  kwa madai ya kuingilia mchakato wa uchaguzi wa nafasi ya Umeya, Desemba 18, 2010 baada ya kuingia ukumbi wa mikutano wa Manispaa na kumtoa kwa nguvu Lema  kisha kumpa kipigo kilichomfanya alazwe Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru. Lema alidaiwa alikuwa anafanya vurugu ndani ya ukumbi.
Tukio hilo lilifuatiwa na vurugu za Januari 5, mwaka huu wakati CHADEMA kilipoitisha maandamano makubwa kupinga uchaguzi wa Meya. Maandamano hayo yalivunjwa na Polisi, yakiacha marehemu watatu na watu wengine zaidi ya 30 wakijeruhiwa vibaya huku kwa mara nyingine  OCD Mwombeji akinyooshewa kidole  akidaiwa kuwa chanzo.
Lema atoka gerezani

Jumatatu wiki hii, katika hatua nyingine, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilitoa dhamana kwa Lema baada ya kutimiza masharti ya dhamana huku yeye akiahidi kuendeleza kile alichokiita kuwa ni mapambano ya ukombozi.
Mbunge huyo wa CHADEMA  aliletwa mahakamani hapo majira ya saa 3:20 asubuhi akiwa ndani ya gari maalumu  la Polisi lenye namba PT 1178 na alipewa dhamana na Hakimu Mkazi Judith  Kamara, baada ya kukamilisha taratibu  na  masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini  wawili wenye vitambulisho na barua za utambulisho ambao walisaini hati  ya dhamana ya shilingi milioni tano kila mmoja.
Baada ya  kukamilisha dhamana yake  Lema  alitoka nje ya Mahakama  saa 5:20 akapokewa kwa shangwe  kwa kubebwa  juu  na umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wamefurika  nje ya viwanja  vya Mahakama hivyo kuanzia saa mbili  asubuhi na waliondoka eneo hilo kwa maandamano makubwa hadi ofisi za CHADEMA Mkoa wa Arusha zilizopo Ngarenaro katika Manispaa ya Arusha.
Msafara wa Mbunge huyo ulipita katika Barabara ya Uhuru kuelekea Ngarenaro na kusababisha shughuli nyingi za kibiashara kusimama kwa zaidi ya saa moja kutokana na uwingi wa watu waliokuwa wamebeba matawi ya miti kuashiria amani.
Waandamanaji  hao walikuwa wanaimba nyimbo mbalimbali  kama:
“Tunamtaka….panya wetu…tunamtaka mbunge wetu…Zuberi (OCD) aondoke...mlituvizia usiku, leo sasa ni mchana, hapatatosha. Hatuandamani, tunampokea shujaa wetu,”.
Tofauti na misafara mingine ya aina hiyo, wa juzi uliachwa uende bila kuingiliwa na Polisi waliokuwa wanalinda amani wakioongozwa na Kamanda wa Operesheni Maalumu za Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Peter Mvulla.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika ofisi za  chama hicho  Lema alisema suluhu ya mgogoro wa Arusha  itapatikana kwa uchaguzi wa umeya kurudiwa na kumuonya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo kuacha kuingilia masuala asiyoyafahamu akisema kufanya hivyo ni sawa  na  kudandia gari asilojua  mwelekeo wake akimaanisha mgogoro  unaoendelea.
Mbunge huyo  alidai kuwa  ni wazi  Serikali inakisaidia chama tawala katika mgogoro  wa nafasi ya umeya na akaongeza kuwa yu tayari kujiuzulu nafasi yake ili kuruhusu uchaguzi mdogo akiahidi kunyakua tena kiti hicho kwa kura nyingi zaidi ya 56, 196  alizopata kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.
Kuhusu kauli aliyodai ya vitisho kutoka kwa Mulongo aliyeonya wanaopanga kuvuruga amani na utulivu Arusha, Lema alisema kiongozi huyo bado anakabiliwa na ‘ushamba’ wa Bagamoyo ndiyo maana anatoa kauli bila kuzifanyia utafiti na kuanza kuibua chembechembe za ukabila kwa kusema wanaondamana Arusha si wenyeji wa Mkoa huu.
"Maisha yangu si kwa ajili ya kuishi leo, bali kufa kwa faida. Ndiyo maana kila siku nasema ni heri vita inayotafuta haki, kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mtu," alisema Lema huku akishangiliwa.

No comments:

Post a Comment