Saturday, November 26, 2011

Madiwani CHADEMA, CCM wala njama kumpindua Meya Moshi

Meya wa Moshi
Meya wa Moshi

ULEVI  wa madaraka umeanza kukisumbua  Chama cha Demokrasia  na Maendeleo (CHADEMA)  katika  Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro Kutokana na mgogoro  wa chini kwa chini unaofukuta  miongoni mwa madiwani wa  chama  hicho wanaotaka kufanya mapinduzi ili kumwondoa madarakani Meya, Michael Jaffary.
Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka 2010, CHADEMA kilishinda nafasi ya ubunge kwa kishindo katika Manispaa ya Moshi kwa Philemon Ndesamburo kuwabwaga washindani wake.
Chama hicho pia kilishinda  viti  vya   udiwani katika  kata 17 kati ya 21 vya Chama cha Mapinduzi hivyo CHADEMA kupata fursa ya kuongoza halmshauri hiyo.
Hata hivyo, pamoja na kupata mafaniko hayo katika kile kiinachoonekana kuwa ni kulewa madaraka baadhi ya madiwani wanadaiwa kuanza kusuka mipango ya kumwondoa Meya katika nafasi yake, wakimtuhumu kuwa hakidhi mahitaji ya kisiasa ya chama na wananchi wa Manispaa ya Moshi.
Taarifa zilizolifikia Raia Mwema mjini Moshi na baadaye kuthibitishwa na vyanzo kadhaa zilieleza kuwa madiwani wanaoongoza harakati za kutaka kumwondoa Meya huyo wametoka katika kata tatu za manispaa hiyo na mwingine wa viti maalumu pamoja na wale wa Chama cha Mapinduzi.
Habari zaidi zinaeleza kuwa madiwani hao wanajenga hoja kuwa Meya Michael Jaffary alihusika na operesheni ya kuvunja vituo vya kuoshea magari (car wash) iliyofanyika miezi mitatu iliyopita. Katika operesheni hiyo zaidi ya vituo 20 vilivyunjwa na askari wa manispaa hiyo.
Vituo hivyo ni vile vilivyojengwa kinyume cha utaratibu na sheria zinazosimamia mipango miji kwa kujengwa katika makazi ya watu, hifadhi ya barabara na maeneo yenye majengo ya umma kama shule.
Manispaa ya Moshi iliendesha operesheni ya kuvunja vituo hivyo vya kuoshea magari katika kata za Bondeni, Mawenzi, Kilimanjaro na Kiusa na operesheni hiyo ilitekelezwa usiku wa manane kwa kutumia askari wa manispaa hiyo
Akizungumza na Raia Mwema moja wa madiwani  wa CHADEMA katika Wilaya ya Moshi (jina linahifadhiwa) alisema wanazo taarifa za uhakika kuwa madiwani hao wamekuwa wakifanya vikao katika hoteli moja mjini hapa kupanga mipango ya kumwondoa meya  madarakani.
“Ni kweli kuna madiwani wenzetu  wameungana na wale wa CCM kusuka mipango ya kumwondoa meya katika nafasi yake na tayari taarifa hizo tunazo na tumeshaanza kuzifanyia kazi,” alisema diwani huyo.
Kiongozi huyo alisema kuwa sababu nyingine inayotolewa na madiwani hao ni hatua ya Manispaa ya Moshi kuvunja pia baadhi ya majengo yaliyojengwa bila kufuata taratibu za ujenzi katika maeneo ya miji.
“Wao wanadai kuwa hatua ya kuvunjwa kwa vituo hivyo vya kuoshea magari na pia baadhi ya majengo kutaondoa umaaarufu wa chama hicho mkoani Kilimanjaro  hivyo meya awajibishwe kwa kuruhusu kuvunjwa kwa vituo hivyo,” alisema.
Diwani huyo alisema baada ya kufanya vikao vya kusuka mpango huo madiwani hao wamekuwa wakiendelea kufanya ushawishi kwa madiwani wengine ili hoja  ya kumwondoa meya itakapoletwa basi iungwe mkono na madiwani wengine.
“Kinachowasukuma hao madiwani ni uroho wa madaraka tu kwani  hoja zao hazina mashiko na masuala wanayoyatetea hayana msingi wala maslahi kwa wananchi wa mji wa Moshi,” aliongeza diwani huyo katika mazungumzo yake na gazeti hili.
Mwenyekiti wa Madiwani wa CHADEMA katika Manispaa hiyo, Jomba Koi, alikanusha kuwapo kwa mgogoro wowote na kumtaka mwandishi wa RaiaMwema kuachana na habari za aina hiyo.
“Mimi ni mwenyekiti wa madiwani na hatuna mgogoro wowote ila nakushauri uachane na habari za aina hiyo haina maana yoyote zaidi ya kuleta hali ya vurugu ndani ya chama,” alisema Koi.
Akizungumzia madai hayo Meya wa Manispaa hiyo Michael Jaffary alishindwa kuthibitisha au kukanusha njama hizo za kutaka kumuondoa katika wadhifa huo.
“Siwezi kuzungumzia hatua hiyo ila nataka nikueleze kuwa kutofautiana kimtazamo ni masuala ya kawaida katika uongozi wa umma na ninachoweza kusema tofauti zilizopo ni za kimtazamo tu ila suala la kutaka kuniondoa madarakani siwezi kulisemea,” alisema meya huyo.
Alisema uamuzi wa kuvunja vituo vinavyolalamikiwa ulifikiwa na vikao halali vya halmashauri na wala si uamuzi wake binafsi hivyo wanaoalalamika kama wapo walikuwa pia sehemu ya uamuzi huo wa pamoja katika halmashauri.
“Mimi kama Meya siwezi kujiamulia majengo na mali nyingine za wananchi zivunjwe ila hayo ni maamuzi (uamuzi) halali yaliyofikiwa katika vikao vya halmashauri hivyo anayelalamika kuhusu mimi atakuwa hanitendei haki,” alisema.
Kuhusu kuvunjwa kwa baadhi ya majengo Meya huyo alisema kimsingi uamuzi huo pia ulifikiwa katika vikao vya Baraza la Madiwani na hatua hiyo inatokana na matayarisho ya maombi ya mji huo kutaka kuwa jiji.
“Unajua tumejiwekea malengo ya kuugeuza mji wa Moshi kuwa jiji katika kipindi cha miaka miwili ijayo kuanzia sasa na moja ya sifa zinazotakiwa ni mji kuwa katika mpangilio unaokubalika hivyo Baraza la Madiwani limeazimia kukomesha ujenzi holela usiozingatia sheria za mipango miji,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo, hakuwa tayari kuzungumzia mgogoro huo akisema bado haujafikishwa rasmi ofisini kwake.
“Sisi ngazi ya mkoa bado hatujapata rasmi taarifa hizo lakini naomba ungeacha kwanza kuandika suala hilo hadi hapo tutakapokutana kwa vikao rasmi na unajua migogoro hii inapokuwa kwenye media (vyombo vya habari) haileti picha nzuri na unavuruga chama,” alisema Ndesamburo ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini.
Naye Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, alikuwa na maoni tofauti na Ndesamburo akieleza kuwa kutofautiana kwa madiwani hao ni hatua nzuri katika kukuza wigo demokrasia ndani ya chama chao.
“Sisi kama mkoa bado hatujapata rasmi malalamiko dhidi ya meya au madiwani lakini kama madiwani wanaona kuna dosari miongoni mwao na wakazungumza si jambo baya bali ni katika kupanua wigo wa demokrasia ndani ya chama chetu,” alisema Lema.
Alisema hata hivyo malalamiko hayo yakiwasilishwa yatashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kichama na muafaka wake utapatikana kwani CHADEMA ni chama kilichokomaa na kimeshakumbana na matatizo ya aina hiyo.

No comments:

Post a Comment